Wananchi wakiwa na madumu tayari kwa kuchota maji kutoka kwenye chemchemi ya maji ya moto. Maji hayo hutumika kwa shughuli mbalimbali. |
MKOA wa Katavi ni miongoni mwa maeneo ya Tanzania yaliyojaaliwa kuwa
na utajiri mwingi wa maliasili ikiwemo wanyama pori, madini ya aina
mbalimbali, ardhi yenye rutuba na misitu. Lakini mkoa huu pia una kitu
kingine, chemchemi ya maji moto. chemchemi hii ya maji ya moto ni
miongoni mwa vivutio vya utalii wa ndani na nje kwani ni maeneo machache
duniani ambayo aghalabu huwa na kitu hiki kisicho cha kawaida.
Mkoani Katavi, kijiji inapopatikana chemchemi hii kimepewa jina la
Majimoto na kipo katika Tarafa ya Mpimbwe wilayani Mlele. chemchemi hiyo
inayobubujisha maji wakati wote ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa
kijiji hicho cha Maji Moto na vitongoji vyake. Kwa mujibu wa simulizi za
wanakijiji wa eneo hilo, chemchemi hiyo ilivumbuliwa na mbwa wa
wawindaji, takribani karne moja iliyopita.
Kila siku mamia ya watu wakiwemo watoto, wanawake, wanaume na vijana
hufika katika chemchemi hiyo wakiwa na vyombo vya kuteka maji kwa
matumizi ya nyumbani. Pia wageni wanafika mahala hapo kwa lengo la
kushuhudia ukweli tu wa uwepo wa chanzo hicho cha maji. Mzee maarufu wa
jadi wa eneo hilo, Gerald Changwa Sibula (63) anasimulia kwamba chanzo
hicho cha maji kiligunduliwa na mbwa wa wawindaji waliotoka anayoita
‘nchi ya Ufipa ya Juu’ ambayo sasa ni mkoa wa Rukwa.
Sibula ambaye ambaye anajitabulisha kwamba ana nasaba na Chifu
aliyewahi kutawala eneo hilo anasema chemchemi hiyo iligunduliwa miaka
1000 pale mbwa wa wawindaji wawili alipowaongoza hadi eneo hilo na
anamtaja mmoja wa wawindaji hao kuwa ni Lukesa aliyekuwa kafuatana na
nduguye.
Anasema kwa kuwa nchi ya Ufipa haikujaliwa utajiri wa wanyama pori
wawindaji maarufu wa eneo hilo akiwemo Lukesa na nduguye walilazimika
kusafiri mwendo mrefu wakipita katika milima, mito na mapori hadi Maji
ya Moto ambako enzi hizo ilijaaliwa kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori
wa kila aina. “Lukesa na nduguye kama simulizi zinavyosema walifika eneo
hili ili kuwinda wanyama pori lakini walihaha kwa siku tatu wakisaka
maji ya kunywa na kupikia chakula bila kufanikiwa,” anasema Sibula.
“Ukosefu wa maji uliwalazimu ndugu hao wawili kushinda na njaa na kiu
kwa siku tatu. Siku ya nne mchana wakiwa wamekata tamaa, ghafla
wakawaona mbwa wao waliokuwa nao kwenye uwindaji wakirejea wakiwa
wametapakaa matope mwili mzima huku wakipiga piga mikia yao kwa furaha.
“Ndipo wawindaji hao wawili walipobaini kuwa mbwa wao wamegundua kilipo
chanzo cha maji na ndipo wawindaji hao wakaanza kuwafatilia kwa karibu
hadi mbwa hao wakawafikisha kwenye chanzo hicho cha maji ambapo walioga,
wakanywa maji hayo na kuchota mengine kwa ajili ya kupikia chakula
kambini kwao,” anasema.
Sibula anazidi kusimulia kwamba wawindaji hao wakiongozana na mbwa
wao walirejea kambini wakiwa na maji ya kupikia chakula na kunywa na
kwamba baada ya kusonga ugali kabla hawajaanza kula walijiuliza wawatuze
zawadi gani mbwa wao. Inaelezwa kuwa kuanzia siku hiyo wawindaji hao
waliwathamini mbwa wao kwa namna ya kipekee wakiwaona kuwa ni wakombozi
wao wakati wa shida ambapo bila wao bila shaka wangekufa kwa kiu.
