MELI mpya ya Mv Mapinduzi (II) imewasili katika Bandari ya Zanzibar
jana kwa ajili ya kuanza safari zake baada ya kukamilika kwa ujenzi wake
nchini Korea Kusini.
Hafla ya kushuhudia kuwasili kwa meli hiyo iliongozwa na Waziri wa
Fedha wa Zanzibar, Omar Yussuf Mzee ambapo alisema ujenzi wa meli hiyo
ni agizo la Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Mzee alisema meli hiyo bado iko katika mikono ya wajenzi hadi sasa na
inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Dk Shein. Alisema meli hiyo ina vifaa
vya kutosha kama vile maboya ya kujiokolea pamoja na boti ndogo ili
kuweka usalama kwa abiria watakaosafiri na meli hiyo.
Waziri wa Fedha alisema meli hiyo itasafiri Pemba pamoja na Dar es
Salaam hivyo kuwataka wananchi kuitunza meli hiyo kwani ni matunda yao.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Dk
Juma Malik alisema lengo ni kulifanya Shirika la Meli lifanye kazi
kibiashara ili kuongeza Pato la Taifa.
Aliwaomba wananchi kuitunza na kuitumia vizuri meli hiyo kwani
wamefanya kazi kubwa na kutumia gharama hadi kufikia kukamilika kwa meli
hiyo.
No comments:
Post a Comment