TTCL

EQUITY

Saturday, January 30, 2016

MALI ZA BILIONI 11/- ZATAIFISHWA NCHINI.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga
JESHI la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP), limetaifisha mali zenye thamani ya Sh bilioni 11 zilizopatikana kwa njia ya uhalifu baada ya kushinda kesi zinazowakabili wahusika.
Kesi hizo ni zile za mwaka jana na mwaka huu, zinazohusu rushwa, ujangili, dawa za kulevya na usafirishaji wa binadamu. Pia taasisi hizo zimetangaza rasmi vita dhidi ya wahalifu wote, wanaojipatia mali kwa njia ya uhalifu.
Aidha, vyombo hivyo vya dola, vimebainisha kuwa kupitia Sheria ya Uharamishaji Fedha zinazotokana na Uhalifu ya Mwaka 1991 iliyoanza kutekelezwa mwaka 2012, vitahakikisha mtu yeyote bila kujali cheo chake wala uonevu, atakayebainika kuwa na mali zilizotokana na uhalifu, pamoja na kupewa adhabu kwa mujibu wa Mahakama pia, mali zake zitataifishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, alisema fedha hizo zimepatikana kutokana na kesi mbalimbali zilizoendeshwa nchini, ambazo washtakiwa pamoja na kutaifishwa, pia walihukumiwa vifungo.
Alisema hatua hiyo ilifanikishwa kupitia Kitengo cha kuharamisha na kufuatilia mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu, kilichoanzishwa rasmi kwa ajili ya kushughulikia na kufuatilia mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu ili kuzitaifisha na kuzirejesha serikalini.
Alisema kitengo hicho kilishirikiana na Jeshi la Polisi, Takukuru na ofisi ya DPP pamoja na wadau wengine kutoka nje ya nchi, ikiwemo Benki ya Dunia kushughulikia kesi mbalimbali za rushwa, dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na kufanikiwa kutaifisha mali, ambazo sasa ni za Serikali.
Alisema katika kipindi hiki kitengo hicho kimepata amri kutoka Mahakama Kuu na Mahakama za chini na kutaifisha magari ya kifahari, fedha taslimu, akaunti za benki na nyumba vyote vyenye thamani ya Sh bilioni 11 kutokana na kesi zinazohusu makosa hayo ya uhujumu uchumi.
Alitoa mfano wa mali zilizotaifishwa ni kiwanja kilichopo jirani na eneo la Ocean Road ambacho pamoja na mmiliki kujenga na baadaye kubomoa nyumba, tayari ameshindwa kesi na kiwanja hicho kimetaifishwa na sasa ni mali ya Serikali.
Alitaja baadhi ya kesi ambazo tayari zimeshughulikiwa na Mahakama kutoa amri ya wahusika walipe faini kuwa ni kesi iliyokuwa ikimkabili raia wa Marekani, John Galant ya uhujumu uchumi ya mwaka jana na Jensen Mubarak, raia wa Qatar.
Alisema tayari Galant amehukumiwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 30,000, sawa na Sh milioni 64.2, kama ilivyokuwa kwa Mubarak. Aidha, alisema kesi nyingine ni inayomhusu raia wa Kuwait, Hussein Mansour aliyekamatwa uwanja wa ndege akiwa na kobe 173 ambaye pamoja na kifungo, amehukumiwa kulipa Dola za Marekani 24,220 sawa na Sh milioni 54.10.
Alisema David Marais na Matinus raia wa Afrika Kusini, katika kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka jana, walikutwa na meno manne ya mamba na jino moja la kiboko, na kuhukumiwa kulipa Dola za Marekani 32,000 sawa na Sh milioni 68.1 na tayari wamelipa.
“Pia kuna kesi iliyowakabili raia wa China walioshtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi huko Mbeya kwa kukutwa na meno 11 ya kifaru walioingia nayo kutoka Malawi, sasa wamefungwa miaka 20, walitakiwa walipe Shilingi bilioni 9.2 lakini wameshindwa kulipa hivyo wanatumikia kifungo cha miaka 20,” alisisitiza.
