“INAWEZEKANA kujiajiri kwa mtu mwenye ulemavu hasa wa viungo, ingawa
kuna changamoto nyingi kutokana na hali halisi ya kimaumbile, pamoja na
kutokuwa na mtandao wa watu wenye fedha wanaoweza kutoa mitaji ili
angalau mwenye ulemavu aanzishe shughuli itakayomuingizia kipato...”.
“Kwa ufupi, ulemavu si umasikini.
Inawezekana mtu mwenye ulemavu akajiajiri au kuajiriwa na kufanya
kazi yenye matokeo mazuri kama yanayoletwa na mtu mwingine yeyote asiye
na ulemavu. Jambo kubwa linalopaswa kutazamwa ni namna atakavyopata
mtaji ajiajiri. Kuwa mlemavu wa viungo haimaanishi kuwa ni kukosa uwezo
wa kufanya kazi”.
Mjumbe wa Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) wilayani Kahama,
Edward Charles ndiye anayesema maneno hayo na kuweka wazi kuwa, watu
wengi wenye ulemavu hasa wa viungo wanakuwa wamejaaliwa maarifa ya aina
mbalimbali yanayohitaji kutumiwa kwa njia tofauti ili mchango wao katika
nchi uwe na manufaa kwa wengine.
Anasema, lakini kutokana na kukosa uwezo wa mitaji, wanashindwa
kutumia maarifa yao ipasavyo hivyo kujikuta wakipoteza muda kutaka
wasaidiwe kwa kuomba omba, kana kwamba maisha ya kujishughulisha na
kujitengenezea ajira au kuajiriwa hayapo katika upande wao. Charles ni
mlemavu wa miguu anayejishughulisha na ushonaji na ung’arishaji viatu
katika wilaya ya Kahama.
Anasema wenye ulemavu wa viungo wanaweza pia kufanya kazi, kutegemea
na aina ya ulemavu wa viungo walio nao. Kwa mujibu wake, mbali na
kufikiria kuajiriwa serikalini au kwenye mashirika ya umma na binafsi,
watu wenye ulemavu ambao wana vipaji na maarifa ya aina mbalimbali,
wanaona ni vema kuchangia kuzalisha ajira kwa kutumia vipaji na uwezo
wao wa maarifa.
Anasema, kuona kwa watu wenye ulemavu kuwa ni vema kuchangia kukuza
ajira na kipato kunaweza kufikia hatua ya utekelezaji, ikiwa
watawezeshwa zaidi kuwa na kianzio, yaani mitaji itakayowawezesha
kuanzisha shughuli wanazoweza kuzisimamia na kuziendeleza kwa kuajiri
watu wengi zaidi wenye ulemavu na wasio na ulemavu, huku wakijipatia
kipato.
Anasema, “Uwezo tunao na nia ya kushiriki kukuza ajira nchini tunayo.
Chabmsingi ni Serikali kutuwezesha zaidi mitaji ili tuweze kuichanganya
na maarifa na ubunifu wetu kuanzisha kitu kikubwa kitakachowafanya
vijana wengi wajishughulishe na si kubweteka au kukimbilia mijini
kuendekeza kuombaomba”.
“Kwa mlemavu yeyote mwenye maarifa na mtaji suala la kusimama
barabarani kuomba au kubweteka na kusubiri kuletewa ni fedheha. Lakini
kwa anayelilia mtaji na kujihakikishia malengo ya kuendeleza shughuli
atakayoianzisha kwa ajili yake na wengine ndani ya nchi yake ni ujasiri,
hivyo ni vema ukaungwa mkono,”anasema. Funzo analotoa Charles anasema
kuwa hakufikiria kubweteka ingawa hakuwa na mtaji mkubwa.
“Nilijikusanya na kuwekeza kiasi kidogo nilichokuwa nacho na
kuanzisha biashara ya kung’arisha viatu ambayo kwa kiais fulani
inamwezesha kuendeleza maisha yake,” anasema.
Kutokana na maelezo yake, chama chao kinafanya juu chini kuhakikisha
wanapata mafunzo ya ujasiriamali kuepusha wasitawaliwe na mawazo ya
kubweteka kwa kutegemea kupewa misaada ya hapa na pale, bali kuwaandaa
wawe na fikra ya kuanzisha miradi ya maendeleo itakaowawezesha kuinua
vipato vyao kwa kipindi kirefu.
“Mtu akikupa mtaji anakuwa amekutoa kimaisha tofauti na
atakayekusaidia chakula leo na kesho na kuenda zake. Anayekupa mtaji
anakuwa amekufungulia mlango wa kujipatia kipato na anayekupa mlo wa
siku anakuwa amekusaidia, lakini msaada huo unaweza kukudumaza na
kukufanya usifikirie kujiendeleza,” anaeleza.
Vijiweni Charles anawaonya watu wenye ulemavu wanaopoteza muda kukaa
vijiweni wakijadili mambo yasiyo na maendeleo, kuacha kufanya hivyo na
badala yake wafuate nyayo za wengine waliojiunga na vikundi vya
ujasiriamali kutengeneza nguvu itakayowawezesha kujiajiri.
