TANGU mwaka 2004 kumekuwa na harakati za Tanzania kutaka kuwa
na vazi lake la taifa, lakini juhudi hizo zinaonekana kushindikana,
huku sababu za msingi zikishindwa kuwekwa wazi na wahusika. Suala la
vazi la taifa ni muhimu sana kwa lengo la kujenga utaifa na kutambulika
kwa haraka kwa raia wa Tanzania, hasa anapokuwa nje ya nchi na pia
kutangaza utamaduni wa Mtanzania.
Tanzania inapokosa vazi la taifa pia inakosa utambulisho wa taifa na
raia wake, kwani kunakuwa na uvaaji holela usiokuwa na tija kama taifa
au kushindwa kuitambulisha nchi kimataifa kupitia mavazi. Desemba 15
mwaka 2011, serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na
Michezo, wakati huo ikiwa chini ya Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi, ilifanya
uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Kubuni Vazi la Taifa.
Kuteuliwa kwa Kamati hiyo kuliamsha imani miongoni mwa Watanzania
sasa kupata utambulisho wa vazi lake. Kamati hiyo iliyokuwa na watu
wanane, Mwenyekiti alikuwa ni Joseph Kusaga, Katibu Angela Ngowi, ambaye
ni miongoni mwa wanamitindo mahiri nchini, huku wajumbe wa kamati
wakiwa ni Habib Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia
Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda, ambaye alitangaza
kujiondoa Desemba 22, 2011.
Licha ya kamati kuzinduliwa rasmi na Waziri Nchimbi, tayari kuanza
kazi yake ya mchakato wa kubuni vazi la taifa, lakini mpaka sasa
haijulikani nini kimetokea hadi kutopatikana kwa vazi hilo
lililotarajiwa kupatikana ndani ya siku 75 tu. Kazi ya kamati hiyo
haikuwa kuanza mchakato mpya wa Vazi la Taifa, bali ilipaswa kumalizia
mchakato ulioanza mwaka 2004. Aprili mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete
alivunja Baraza la Mawaziri, Waziri Nchimbi akahamishiwa Wizara ya Mambo
ya Ndani na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Fenella Mukangara, ambaye
kimsingi alipaswa kufuatilia suala hilo. Septemba 10, 2012, Kamati ya
Vazi la Taifa chini ya Kusaga ilikabidhi ripoti kwa Waziri Mukangara
kupitia kwa Katibu wa Kamati hiyo, Angela Ngowi, akiwa na wajumbe wa
kamati hiyo, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo.
Wakati wa makabidhiano hayo, Angela alisema katika mchakato wa kupata
vazi hilo, walipokea zaidi ya michoro 200 kutoka kwa wasanii 88 wa hapa
nchini na kupitisha michoro sita iliyokuwa imekidhi vigezo na kuikabidhi
kwa wataalamu wa vitambaa kwa ajili ya kutoa uamuzi wao. Baada ya
kupokea ripoti hiyo Dk. Fenella akaiagiza menejimenti ya wizara yake
chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu, ichague vitambaa vitatu kati ya
vitano vilivyopendekezwa na kamati na kupelekwa ngazi ya sekretarieti ya
Baraza la Mawaziri, kamati ya ufundi ya makatibu wakuu na hatimaye
Baraza la Mawaziri. Leo hii ni miaka mitatu tangu ripoti hiyo itue kwa
waziri husika, lakini hakuna kinachozungumzwa tena kuhusiana na vazi
hilo, hivyo kuwaacha midomo wazi Watanzania wakiwa hawajui hatima ya
vazi hilo. Kitendo cha ukimya huo kimesababisha Watanzania kuendelea na
kasi ya kushabikia mavazi ya tamaduni za nje (hasa za nchi za Ulaya na
Afrika Magharibi), si kwenye mavazi tu, bali hata katika sanaa nyingine
kama vile filamu na muziki kwa kasumba tu kwamba hizo ndizo bora na
hazina mpinzani.
Endapo ahadi ya serikali ingetimia, leo hii Watanzania wangekuwa
‘wakijimwaya’ na vazi hilo ambalo kwa namna yoyote ile ni fahari na
heshima kwa kila Mtanzania. RAI ilifanikiwa kuzungumza na mwanamitindo
wa kimataifa wa Tanzania, Millen Magese kuhusu mtazamo juu ya suala
hilo, ambapo bila kusita alionesha wasiwasi wake na hatua hiyo ya
serikali kulikalia kimya suala hilo ilhali lilikuwa linakaribia mwisho.
Wabunifu wa mavazi wako wengi na tayari wameshapendekeza michoro, hivyo
kitendo cha kulikalia kimya suala hilo siyo tu linarudisha nyuma
jitihada hizo, bali pia linawavunja moyo wahusika waliohangaika nalo
toka hatua za awali. Flaviana Matata naye ni mmoja wa wanamitindo wa
kimataifa anayekerwa na hali hiyo, ambapo kwa mtazamo wake ni aibu kwa
Tanzania mpaka sasa kutokuwa na vazi lake la taifa na badala yake
wananchi wale ndio kuwa wavaaji wakubwa wa mavazi ya wengine, hasa
wanapotoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment