Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salum Jecha.
Umoja wa Ulaya (EU) umeiweka Tanzania njiapanda
baada ya kutoweka wazi msimamo wake juu ya uamuzi wa kurudiwa kwa
uchaguzi mkuu wa Zanzibar na iwapo watatuma waangalizi au la.
Kwa mujibu wa taratibu, Nchi za Ulaya, Afrika na Jumuiya zake,
hutuma waangalizi mbalimbali kwenye uchaguzi unaofanyika katika nchi
mbalimbali ili kujiridhisha na mwenendo wa uchaguzi husika.
Nipashe ilitaka kujua maoni ya EU baada ya Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salum Jecha, kutangaza kurudiwa uchaguzi
mkuu wa Masheha, Wawakilishi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kuwa utafanyika Machi 20, mwaka huu.
Kadhalika, Umoja wa Mataifa, Marekani na Jumuiya ya Afrika
Mashariki, zimekuwa kimya katika kueleza kama zitapeleka waangalizi
katika uchaguzi huo, ambao Chama cha Wananchi (CUF), wametangaza
kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
Msemaji wa EU nchini, Susanne Mbise, alisema juzi kuwa Umoja huo
hauwezi kueleza chochote kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa
sasa na kama watapeleka waangalizi kama ulivyofanya katika uchaguzi wa
Oktoba, mwaka jana au la.
“EU haiwezi kutoa maoni yoyote kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar,
pia kutuma waangalizi,” alisema katika majibu aliyotuma kwa mwandishi wa
gazeti hili.
Aidha, msemaji huyo alisema kuna taarifa ya uongo inasambaa kwenye
mitandao ya kijamii ikieleza kuwa EU imetangaza nafasi za kazi ya
waangalizi katika marudio ya uchaguzi huo.
Katika taarifa yake, EU imekanusha vikali tangazo la kutafuta
waangalizi lililosambazwa kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp na
facebook wanaotumia nembo ya EU, na kwamba hawaitambui taasisi hiyo na
tangazo hilo la kazi.
“Pia timu ya waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM)
haina taarifa za taasisi hiyo na tanagzo la kazi. Haitafuti watu wa
kufanya kazi ya uangalizi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa,”
alifafanua.
Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, EU EOM ilitoa wito kwa
ukamilishwaji wa haraka wa mchakato wa uchaguzi Zanzibar kulingana na
kanuni za uchaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na
kuaminika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwangalizi Mkuu wa EU EOM,
Judith Satgentini, alisema “EU EOM iko tayari kurejea nchini kuangalia
mchakato wa uchaguzi Zanzibar pindi makubaliano ya kuendelea
yatakapofikiwa".
Mwenyekiti wa Zec, Jecha alitoa tamko la kufutwa kwa uchaguzi mkuu
wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, baada ya kueleza kasoro tisa
zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Tamko hilo limezidi kuigusa jumuiya ya ndani na ya kimataifa huku
wengi wakiomba serikali ya Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati
kumaliza hali hiyo.
Mwaka jana, Marekani ilikwishandika barua serikali ikisihi uchaguzi
huo kukamilishwa kwa kufuata matakwa ya Wanzanzibari ili Tanzania iweze
kuongeza vigezo vya kupatiwa msaada wa dola za marekani milioni 472.8
sawa (Sh. bilioni 993) kutoka Shirika la Maendeleo la Changamoto za
Milenia (MCC), kwa ajili ya ukuzaji wa sekta ya nishati.
Hata hivyo, kutokana na kushindwa kufikiwa matakwa hayo, Tanzania ikikosa fedha hizo.
Kumekuwa na mvutano baina ya chama tawala (CCM) na chama kikuu cha
upinzani visiwani humo (CUF). Katika mvutano huo, CUF inataka kutangazwa
kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, ambao mgombea urais wake, Maalim
Seif Sharif Hamad, alijitangaza mshindi kwa kupata kura 200,007 dhidi ya
178,363 alizopata mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein.
Wakati mazungumzo ya maridhiano baina ya Maalim Seif na baadhi ya
viongozi wa CCM yakiendelea, alizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, Januari 19, mwaka huu, na kutangaza kujitoa.
Mpaka anajitoa, Maalim Seif, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, marais
wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zainzibar, Balozi Seif Ali Iddi, walikuwa
wamekutana mara tisa kwa nyakati tofauti katika vikao hivyo ambavyo
vilikuwa vimetawaliwa na usiri mkubwa.
Kutokana na sintofahamu hiyo, mataifa makubwa kama Marekani, na
Denmark, yalisusia sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika
Januari 12, mwaka huu.
Katika uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana,
waangalizi wa nje, wakiwamo EU na UN, walitoa tamko la kuridhishwa na
mwenendo wa uchaguzi na kueleza ulikuwa huru na haki. Pia waangalizi wa
ndani walisema ulikuwa huru na haki.
CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment