KASI ya utendaji kazi
katika Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli, imehamia Shirika la Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA), baada ya Serikali kuagiza Menejimenti ya
shirika hilo kuanza kujitegemea ifikapo Juni, mwakani kuhakikisha
inalipa watumishi wake mishahara.
Serikali imesisitiza kwamba haitaendelea kubeba mzigo wa kulipa wafanyakazi wa Tazara mishahara ifikapo mwezi huo.
Agizo hilo lilitolewa
na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Dkt.Shaaban Mwinjaka, wakati wa hafla
ya kukabidhi mabehewa 18 na vichwa vinne kwa ajili ya reli ya Tanzania
kutoka nchini China, vyenye thamani ya dola za Marekani mil 22.4.
Lengo la msaada huo ni kuendeleza mahusiano mazuri ya nchi tatu za Tanzania, Zambia na China.
Alisema kuwa,serikali
haitaendelea kuibeba Mamlaka hiyo kwa kuwalipa watumishi wake mishahara
na badala yake itumie fursa zilizopo kusimama yenyewe.
"Upatikanaji wa
mabehewa haya kutoka serikali ya China ni moja ya fursa itakayowezesha
TAZARA kusimama, Viongozi wa Menejiment tumieni fursa zilizopo
kuhakikisha mnasimama imara, kwani Serikali mpaka kufikia Juni 2016
haitabeba jukumu la kuwalipa watumishi wenu mishahara,"alisema Dkt.
Mwinjaka.
"Inasikitisha sana kuona TAZARA ikiwa hoi hadi na kufikia kubeba tani 87,000 kwa mwaka wakati lengo likiwa ni kubeba tani milioni tano,",alisema na kuitaka Menejimenti ya Tazara kukimbia mchakamchaka ili kuondokana na hali hiyo.
Aidha aliitaka Tazara kufanya mabadiliko ya uongozi ili kuweza kuboresha utendaji kazi huku akisisitiza kuwa Tanzania na Zambia bado ziko tayari kuendelea na mashirikiano katika sekta hiyo ya uchukuzi ili kuweza kufikia malengo.
Hata hivyo Balozi wa Zambia nchini, Judith Kapijimpanga, alisema ushirikiano wa nchi hizo ulianza tangu zamani na kwamba lengo kubwa likiwa ni kuimarisha sekta ya uchukuzi.
Alisema mbali na
kuimarisha sekta hiyo pia imewezesha kurahisisha usafiri wa reli hasa
kwa watu wa hali ya chini, kwani treni hizo zimekuwa zikifanya safari
kutoka Tanzania hadi Zambia.
Naye mwakilishi kutoka
Serikali ya China, Zhao Zhongning, alisema kuwa,serikali ya china
itaendelea na mashirikiano na Tanzania kwa kuzingatia taratibu
zinazokubalika.
Alisema kuwa kwa miaka
mingi nchi hiyo imekuwa ikishirikiana katika shughuli mbalimbali za
kimaendeleo hususan uchukuzi na kwamba ndiyo nchi iliyojenga reli hiyo
tangu enzi za rais wa awamu ya kwanza.
Wafanyakazi Tazara
walilalamikia menejimenti kwa kushindwa kusimamia ufanisi wa kazi huku
wakimuomba rais Dkt. Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza ili kujionea
madudu yanafanyika ikiwemo kuwachukulia hatua zaidi viongozi wao.
No comments:
Post a Comment