TTCL

EQUITY

Saturday, January 30, 2016

KESI YA MHANDO WA TANESCO YACHUKUA SURA MPYA.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando.
 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema itatoa uamuzi Februari Mosi, mwaka huu, kuhusu mabishano ya kisheria yaliyotokana na upande wa Jamhuri kupinga nyaraka za aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, kupokewa kama kielelezo.
 
Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Kwey Rusema, baada ya kusikiliza ushahidi wa utetezi wa Mhando.
 
Mhando aliomba kuwasilisha nyaraka zinazoonyesha kufuatwa taratibu za zabuni mahakamani hapo kama kielelezo.
 
Hata hivyo, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alipinga nyaraka hizo kupokewa kama kielelezo hali iliyosababisha mabishano ya kisheria kwa pande zote mbili.
 
Hakimu Rusema alisema mabishano hayo yatatolewa uamuzi Februari Mosi, mwaka huu.
 
Mbali na Mhando, washtakiwa wengine ni anayedaiwa kuwa mke wake, Eva Mhando, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Santa Clara Supplies, wahasibu wafawidhi wa Tanesco, France Mchalange, Sophia Misidai na Ofisa Ugavi, Naftali Kisinga.
 
Jana kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri.
 
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 31, mwaka 2011 katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco, Dar es Salaam, Mhando akiwa mwajiriwa kwa nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, alitumia vibaya mdaraka yake.
 
Ilidai kuwa Mhando alitumia vibaya madaraka yake kwa kuangalia maslahi yake binafsi baada ya kuipa zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kampuni inayongozwa na mke wake, Eva na watoto wake, vyenye thamani ya Sh. milioni 884.5 na kuisababishia kampuni hiyo kupata faida ya Sh. 31,747,000 kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment