Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokutana na Makatibu
Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini Ikulu jijini
Dar es salaam na kuwataka kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi,
nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
WATANZANIA wanauanza mwaka mpya wa 2016 leo huku wengi wakiwa na shauku ya kujua hatma ya mambo kadhaa yakiwamo ya kuanza kwa utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuingia Ikulu.
WATANZANIA wanauanza mwaka mpya wa 2016 leo huku wengi wakiwa na shauku ya kujua hatma ya mambo kadhaa yakiwamo ya kuanza kwa utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuingia Ikulu.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, Magufuli
aliyekuwa akipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliibuka
mshindi baada ya kuzoa asilimia 58.46 ya kura zote halali zilizopigwa na
hivyo kuwaacha wapinzani wake saba, akiwamo Edward Lowassa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyekuwa akichuana naye kwa karibu
katika kipindi chote cha kampeni.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia mahojiano na wachambuzi
mbalimbali wa masuala ya siasa, uchumi na jamii umebaini kuwa yapo mambo
takriban tisa ambayo Watanzania wengi wanatarajiwa kuyafuatilia kwa
karibu ili kujua kitakachotokea. Kwa kiasi kikubwa, mambo hayo
yamejikita katika Nyanja za siasa, uchumi na kijamii.
Katika uchunguzi wake, Nipashe imeyabaini mambo hayo kuwa ni
utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kwa kila mtoto wa Tanzania kuanzia
shule ya msingi hadi kidato cha nne; mchuano wa wabunge watokao CCM na
wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema,
Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi; kuendelea kwa mchakato wa
katiba mpya; hatma ya Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo yake ya
uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25; athari za kuendelea kushuka kwa bei
ya mafuta katika soko la dunia; kuendelea kuporomoka kwa thamani ya
shilingi dhidi ya dola ya Marekani; tishio la mvua kubwa za el-nino kwa
usalama wa chakula na miundombinu na pia mustakabali wa utitiri wa
magari ya kifahari maarufu kama ‘mashangingi’ katika taasisi na
mashirika ya umma.
Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
“Kuanza kwa mwaka huu ni muhimu kwa historia ya Tanzania kwani kuna
matumaini makubwa ya kuanza utekelezaji wa ahadi kubwa za serikali ya
awamu ya tano ikiwamo ya utoaji wa elimu bure, ujenzi wa fly-overs,
mpango wa kugawa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa na pia
ujenzi wa zahanati katika kila kijiji,” alisema mmoja wa wachambuzi
waliozungumza na Nipashe.
Ahadi elimu bure, zahanati kila kijiji
Utekelezaji wa ahadi kuu za serikali ya awamu ya tano ni mojawapo
ya eneo linalotarajiwa kufuatiliwa na Watanzania kwa karibu mwaka huu.
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, Magufuli aliwakuna wengi kutokana na
ahadi zake kuhusiana na uboreshaji wa huduma za jamii kama elimu, afya
na maji. Karibu katika kila eneo alilofika na kufanya mikutano yake ya
kampeni, Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itabeba jukumu la kutoa
elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne na kwamba,
hakutakuwa na mchango wowote kwani anapoahidi elimu anamaanisha ‘ni bure
kweli’ pasi na kuwasumbua wananchi kwa michango itokanayo na kisingizio
chochote kile.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliamuru kuwa Sh. bilioni 136
zilizotokana na mapato yaliyovunja rekodi ya Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi
yaliyokusanywa na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) zielekezwe katika sekta
ya elimu ili kuanza utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kuanzia Januari,
2016. Kadhalika, mwaka huu serikali inatarajiwa pia kutoa mwelekeo wa
namna ya kuanza kwa utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa zahanati katika
kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata, hospitali ya wilaya katika
kila wilaya na kuwapo kwa hospitali ya rufaa katika kila mkoa. Mpango
wa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji nchini kwa kasi mpya ya
serikali ya awamu ya tano inayobebwa na kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ ni
eneo jingine linalotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu. Ahadi nyingine
maarufu zitakazofuatiliwa kwa karibu ni ya kutoa milioni 50 kwa kila
kijiji na kila mtaa na pia ujenzi wa barabara za juu (flyovers) kwa nia
ya kupunguza foleni za magari katika makutano ya barabara kuu kama za
Mandela na Nyerere jijini Dar es Salaam. Ipo pia ahadi ya kuanzishwa
kwa mahakama ya kushughulikia ufisadi, ikibebwa na kauli ya Magufuli
katika mkutano mmojawapo wa kampeni pale aliposema: “Nitasimamia
uundwaji wa Mahakama ya kushughulikia mafisadi na majizi wa nchi hii ili
wafungwe.”
