VYAMA vya chadema na chama cha ACT-Wazalendo vimelaani vikali hatua ya Serikali
kusitisha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kurusha matangazo ya
moja kwa moja katika vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.
Vimesema hatua hiyo ya Serikali inaonyesha wazi kuwa imedhamiria kuendesha nchi kidikteta.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Kaimu
Katibu Mkuu wa Chadema (Taifa), Salum Mwalimu alisema hoja zilizotolewa
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye za
kusitisha matangazo hayo hazina mashiko na hazina uhalisia na kitaaluma.
Alisema tamko hilo la Waziri Nape limekiuka Katiba ambayo inaeleza wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kupata habari.
Mwalimu alisema Chadema pia wanamtaka Waziri Nape alete uchambuzi
namna ambavyo Sh bilioni 4.2 zinatumika kutokana na vipindi hivyo vya
Bunge.
“Nimefanya kazi kwenye vituo vya televisheni, lakini kila nikichambua
sioni uhalisia wa gharama hizo, hivyo ni lazima atuchambulie
zinatumikaje,” alisema.
Alisema pia wanamtaka ataje utafiti aliousoma unaodhihirisha kwamba
muda wa saa nne usiku unafaa kurushwa kwa matangazo hayo yatakayokuwa
yamerekodiwa ili wananchi waweze kuyafuatilia.
“Awali itakumbukwa kwamba wakiwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa na Waziri Nape walipiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama
vya siasa kwa maelezo kwamba waachwe wale walioshinda katika uchaguzi
mkuu wafanye kazi huku ni kukiuka sheria ambayo inaruhusu vyama kufanya
mikutano ya hadhara.
“Lakini kama hiyo haitoshi, baadaye Jeshi la Polisi nalo lilitoa
tamko lao ambalo lilikazia tamko lile lililotolewa na Serikali la kupiga
marufuku mikutano ya hadhara,” alisema.
Alisema wakitazama hata namna ambavyo kamati za Bunge zilivyoundwa
zinaonyesha wazi nia ya Serikali kutaka kujilinda dhidi ya maovu yake.
“Kama tatizo ni fedha za kuwalipa TBC watueleze, watupe na hizo gharama
zinazohitajika, tupo tayari kuhamasisha wananchi kwa kufungua akaunti
maalumu ili wasaidie kuchangia kupatikana kwa fedha hizo za kulipia
matangazo.
Kwa upande wake, Chama cha ACT-Wazalendo kuputia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba jana, kilisema uamuzi huo wa Serikali ni aibu na ni hatari kwa ustawi wa nchi inayoendeshwa kidemokrasia.
“Tunalaani tukio la aibu katika nchi yetu pale Serikali ilipofanya
jaribio la hatari la kuzuia wananchi kuona na kusikia kinachoendelea
bungeni.
“Kitendo cha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzuia kuonyeshwa
moja kwa moja vipindi vya Bunge katika televisheni ya Taifa ni cha
kijima na sisi ACT-Wazalendo tunakilaani kwa nguvu zetu zote,” alisema
Mwigamba katika taarifa hiyo.
Alisema wanakitafsiri kitendo hicho cha Serikali kama mwendelezo wa
hatua na juhudi za Rais Dk. John Magufuli za kuminya demokrasia na
kusimika utawala wa kiimla.
KAULI YA MOAT
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania
(MOAT), Henry Muhanika akizungumzia na MTANZANIA juu ya hatua ya
Serikali kusitisha matangazo ya TBC, alisema hatua hiyo imewashtua wadau
wa habari nchini.
“Ukweli ni kwamba hatua hiyo imetushtua na kamwe haijatufurahisha kwa
sababu matangazo ya moja kwa moja yana umuhimu wake katika kufikisha
ujumbe kwa wananchi.
“Ukiondoa kipindi cha maswali na majibu, kuna kipindi kingine ambacho
huenda matangazo yake yatahaririwa na wakati mwingine yatatoa picha
nyingine tofauti na vile ambavyo watu wangeshuhudia moja kwa moja,”
alisema.
Muhanika alisema inasikitisha kuona kwamba hatua hiyo imekuja hivi
sasa wakati ambao unaandaliwa muswada wa habari kwa ajili ya watu kupata
haki ya kupata habari.
“Hii inapunguza lengo na hatujaelewa kwa nini imekuwa hivi kwa sababu
utaratibu huu unakuja wakati huu na hatuna uhakika nini kitatokea baada
ya hapo. Tunajiuliza ikiwa TBC imeshindwa kurusha moja kwa moja kwa
kuwa inategemea kodi za wananchi je, vyombo vingine vitaruhusiwa? Jambo
hili linatutia wasiwasi juu ya uhuru wa habari nchini,” alisema.
No comments:
Post a Comment