Alisema pia gari lao Toyota Surf T103 DER, limetaifishwa tayari na ni mali ya Serikali. Aidha, mkoani Tanga katika kesi ya uhujumu uchumi pia magari mawili aina ya Rav 4 na Suzuki, yote mapya, yalitaifishwa, na Dar es Salaam magari matatu.
Mganga alisema katika kesi ya usafirishaji wa binadamu iliyokuwa ikiwakabili raia wawili wa India pamoja na kutakiwa kulipa kiasi cha Sh milioni 15, pia walitaifishwa magari yao matatu yaliyokuwa yakitumika kusambazia wasichana kwa ajili ya shughuli za ukahaba.
Maganga alisema pamoja na kwamba kuna madai kuwa Serikali haishughulikii kesi za dawa za kulevya, lakini juzi mjini Moshi, kesi mbili za dawa ya kulevya zilitolewa hukumu, ambazo washtakiwa wote walihukumiwa kifungo cha maisha.
Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mkenya, Joseph Mungy aliyehukumiwa kwa kosa la uhujumu uchumi kwa kukutwa na kilo 3.2 za dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya Sh milioni 162. Amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Kesi nyingine ni ile iliyomkabili Musa Ramadhani na Hamis Sulya, waliokutwa na dawa za kulevya aina ya heroine yenye thamani ya Sh milioni 143, wote wamehukumiwa kifungo cha maisha na mali zao zinahitajika zitaifishwe.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alisema kutokana na mkakati huo, ambao vyombo hivyo vitatu vya dola vimejiwekea, Polisi imekamilisha upelelezi wa kesi 23 zilizowasilishwa na DPP.
Alisema kati ya kesi hizo, tatu zimeshatolewa uamuzi, 20 zilizobaki ziko kwenye hatua ya maombi ya kupata amri ya Mahakama ili zizuiwe au kutaifishwa. Mali zinazohusiana na uchunguzi wa kesi hizo ni nyumba, viwanja, magari, boti na fedha taslimu.
Aliwataka wananchi, kushirikiana bega kwa bega na Polisi katika kutoa taarifa za mali zilizopatikana kwa njia ya kifisadi ;huku akiwahakikishia juu ya suala la usiri na ulinzi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria. “Nawahakikishia wananchi Polisi itaendelea kulinda taarifa zitakazotolewa na wananchi kwa mujibu wa sheria.
Ndugu zangu nchi yetu tutaijenga wenyewe endapo tutashirikiana kudhibiti uhalifu huu,” alisisitiza. Alisema tayari vyombo hivyo vya dola vimebaini kuwa wahalifu wengi wa mali hutumia majina ya wake, waume, watoto na wakati mwingine ya watu wasiokuwepo ili kuendelea kufaidika na mali walizozipata isivyo halali.
“Nawaomba wananchi msijihusishe kwa hali yeyote ile kuficha umiliki wa mali ya mtu mwingine kwa kudanganywa au kurubuniwa. Kwani kwa mujibu wa Sheria aliyeshiriki kuficha mali ya mtu mwingine inayohusiana na uhalifu kwa njia yoyote ile anaweza kushtakiwa kama aliyetenda kosa la ufisadi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Takukuru, Alex Mufungo, alisema vyombo hivyo vitatu sasa vimejipanga na mwelekeo wake ni kutaifisha mali zinazopatikana kwa uhalifu.
“Azimio letu si kufunga mtu tu hiyo haitoshi, bali sasa tutaanza kutaifisha mali,” alisema. Aliwataka Watanzania kuanza kuchukia uhalifu wa mali na kuwachukia wale wote wanaojipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwa kuwafichua ili wachukuliwe hatua.

No comments:

Post a Comment