Kwa mara nyengine tena, Zanzibar imo
kwenye mzozo usioweza kuelezeka kwa msamiati wowote zaidi ya uhuni wa
waroho wa madaraka, japokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Masuala ya Afrika
Mashariki na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga anatumia
kijembe cha “utamaduni wa kisiasa wa Zanzibar”. Huu si utamaduni. Huu ni
uhuni uliopewa sura ya kisiasa kwa kuwa unatendwa na wanaoitwa
wanasiasa.
Ni jambo jema kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(SMT) sasa inaonekana kusaka suluhisho la uhuni huu, baada ya Rais John
Magufuli kukutana kwa mara ya kwanza na Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, mwanzoni mwa wiki hii. Mkutano
huu ulichukuwa masaa mawili na ukaishia kwa taarifa fupi kwa waandishi
wa habari, ikiwa ni mara ya kwanza tangu vikao vinavyoendelea ikulu ya
Zanzibar vikiwashirikisha marais wastaafu wa Zanzibar pamoja na Maalim
Seif na Balozi Seif Ali Iddi kuwa na taarifa kwa waandishi wa habari
kutoka Ikulu.
SIASA ZA MUUNGANO KUELEKEA ZANZIBAR:
Licha ya kuupenda kwangu ‘Muungano’, mimi si muumini wa ‘siasa za
Muungano‘ kuelekea Zanzibar. Kwa hakika, nina mziya na dhima ya viongozi
wa SMT, nikiamini kuwa wanatumikia sera maalum dhidi ya Zanzibar
ambayo, hata kama haikuandikwa popote, inasomeka hivi: “Muungano imara
kwa Zanzibar dhaifu, Zanzibar imara kwa Muungano dhaifu.” Na kwa vile
kuwa na Muungano imara ndilo lengo kubwa na la kipekee, basi kila hatua
moja inayochukuliwa kuelekea kwenye lengo hilo huidhoofisha Zanzibar kwa
makusudi.
Mafanikio ya sera hiyo yanawezeshwa kwa kiasi kikubwa sana na
viongozi wa Zanzibar wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani
kwao wao hiyo ndiyo njia pekee ya kubakia madarakani. Nje ya mduara wa
papo kwa papo wa kuitumikia na kutumiliwa na sera hiyo, viongozi wa CCM
Zanzibar hawana pengine pa kushika.
Ile inayoitwa ‘migogoro ya kisiasa’ visiwani Zanzibar, ukiwemo huu
uhuni wa tarehe 28 Oktoba 2015, ina mahusiano makubwa sana na mduara
huu. Kwa hivyo, suluhisho la kudumu na la uhakika limo kwenye jitihada
za kuuvunja mduara wenyewe kwa maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na ya Zanzibar.
Hapa ndipo penye kiini cha makala hii inayoongozwa na kile
kinachoitwa ‘husnu-dhana’ (dhana njema), licha ya kuwa mwenyewe nina
mziya nilioutaja hapo juu na, hivyo, ninaweza kuhojika na pia
kukosoleka.
Je, Magufuli si mwana-CCM? Je, naye si kiongozi wa SMT?
Sasa kipi kinachonifanya niwe na dhana njema kwake? Jawabu ni moja tu – Rais Magufuli ameonesha kuwa ni ‘mwana-CCM asiye ule u-CCM tuliouzoea kupitia utendaji wake. Hivyo, dhana yangu njema itabakia hadi pale naye atakapobadilika. Akibadilika, sitakuwa nimepoteza jambo zaidi ya kurejea kwenye kile nilichokuwa nikikiamini tangu mwanzoni.
Sasa kipi kinachonifanya niwe na dhana njema kwake? Jawabu ni moja tu – Rais Magufuli ameonesha kuwa ni ‘mwana-CCM asiye ule u-CCM tuliouzoea kupitia utendaji wake. Hivyo, dhana yangu njema itabakia hadi pale naye atakapobadilika. Akibadilika, sitakuwa nimepoteza jambo zaidi ya kurejea kwenye kile nilichokuwa nikikiamini tangu mwanzoni.
Niliwahi kuwa na msimamo dhidi ya Benjamin Mkapa na pia Jakaya
Kikwete wakiwa marais wa SMT juu ya kile walichoitendea Zanzibar na kwa
bahati mbaya sana kwangu ni kuwa hawakunisuta kwa kutenda kinyume na
khofu zangu mpaka siku wanaondoka madarakani. Hawakubadilika, nami
sikubadilisha msimamo wangu. Rais Magufuli asipobadilika, nami
sitabadilisha, lakini akibadilika, nami nitabadilisha.
Kuna kitu kinaniambia kuwa Rais Magufuli ni kiongozi anayejaribu
kupapasa kuongoza njia akiwa gizani. Anaweza kuwa anafanya makosa katika
kupapasa huko, lakini ni kiongozi anayejaribua, nami kama raia nina
wajibu wa kumsaidia kuepuka makosa ambayo niliyaona kwa watangulizi
wake, ili ajuwe anapopapasa anaashika nini na nini humo gizani alimo na,
hatimaye, endapo atafanikiwa, basi itakuwa imefanikiwa Tanzania,
itakuwa imefanikiwa Zanzibar.
1. Kuepuka Unafiki wa Mkapa na Kikwete
Kosa la kwanza la Mkapa na Kikwete kuhusiana na Zanzibar lilikuwa ni
unafiki wao wa kujidai wanaulinda Muungano kwa gharama za haki, uhuru na
heshima ya Wazanzibari. Mwaka 2005 wakati Mkapa anaulizwa na waandishi
wa habari wa kimataifa kwa nini alituma wanajeshi na silaha nzito
visiwani huko, alijibu kwa kebehi: “Kwa nini hamuulizi kwa nini Bush
amepeleka vifaru na majeshi Iraq!?” Mwaka mmoja nyuma, aliyekuwa waziri
wake wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Phelomon Sarungi,
alisema kwamba “Muungano na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni watoto
pacha na hivyo jeshi halitavumilia kuona Muungano unahatarishwa.”
Miaka 10 baadaye, Kikwete alifanya yale yale aliyofanya Mkapa.
Nilikuwepo wakati ofisi za kutangazia matokeo za Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC), Bwawani, zikivamiwa na luteka ya kijeshi siku moja kabla
ya uchaguzi kufutwa kihuni na Jecha Salim Jecha tarehe 28 Oktoba. Jeshi
liliendelea kuvikalia vituo na maeneo muhimu miezi takribani miwili
baada ya hapo, hadi Maalim Seif alipokutana na Rais Magufuli tarehe 21
Disemba.
Rais Magufuli atafanikiwa pakubwa kama ataliangalia suala la Zanzibar kwenye uhalisia wake na bila kuzamisha kichwa mchangani.
a. Ayaone mafungamano makubwa baina ya siasa za uchaguzi wa Zanzibar na sera ya Muungano kuelekea visiwa hivi.
b. Alione tatizo lililomo ndani ya chama chake, ambacho bado
hakijataka kuutambua uhalisia kuwa pande hizi mbili za Muungano zinaweza
kutawaliwa na vyama viwili tafauti vya kisiasa.
c. Rais Magufuli auone mtego uliomo kwenye mduara wa papo kwa papo wa
kutumiliana baina ya CCM Dodoma na CCM Kisiwandui kwa maslahi ya
kikundi cha watu na sio chama kizima wala nchi nzima.
Kikundi cha Dodoma kinajenga picha kuwa bila wenzao wa Zanzibar
kukidhi matakwa yao, basi hawawezi kusalia madarakani, na kikundi cha
Zanzibar kinatumia fursa hiyo kujenga vitisho kwa wenzao wa Tanganyika
kwamba bila ya wao kuwapo madarakani, basi hakutakuwa tena na Muungano.
Kosa hili ni la muda mrefu. Lilikuwa likitendwa hata na Mwalimu Julius Nyerere wakati akivumilia uimla wa serikali ya awamu ya kwanza visiwani Zanzibar.
Kosa hili ni la muda mrefu. Lilikuwa likitendwa hata na Mwalimu Julius Nyerere wakati akivumilia uimla wa serikali ya awamu ya kwanza visiwani Zanzibar.
Rais Magufuli anaweza kujifunza kwa kutokuingia kwenye mtego huu, na
kama akiliendea vyema atagundua kuwa kiini cha yote kimo kwenye muundo
wa Muungano na hapo, hapana shaka, ndipo atakapofahamu kuwa hataweza
kulimaliza la Zanzibar salama usalimini na milele, kama hapakupatikana
katiba mpya inayoakisi uhalisia huu.
2. Kukosa Uthubutu wa Kisiasa
Kosa la pili la watangulizi wake ni kukosa uthubutu na kukumbizia
majukumu kwengine, ambalo yumkini linatokana na hilo la kwanza la kuwa
wanafiki. Wote wawili, kwa nyakati tafauti, walitaka kuonesha kuwa
matatizo ya Zanzibar yanasababishwa na kundi la wahafidhina wenye nguvu
za ajabu ndani ya chama chao kwa upande wa Zanzibar.
Rais Jakaya Kikwete
Wakati akizungumza na mwandishi wa jarida la Prospect, Jonathan
Power, mwishoni mwa utawala wake, Mkapa alielezea masikitiko yake jinsi
wenzake Zanzibar walivyomzuwia kuleta mabadiliko ya kidemokrasia na
heshima kwa haki za binaadamu. Naye Rais Kikwete hata alipokuwa bado
waziri wa mambo ya nje wakati wa Mkapa, alinukuliwa akisema amechoka na
kuuliziwauliziwa mgogoro wa Zanzibar kila anapokwenda duniani na sasa
ulikuwa umefika muda wa kuumaliza kabisa kabisa, lakini ulipofika
mkutano wa Butiama wa uliokuwa uwe Muafaka II, akasalimu amri mbele ya
wahafidhina hao hao.
Kwa sababu ya kukosa kwao uthubutu wa kulikabili tatizo halisi,
wakawageukia wapinzani kwa lugha za kibaguzi na dharau kama wao ndio
wenye jukumu la matatizo yaliyopo Zanzibar.
Katika hotuba yake ya kwanza bungeni Disemba 2005, Kikwete alisema
anasikitishwa na “mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar”, lakini kama
alivyofanya mtangulizi wake Mkapa mwaka mmoja kabla ya hapo, naye
akatupa lawama za mpasuko huo kwa kundi fulani tu la watu – Wapemba.
Msimamo kama huu pia ulikuwa umeanza kufuatwa na utawala wa Rais
Magufuli na, kwa hakika, ndio maana ya kauli ya Balozi Mahiga ya
“utamaduni wa kisiasa wa Zanzibar.”
Matokeo ya kukosa uthubutu kwa Mkapa na Kikwete sio tu kwamba
yameendelea kuwa muendelezo wa uhuni wa kila baada ya miaka mitano
visiwani Zanzibar, bali pia wote wawili wameondoka na kuiwachia hali
kuwa mbaya zaidi kuliko walivyoikuta. Wote waliyawachia makundi ya
kihalifu yaundwe na yatekeleze hujuma dhidi ya maisha na mali za
wananchi wa Zanzibar – majanjawidi yaliundwa wakati wa utawala wa Mkapa
na Kikwete ameondoka akiyaacha mazombi na masoksi – huku wao
wakiyaangalia hayo kuwa ni “matatizo ya Wazanzibari wenyewe.”
Lakini Rais Magufuli amejipatia mwenyewe jina la “mpasua majipu”,
ambalo linamaanisha kuwa “mtu mwenye kuthubutu.” Ikiwa kweli upasuaji
wake majipu utaakisika kwenye suala la Zanzibar, hapana shaka
atafanikiwa. Na wala hapaswi kuchimba mbali sana. Kwa mfano, akiwa rais
na amiri jeshi mkuu wa nchi, ana nyenzo na taasisi za kumpa taarifa zote
za ukweli wa nini kilifanyika Zanzibar ndani ya miaka 10 iliyopita na
nini kinaendelea sasa. Ndani ya ripoti hizo, muna mikasi ya kutosha ya
kulipasua jipu la Zanzibar, sindano za kushonea, dawa za kulipaka na
bendeji za kulifungia. Baada ya miaka mitano tu, kitakachobakia kitakuwa
ni kovu na sio tena kidonda.
