MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amepinga hatua za
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) kuongeza bei ya
maji kwa madai ongezeko hilo litasababisha wananchi wengi kukosa huduma.
Mulongo alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza
na wafanyakazi wa Mwauwasa, namna wanavyotoa huduma kwa wananchi,
changamoto zinazowakabili pamoja na mafanikio ya mamlaka hiyo.
Hivi karibuni Mwauwasa, ilitangaza kuomba kuongeza bei ya maji kwa
kile ilichodai kupanda kwa gharama za mita za maji hivyo wanapendekeza
kuongeza bei ya maji kitendo ambacho wananchi wengi jijini hapa
walikipinga.
Mulongo akizungumza na wafanyakazi hao amesema kuwa katika
ufuatiliaji alioufanya amebaini kwamba kuna mchezo uliandaliwa na
mamlaka hiyo kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe na sio wananchi hivyo
haungi mkono hatua hizo.
“Mimi ninafahamu kwamba hawa watu ambao mliwaleta na wakakubaliana na
nyie kuongeza bei ya maji ni wa kwenu ambao mliwaaandaa ili
kuwaaminisha wananchi, sasa suala hilo siliungi mkono.
“Utaratibu wa kuongeza bei ya maji ambao nyie mnadai kupanda kwa
gharama za mita za maji kaeni muangalie upya namna ambayo mtafanya,”
amesema Mulongo.
Hata hivyo Mulongo aliwataka wafanyakazi hao kuwajibika kwani ni
wajibu wao kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi
hususani wanaoishi katika maeneo ya miinuko.
No comments:
Post a Comment