MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imeanza kutoa leseni za muda mfupi kwa kuongeza idadi ya mabasi katika njia ya Dar es Salaam hadi Arusha.
Hatua hiyo ya Sumatra imekuja ili kukabiliana na ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma za usafiri kwenda maeneo mbalimbali nchini, ambapo watu wengi wanataraji kufanya safari kwenda makwao kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka.
Akizungumza jana kuhusu hatua hiyo, Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray, alisema Sumatra imetoa leseni kwa mabasi matano ambayo yalianza kutoa huduma za usafiri kuanzia Desemba moja na leseni hizo zitakoma Januari 30, mwakani.
Mziray aliyataja mabasi ambayo hadi sasa yameshapewa leseni za muda kwa ajili ya kupunguza kero hiyo ya usafiri kwa njia ya Dar es Salaam-Arusha na ambayo tayari yameshaanza kutoa huduma hiyo ni yenye namba za usajili T431BYX, T473CCC, T694 ALX, T924DFR na T922 DFR.
Aidha, alisema mabasi mengine 10 yanataraji kuanza kutoa huduma kuanzia Desemba 7, mwaka huu katika njia tofauti za Dar-Mbeya, Dar –Songea, Dar- Mwanza na Dar -Mtwara, huku bado wakikaribisha wasafirishaji wengine kujitokeza kuomba njia wanazodhani zina uhitaji wa nyongeza ya usafiri.
“Mamlaka inawakumbusha wamiliki wa mabasi wanaotaka kubadili njia kuomba leseni za muda mfupi kwa lengo la kutoa huduma ya usafiri kwa mikoa yenye upungufu wa huduma ya usafiri katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka,” alisema Mziray.
Pia aliwakumbusha abiria kupanga safari zao mapema na walipe viwango vya nauli vilivyoidhinishwa na mamlaka hiyo, huku akitoa tahadhari pia kwa wamiliki wa mabasi kutovunja sheria kwa kuingiza mabasi yao katika njia mpya bila leseni hizo kwani kufanya hivyo ni uvunjaji wa sheria.
“Wapo wamiliki wanaovunja sheria kwa kuingiza mabasi yao katika njia ambazo hawana leseni na bila ukaguzi wa mabasi yao… Kabla ya kupatiwa leseni kuna ukaguzi hufanyika na hiyo ni faida kwa mmiliki wa gari,” alisema Mziray.
No comments:
Post a Comment