TTCL

EQUITY

Friday, January 1, 2016

Fahamu yaliyojiri Tanzania mwaka 2015

Kumaliza mwaka salama si jambo dogo hata kidogo, ni jambo kubwa na la kumshukuru Mungu aliyeipigania nchi yetu ikavuka salama kiuchumi kisiasa na kijamii.
Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambayo inasifika kote ulimwenguni ambapo mwaka huu nchi ilikuwa na mtihani mkubwa na dunia nzima ilikuwa ikiimulika nchi hasa katika uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge pamoja na Madiwani.
Ni mwaka ulioanza kwa matukio mazito kadhaa ya kukatisha tamaa ambapo itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa mwezi wa tatu zaidi ya watu 42 walifariki dunia wengine 91 kujeruhiwa na wengine zaidi ya 900 kukosa makazi kutokana na mvua ya mawe na upepo mkali katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Wakati hayo yakiendelea suala la uzembe wa madereva, unywaji wa pombe, uchakavu wa magari na miondombinu viliteketeza mamia ya watu kwa ajali za barabarani na kuacha wengine walemavu pamoja na uharibifu wa mali.
Mwaka huu pia umekua ni wa majonzi kwa kuwapoteza ndugu jamaa na marafiki na kwa upande wa kisiasa wabunge wengi walipoteza maisha kutokana na maradhi mbalimbali na ajali akiwemo aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi Kapten John Komba, Mbunge wa ukonga Eugen Mwaiposa, Mbunge wa Geita Donald Max, Mbunge wa Ulanga Mashariki Celina Kombani, Mbunge wa Handeni Abdalla Kigoda, na Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe.
Ni mwaka ambao pia matukio ya kikatili dhidi ya watoto yalibainika mfano kituo kimoja huko Pasua Moshi kilikutwa kikiwa kimewaficha watoto 13 wakipatiwa mafunzo ya siri bila ya wazazi wao kujua, huku katika maeneo mengine watoto wakiripotiwa kuchomwa moto ,kubakwa na kulawitiwa. Wakati huo huo wenye ulemavu wa ngozi, wazee na kinamama wakongwe nao walikubwa na maswahibu katika maeneo mbalimbali na kusababisha vifo na majeruhi.
Vilevile kwa upande wa polisi hali nayo haikuwa shwari sana ambapo vituo kadhaa vilivamiwa na askari kuporwa silaha, kuuawa na vituo vingine kuchomwa moto mfano kituo cha polisi Ikwiriri mkoani Pwani pamoja na Sitakishari Jijini Dar es salaam.
Hali ya wananchi juu ya utii wa sheria bila shuruti nayo haikueleweka kwa wananchi wengine ambapo matukio mengi yaliripotiwa na la hivi juzi juzi ni la kuuawa kikatili kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita Alfonce Mawazo kwa kukatwakatwa mapanga na lingine la meneja wa Zantel Gabriel Kamukara aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana juzi.
Migogoro ya wakulima na wafugaji nayo ilishika hatamu katika maeneo ya Kiteto mkoani Manyara na Kilosa mkoani Morogoro na kusababisha vifo na majeruhi kwa binadamu pamoja na ng'ombe zaidi ya 150 kukatwakatwa kwa mapanga kwa lengo la kulipiza pamoja na uchomwaji wa nyumba na mali.
Katika hatua nyingine nchi ilivuka kihunzi kilichoshinda nchi nyingi kwa kufanya uchaguzi mkuu wa kihistoria, uchaguzi uliofanya dunia nzima iitazame Tanzania baada ya vyama vyenye nguvu kisiasa vya CHADEMA, NLD, NCCR kuungana kwa pamoja na kuongoza mashambulizi ya maneno na sera nchi nzima dhidi ya chama tawala CCM.
Ambapo hadi mwisho wa kampeni wananchi wakaamua kukirejesha chama cha mapinduzi kupitia kwa Dr. John Pombe Magufuli aliyepata kura milionin 8 sawa na asilimia 58.46% dhidi ya mpinzani wake wa karibu kupitia umoja wa katiba ya wananchi Edward Lowassa aliyepata kura milioni 6 sawa na asilimia 39.97%.
Wakati Tanzania bara ikiendelea na shughuli zake chini ya serikali ya awamu ya tano kisiwani Zanzibar hadi sasa majadiliano yanaendelea baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzbar hadi hapo utakapo tangazwa tena.
Katika kile kilichoitwa kutumbua majipu, Rais Dr,Magufuli akabaini upotevu wa mabilioni ya shilingi kwa kupitishwa kwa makontena zaidi ya elfu 10 bandarini bila kulipiwa ushuru, pia akakomesha safari za nje na vikao visivyo vya lazima na kuwabana watendaji wazembe ambapo kwa muda mfupi akaweka rekodi ya kukusanya shilingi trilioni 1.3 huku waliosababisha ubadhirifu huo wakitiwa hatiani.
Hata hivyo katika kuonyesha njia, pia rais alikataa sikukuu ya kupata uhuru tarehe 09 desemba mwaka huu kutofanyika gwaride na halaiki ila ufanyike usafi nchi nzima na fedha zilizotengwa shilingi bilioni 4 zitumike katika ujenzi wa barabara kutoka Moroco hadi Mwenge jijini Dar es salaam ujenzi ambao tayari umeanza.
Hata hivyo tukio la funga mwaka ambalo lilikusanya vyombo vyote vikubwa vya ulimwengu ni watu watano waliofukiwa na kifusi katika mgodi wa Nyangata kukaa siku 41 mgodini wakila vyura na mende na kutoka wakiwa hai.
Hakika mambo ni mengi sana yaliyofanyika kwa mwaka huu, katika kila nyanja ambayo mengi yalitia moyo huku mengine yakiumiza hivyo ni wajibu wa kila mmoja kumshukuru Mungu na kuzidi kudumisha amani na mshikamano uliopo nchini.

No comments:

Post a Comment