“Walemavu hapa Kahama hatupo wengi sana kiasi cha kushindwa
kuwezeshwa mitaji na kuanzisha miradi. Tuna uwezo wa maarifa ya aina
tofauti hivyo ni vizuri tukawepo pamoja na kufikiria ni nini tufanye ili
Serikali itutazame zaidi kwa upande wa mitaji”, anasema.
Anaongeza kuwa, Mungu hamnyimi mtu kila kitu ndio maana unakuta
mlemavu wa viungo iwe kwa sababu ya kuzaliwa na ulemavu au ajali,
anakuwa na namna mbadala ya kufanya jambo ambalo mtu asiye na ulemavu
analifanya.
Kinachokuwa kigumu ni kianzio tu (mtaji). Kwa walemavu waliosoma,
amewashauri wasikubali kubweteka bali watumie elimu yao hata kutoa
ushauri kwa walemavu wengine ili, pamoja na kuwanufaisha kwa kupanua
mawazo yao kwa njia ambayo ni chanya zaidi, wasidumaze yao. Ombi kwa
Serikali Anaiomba Serikali iendelee kuwatazama kwa jicho la karibu watu
wenye ulemavu kwa kuwarahisishia mazingira ya kupata mitaji kutoka
katika taasisi zake za fedha kwa kuwa wengi wao hawana dhamana inayoweza
kukubaliwa na taasisi hizo.
Anasema, Serikali ya CCM imekuwa ikitukumbuka kwa njia mbalimbali,
hasa kupitia wenzao walioko katika miji mikubwa kama vile Dar es salaam
ambapo waliobahatika kupata vyombo vya usafiri zikiwemo bajaj
wameruhusiwa kuendesha biashara ya usafirishaji katika maeneo ambayo
wengine hawaruhusiwi. Kwa kufanya hivyo, imewatengenezea fursa nzuri ya
kujiingizia kipato bila kushindanishwa na wasio na ulemavu.
“Sasa changamoto imebaki kwetu sisi tulio nje ya miji mikubwa, kwa
sababu mitaji yetu ni midogo sana. Mwenye biashara inayoonekana kuwa
kubwa ni pamoja na anayejishughulisha kama mimi hapa kwa kushona viatu,
lakini ukiangalia hali halisi tunachokizalisha kwa mtaji huo mdogo
hakitoshi na wala hatuzalishi ajira kama tunavyotaka,” anasema.
Anaeleza kuwa kuna mashirika yasiyo ya Serikali yanayojitoa kusaidia
watu kwa kuangalia matabaka yao, jambo linalowafanya wenye ulemavu
kushindwa kufikiwa. Kutokana na hilo, anaiomba Serikali iwaondoe katika
fedheha ya kuachwa nyuma na mashirika ya aina hiyo kwa kuitengenezea
jinsi ya kupata mitaji wajikwamue na kuwezesha wengine wengi zaidi
kushiriki ajira katika miradi ya ujasiriamali watakayoianzisha.
“Kuna fedha za Serikali asilimia tano inayotolewa kwa kundi la vijana
kupitia Halmashauri za Wilaya ili ziwawezeshe katika shughuli za
maendeleo, sisi walemavu vijana wa Kahama hatujui lolote kuhusu fedha
hizo hivyo tunaziomba mamlaka husika zitufikirie angalau katika awamu ya
Tano ya uongozi wa Dk Magufuli zitufikie,” anasema.
Zaidi, anaeleza kuwa ikiwa watapata mgawo katika fungu hilo, watu
wenye ulemavu katika eneo lao wataweza kufanya mambo ya msingi
yatakayonufaisha wengi na si wao pekee. Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la
Watu wenye Ulemavu mkoani Shinyanga (SHIVYAWATA), Michael Nkanjiwa
anasema wanamshuku Rais John Magufuli kwa kutoa kibali cha kufanya
sherehe siku ya Walemavu kitaifa mkoani Mwanza, akiamini kuwa itachangia
wengi kuhamasika kuwakumbuka watu wa kundi hilo.
“Tuna imani na Rais Magufuli kutokana na kauli alizozitoa wakati wa
kampeni zake za urais. nakumbuka aliahidi kutowabagua watu wenye ulemavu
kwa hiyo imani yetu imesimama katika kuona hilo linatokea,” anasema.
Anaeleza kuwa, jambo la muhimu wanalomuomba ni kuwaondolea imani
mbaya wakopeshaji hasa taasisi za fedha kuwa watu wenye ulemavu si
walipaji wa mikopo, kwa kuwapa taarifa sahihi za wanaoirejesha.
“Tunaonekana ni wa kushindwa kurejesha mikopo, lakini ukweli ni kwamba
nasi tunaweza kuilipa ikiwa masharti yatafanywa kuwa rahisi kulingana na
hali zetu. Si kweli kuwa hatuwezi”.
No comments:
Post a Comment