TTCL

EQUITY

Tuesday, December 22, 2015

Tumbua ya Magufuli hawa wamekwenda

Kazi imeshika kasi! Mpango wa Rais Dk. John Magufuli kutumbua majipu, umesababisha kung’olewa kwa vigogo 34 ambao ni watumishi wa umma huku Usalama wa Taifa wakitajwa kuzizingira nyumba za vigogo hao, Uwazi linakupa zaidi.
Magufuli3 (1)
Rais Dk. John Magufuli.

Kwenye Mtaa wa Kondo, Bahari Beach, Kata ya Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni, Dar, taarifa zinasema siku chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza zoezi la kutumbua majipu, maofisa hao walifika katika nyumba hizo na kuzifanyia upekuzi uliodumu kwa zaidi ya saa moja.
Wananchi wa eneo hilo waliliambia Uwazi kuwa nyumba zilizopekuliwa ni pamoja na anayoishi aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha Bandari Kavu TRA, Rajab Mdoe na ya Habibu Mponezya ambaye alikuwa Meneja wa Kitengo cha Ushuru.
“Tumepata taarifa kuwa pia akaunti zao za benki zimezuiwa wakati uchunguzi ukiendelea. Kwa kweli tunaushukuru uongozi wa Rais Magufuli, ameanza vizuri,” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka kutaja jina.

wpid-Crescentius-Magori
MWENYEKITI SERIKALI YA MTAA
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kondo, Hamis Haule alipohojiwa na Uwazi kuhusiana na madai hayo, alikiri kufika kwa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na kufanya upekuzi katika nyumba za vigogo hao ambao kwa sasa wamesimamishwa kazi huku wakiendelea kuchunguzwa.
“Ni kweli walikuja watu ofisini kwangu, wakajitambulisha ni Usalama wa Taifa lakini hawakunikuta, wakafuatana na Mtendaji wa Mtaa wa Kondo, George Rupia hadi katika nyumba hizo na kufanya upekuzi ikiwa ni pamoja na kuchunguza hati zao za kusafiria kisha kuzishikilia,” alisema mwenyekiti huyo.

WATUHUMIWA NAO WAAHIDI
Wakati hali ikiwa hivyo, baadhi ya ndugu wa vigogo hao waliozungumza na Uwazi juzi, walisema watuhumiwa hao nao wamekaa mkao wa kuwataja kwa majina ‘wakubwa’ wao kwa vile ndiyo walikuwa wakikwamisha utendaji wao kwa kutoa ‘vimemo’ vya kuruhusu ukwepaji wa kodi.

Mwinjaka
Mwinjaka.
“Unajua hii ishu ina mapana yake. Ni kweli Rais Magufuli anatumbua majipu. Lakini na hawa watu nao wana majipu makubwa ya kuyatumbua kuliko hayo ya Magufuli,” alisema ndugu mmoja wa watuhumiwa hao.

WALIOKWENDA
Katika harakakati zake za kutumbua majipu, Rais Magufuli ameshavunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) iliyokuwa na mwenyekiti, Profesa Joseph Msambichaka, wajumbe ni mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu, Mhandisi Mussa Ally Nyamsingwa, Mhandisi Donata Mugassa, Mhandisi Gema Modu, Dk. Francis Michael, Crescentius Magori na Flavian Kinunda.
Hatua ya kuvunjwa kwa Bodi ya TPA ilitokana na kushindwa kuisimamia vyema bandari na kusababisha makontena 2,716 kutolewa kwenye geti namba 5 bila kulipia kodi hivyo kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

DSC_0092
Mussa.

KUNG’OLEWA KATIBU MKUU
Hasara hiyo kwa taifa, pia ilimfanya Rais Magufuli afute nafasi ya Mkurugenzi wa TPA, Awadhi Massawe na kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kutokana na ubadhirifu wa Sh. bilioni 16 ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty alisimamishwa kazi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Jumanne Sagini kwa tuhuma za kusimamia vibaya ujenzi wa barabara za manispaa hiyo na kujengwa chini ya kiwango pia rais alimng’oa Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Rashid Bade.

45
Bade.
KAMATAKAMATA
Makontena yaliyopotea bandarini yalimfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasimamisha kazi na kukamatwa kwa maofisa 12 wa mamlaka hiyo.
Waliokumbwa na kamatakamata hiyo ni Shaban Mngazija (meneja mapato), Rajab Mdoe (mkurugenzi wa fedha na mkuu wa bandari kavu) na Ibin Masoud.
Maofisa wa TPA waliokuwa wakifanya kazi bandari kavu na kuruhusu makontena hayo kwenda kwa wateja bila kulipiwa kodi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataja kuwa ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante na James Kimwona.
Novemba 27, mwaka huu, waziri mkuu alibaini upotevu wa makontena 329 na ile ziara yake ya Desemba 4, mwaka huu, ilibaini upotevu wa makontena 2,387.
Aidha, watu wanane kati ya 12 waliokuwa wakishikiliwa na kuhojiwa na polisi kutokana na upotevu wa makontena 329 na ukwepaji ushuru zaidi ya shilingi bilioni 80, walipandishwa kizimbani Mahakama ya Kisutu, Dar.

AWADH MASSAWE
 Masawe.

Watuhumiwa hao ni aliyekuwa Kamishna wa Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki, wanaokabiliwa na mashitaka mawili ikiwemo kuhujumu uchumi na upotevu wa kiasi cha shilingi bilion 12.7.
Waliopandishwa kizimbani pamoja na Tiagi Masamaki ni Habib Hamis (meneja huduma na wateja TRA), Haroun Mapande (mkuu wa mfumo wa ICT -TRA), Raymond Adolf (afisa), Eliachi Mrema (afisa bandari kavu ya Azam), Ashraf Yusuf Khan (meneja wa ICD ya Azam) na Bolton Adolf (meneja udhibiti wa TRA).
MUHIMBILI NAO
Magufuli pia alivunja Bodi ya Wakurugenzi Hospitali ya Taifa Muhimbili na kutengua nafasi ya Kaimu Mkurugenzi, Dk. Hussein Kidanto.

Hosea 
 Hosea.

TAKUKURU KUKANUKA
Magufuli pia alikinukisha kwa kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea kwa sababu ya kutoridhishwa na utendaji wa taasisi hiyo. Pia Rais Magufuli akaagiza kusimamishwa kazi watumishi wanne wa taasisi hiyo ambao walisafiri nje ya nchi licha ya yeye kupiga marufuku.
Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nakitasi ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali kutoka kwa rais au Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue.Imeandaliwa na Elvan Stambuli, Makongoro Oging’ na Issa Mnally.

No comments:

Post a Comment