3. Kiburi dhidi ya upinzani
Kosa la tatu ambalo Rais Magufuli anapaswa kuliepuka ni kiburi cha
kupuuzia nguvu za upinzani visiwani Zanzibar, akidhani kwamba unafiki na
kukosa uthubutu kunatosha kuwatenga kando. Ukweli kwamba CCM imekaa
madarakani muda mrefu na inadhibiti mihimili yote ya dola uliwalevya
sana Mkapa na Kikwete, ambao daima walidhani upinzani visiwani Zanzibar
hauna njia yoyote ya kukabiliana na dola zaidi ya kulilia mazungumzo,
vikao na miafaka, ambayo wao ndio wanaoiamulia ajenda na hatima yake.
Ni kweli kuwa uongozi wa CUF unaamini sana kwenye siasa za
diplomasia, labda kwa kuzingatia pia mazingira hayo mbayo unakabiliana
nayo. Kuelekea uchaguzi wa 2005, Maalim Seif alimuandikia mara kadhaa
Mkapa wakutane, na hakuna siku Mkapa alijibu barua hizo. Kuelekea 2015,
mara kadhaa Maalim Seif alimuandikia Kikwete waonane, lakini ilimchukuwa
miezi kukubali na hata walipokutana mjini Dodoma mwezi mmoja kabla ya
uchaguzi, mazungumzo yao hayakuchukuliwa hatua yoyote. Mmoja wa watu
waliokutana na Kikwete baada ya hapo, aliniambia Kikwete aliwaambia
anashangazwa na Maalim Seif kila siku anamuendea na matatizo tu na
hakuna siku amemuendea angalau na “pendekezo la kupanda miembe kisiwani
Pemba.”
Inafahamika kuwa hata mkutano wa tarehe 21 Disemba 2015 kati ya
Maalim Seif na Rais Magufuli ulikuja baada ya barua saba tafauti kutoka
kwa Maalim Seif kuomba mazungumzo hayo. Mkapa na Kikwete waliichukulia
siasa ya diplomasia ya Maalim Seif kuwa ni udhaifu. Wakautumilia udhaifu
huo. Wakadhani kwamba wanamuhujumu Maalim Seif na CUF yake. Matokeo
yake ni kuwa sio tu CUF ilikibwaga chama chao kwenye uchaguzi wa 2015
visiwani Zanzibar, bali pia athari za nguvu yao zilivuuka maji na kuupa
mbolea upinzani upande wa Tanganyika na kwa mara ya kwanza ukakaribia
asilimia 40 ya kura za urais.
Siasa Za Diplomasia Zafanya Kazi
Hii inamaanisha kuwa siasa za diplomasia za upinzani visiwani
Zanzibar zina nguvu kubwa na wala si alama ya udhaifu. Kuna faida ya
kipekee kwa Magufuli kufanya kazi na watu ambao wanaamini kwenye
diplomasia kuliko kuwaachia waje wageuke kuwa waumini na siasa za
mapambano. Baada ya yote, wote ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, naye ndiye mwenye dhamana ya kuwalinda na kuwatumikia.
Kwa hivyo, kama ni kiongozi wa kujifunza, makosa ni mwalimu mzuri na
Rais Magufuli mahala pa kuanzia anapo. Vyenginevyo, miaka mitano au kumi
ijayo, tunaweza kurudi tena hapa kuandika yale yale tuliyoyaandika
kuhusu Mkapa na Kikwete. Huenda wenyewe wanadhani kuwa yetu ni maneno
ya chura mtoni tu yasiyomzuwia ndovu kunywa maji, lakini mambo yana zama
na zamu na dunia inabadilika.
Imeandaliwa na Mohammad K.Ghassani
No comments:
Post a Comment