Siasa za CCM, Ukawa kuhamia bungeni
Hakika, hili ni eneo jingine linalosubiriwa kwa hamu mwaka huu.
Baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015, sasa joto la
kisiasa linatarajiwa kuhamia katika vikao vya Bunge la 11 ambavyo
vitaanza Januari 27, 2016. Kuongezeka kwa idadi ya wabunge wa vyama vya
upinzani vinavyounda Ukawa, ambao sasa wamefikia 121, kunatarajiwa
kuongeza mchuano baina yao na wabunge wa chama tawala, CCM.
Mchakato wa katiba mpya
Baada ya kukwama kwa mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya katika
serikali ya awamu ya nne, sasa wwali kubwa linalotatiza wengi ni lile la
kutaka kujua kwamba je, Serikali ya Magufuli itaendelea pale katiba
hiyo iliposhia kwa kuruhusu upigaji kura wa wananchi kwa katiba
inayopendekezwa au mchakato utaanza tena upya kwa kukusanya maoni nchi
nzima kama ilivyofanywa na kamati maalumu iliyoongozwa na Jaji mstaafu
Joseph Warioba? Hili ni jambo linalotarajiwa kupatiwa majibu mwaka huu.
Hatma ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar
Tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim
Jecha, afute uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo Oktoba 28, 2015, kumekuwa na
mgogoro mzito wa kisiasa baina ya pande mbili kuu, yaani chama tawala
(CCM) kinachosisitiza kuwa uamuzi wa Jecha uheshimiwe kwa kurudia
uchaguzi huo na CUF kinachotaka mchakato wa majumuisho ya kura uendelee
kwani hakukuwa na kasoro kubwa za kuufuta uchaguzi huo wote hasa baada
ya kusifiwa na waangalizi wa ndani na wa kimataifa kuwa ‘ulikuwa huru na
wa haki’.
Hadi sasa, mazungumzo yamekuwa yakiendelea baina ya CCM chini ya
mgombea wake wa urais, Dk. Ali Mohamed Shein na CUF inayoongozwa na
mgombea wake wa nafasi hiyo ya urais, Maalim Seif Shariff Hamad. Je,
nini hatma ya mazungumzo hayo na mustakabali wa Zanzibar baada ya hapo?
Wengi wanatarajia kupata majibu mwaka huu unaoanza leo.
Kushuka bei ya mafuta katika soko la dunia
Eneo jingine linalotarajiwa kuangaliwa kwa jicho la karibu na
Watanzania walio wengi ni pamoja na athari za kiuchumi zitokanazo na
kuporomoka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia. Wapo wanaotaka
kujua kama kushuka huko kwa bei ya mafuta kutaleta matokeo ya kuonekana
kwa uchumi wa nchi na pia kwa mtu mmoja mmoja.
Kwa mfano, wakati serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete ikiingia
madarakani kwa mara ya pili mwaka 2005, pipa moja la mafuta ghafi
katika soko la dunia lilikuwa likiuzwa kwa wastani wa dola za Marekani
90. Hata hivyo, bei hiyo iliendelea kuporomoka siku hadi siku na hadi
kufikia jana, pipa moja la mafuta ghafi, kwa mujibu wa Shirika la habari
la Reuters, lilikuwa likiuzwa kwa dola za Marekani 37.18.
Swali kubwa linalotarajiwa kuwa vichwani mwa wengi ni kwamba je,
Serikali ya Magufuli itawezesha vipi wananchi wa kawaida kunufaika
kiuchumi kutokana na kushuka huko kwa bei ya mafuta katika soko la
dunia? Uchumi mpana utaathiriwa vipi na anguko hilo la bei ya mafuta
kila uchao?
Kuporomoka kwa thamani ya shilingi
Kati ya mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na athari hasi za
kiuchumi ni kuporomoka kila uchao kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola
ya Marekani.
Kwa mfano, wakati serikali ya Rais Kikwete ikiingia madarakani kwa
mara ya kwanza mwaka 2005, dola moja ya Marekani ilikuwa ikibadilishwa
kwa wastani wa Sh. 1,162.23; mwaka 2010, dola moja ilikuwa ikibadilishwa
kwa wastani wa Sh. 1,410.22 lakini kufikia jana, kwa mujibu wa taarifa
za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), dola moja hubadilishwa kwa Sh. 2,159.21.
Watanzania wengi wanatarajia kuona serikali ya awamu ya tano ya Rais
Magufuli ikitafuta njia bora ya kudhibiti kasi ya kuporomoka kwa
shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Tishio la mvua za el-nino
Kwa mujibu wa ripoti za mamlaka mbalimbali za hali ya hewa ikiwamo
TMA, Tanzania ni miongoni mwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zeney
uwezekano wa kukumbwa na baa la mvua za el-nino.
Kama hofu hiyo itakuwa ya kweli, hasa kutokana na mwelekeo wa hali
ya hewa, maana yake ni kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais
Magufuli itakumbana na changamoto ya kuandaa mikakati ya kukabiliana na
athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na mvua za el-nino.
Mvua za aina hiyo ziliponyesha mwaka 1998, taifa lilikumbana na
athari kubwa za kuharibika kwa miundombinu ya usafiri kama reli na
barabara, madaraja yalisombwa na majengo kadhaa kuliharibiwa. Aidha,
mvua hizo kubwa huathiri uzalishaji wa chakula na hivyo kuibua hofu ya
kuwapo kwa njaa. Tishio hilo la el-nino ni miongoni mwa mambo
yanayotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu mwaka huu wa 2016.
Mustakabali wa ‘mashangingi’ serikalini
Wakati akilihutubia Bunge la 11 kabla ya kulizindua Novemba 20,
2015, Rais Magufuli alisisitiza dhamira ya serikali yake kuhakikisha
kuwa matumizi ya magari ya serikali yanadhibitiwa, hasa yale ya
‘kifahari’ aina ya VX-V8 maarufu kama mashangingi. Kinachosubiriwa na
wengi kuanzia leo, ni kuona kama matumizi ya magari hayo yatasitishwa
rasmi ama la.
Mchakato wa Magufuli kutwaa uenyekiti CCM
Baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM na baadaye kuibuka
mshindi, Magufuli anatarajiwa kutwaa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho
ili kutimiza dhana ya ‘kofia mbili’, yaani Rais kuwa vilevile ndiye
mwenyekiti wa chama hicho. Kwa mujibu wa katiba ya CCM, Rais mstaafu
Jakaya Kikwete bado anastahili kushikilia wadhifa huo hadi mwaka 2017.
Hata hivyo, desturi ya chama hicho ya kuzingatia dhana ya ‘kofia mbili’
inampa Magufuli nafasi ya kuwa mwenyekiti kabla Kikwete kumaliza muda
wake. Hivyo, hili ni eneo mojawapo linalotarajiwa kuangaliwa kwa karibu
ili kujua mwelekeo mpya wa chama tawala chini ya uenyekiti wa Rais
Magufuli.
WASEMAVYO WANASIASA KUHUSU MWAKA MPYA
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliiambia Nipashe
kuwa mwaka ulioisha jana wa 2015 ulikuwa ni mzuri kwa kuwa uchaguzi
ulimalizika salama pasipo kuwa na fujo na wao kuaminiwa na Watanzania
kuendelea kuongoza.
Aliongeza kuwa kwa mtazamo wake, mwaka 2015 ulikuwa ni wenye matukio mengi mazuri na machache mabaya.
Mwenyekiti wa Chama Cha United Peoples Demokratic Party (UPDP),
Fahmi Dovutwa, alisema mwaka uliopita ulikuwa ni wa changamoto kubwa
kisiasa kutokana na kuwapo kwa uchaguzi mkuu na kwamba, muhimu
linalopaswa kuzingatiwa kwa mwaka unaoanza leo ni kuendelea kutunzwa kwa
amani ya nchi.
Katibu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alisema mwaka 2015 ulikuwa
ni mwaka wa mafanikio kwa chama chao kwa kuwa walifanikiwa kusimamisha
mgombea urais katika uchaguzi mkuu na mwishowe wakafanya vizuri kwa
kushika nafasi ya tatu.
Katika uchaguzi mkuu, ACT ambacho ni chama kipya, kilipata mbunge
mmoja, madiwani 51 nchi nzima, pamoja na kuongoza halmashauri ya Kigoma
Ujiji na kupata meya.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema
mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka mzuri kwao kwani walipata wabunge wengi
kulinganisha na chaguzi zilizopita na hivyo, mwaka huu wataendeleza
harakati zao za kujiimarisha zaidi na mwishowe kujiongezea wanachama.
Mbunge Waitara baada ya kusikiliza taarifa hizo kutoka kwa diwani
na kwa mwenyekiti wa shule, alisema kuwa atafika Ofisi za Ilala na kesho
atafanya mkutano wa hadhara ili wanakijiji wafahamu hali halisi ya eneo
hilo.
No comments:
Post a Comment