Anasema kila walipokuwa wakiandaa chakula, kwa kuthamini mchango wa
mbwa wao walianza kuwapa wao chakula kwa kusema “Kwanza Ipimbwe Iliyee”
yaani kwanza ale mbwa. Anasema msemo huo uliendelea kutumika na
kurithiwa na kizazi kimoja hadi kingine na kusambaa sehemu mbalimbali
hatimaye watu wa eneo hilo wakajulikana kama Wapimbe. Watu hao
walijijengea utamaduni wa kumuenzi mbwa na kusababishwa eneo hilo
kujulikana kama Mpimbwe hadi leo.
Kwa sasa kijiji hicho cha Majimoto ni miongoni mwa vijiji vilivyopo
katika kata ya Mpimbwe. Maajabu mengine ya chemchemi hiyo ni kwamba kina
chake cha maji hakiongezeki wala kupungua na pia joto la maji hayo
halipungui wala kuongezeka. Ingawa kwa kawaida sehemu nyingine maji
hupungua wakati wa kiangazi na kuongezeka wakati wa masika, katika
chemichem hiyo hali ni tofauti.
Kina cha maji hakiongezeki wala kupungua hata kama watu watachota
maji kwa wingi kiasi gani huku joto nalo likiwa haliathiriki kwa lolote.
Wakazi wa kijiji cha Majimoto wanaeleza kuwa maji kutoka katika
chemchemi hiyo ni ya moto na huchukua saa sita kupoa jambo
linalosababisha wageni kupata shida wakati wa kuyanywa sababu ni ya moto
na yana ladha ya chumvi.
“Kwa sisi wenyeji tunayatumia maji haya kwa matumizi mbalimbali
yakiwemo kupikia, kunywa, kuoga na kufulia,” anasema Kiomboi Rasta,
mkazi wa kijiji cha Majimoto. Anasema wakazi wa eneo hilo wamekunywa
maji hayo tangu walipokuwa watoto lakini hadi sasa hawajasikia mtu
yeyote kadhurika kutokana na kutumia maji hayo. Mariam Klaudio anasema
yeye na familia yake wanaamini maji hayo kuwa na salama hivyo huyanywa
bila kuchemsha.
“Ni maji meupe… Hayana kiluwiluwi cha mdudu yeyote yule na hivyo
hatuna sababu ya kuyachemsha kwa sababu yameshachemshwa tayari na
Mwenyezi Mungu… Sisi tumebahatika kupata maji ambayo tumechemshiwa
tayari,” anasema Klaudio. Robert Salum Mashishanga ambaye ni mwanzilishi
wa kijiji hicho anasema alifika eneo hilo mwaka 1991 likiwa pori tu
alikitokea mkoa wa Shinyanga. Mwaka 1994 aliweka mashine ya kusaga
ambayo ilikuwa ikitumia maji kutoka chanzo hicho cha maji.
Anasema chemchemi hiyo pia imekuwa chanzo cha kutunza utamaduni na
mila za wakazi wa eneo hilo kwa kuwa hadi sasa wanazingatia miiko
iliyowekwa na mababu zao. Sibula anaeleza kuwa miiko iliyokuwepo wakati
huo ni kwamba hadi sasa mgeni akifika kijijini hapo kwa mara ya kwanza
anakaribishwa kwa kugusisha kichwa chake juu ya jiwe lililopo karibu na
chanzo hicho cha maji ndipo ataruhusiwa kunywa au kunawa maji hayo.
“Hata wewe mwandishi ni lazima ugonge kichwa chako kwenye jiwe hili
ili upate kibali cha kuyatumia maji hayo na kupata maelezo ya kina
kuhusu chemchemi hii… Huu ni utaratibu wa kawaida ili kudumisha mila na
desturi za kuilinda chemichem hii,” anasema Sibula. Sibula anasema kuwa
miaka ya nyuma eneo la chemchemi hiyo lilitumika kama kitovu cha
mawasiliano. Anafafanua kwamba karibu na chemchemi hiyo kulikuwa na
ngoma iliyokuwa na uwezo wa kujipiga yenyewe na kutoa mlio ulioashiria
jambo fulani.
“Haijulikani ni nani aliyeiweka ngoma hiyo ila ilipojipiga watu wote
walilazimika kuacha shughuli zao na kutimua mbio hadi kwenye makazi ya
chifu ili kusikiliza taarifa mpya kutoka kwa chifu,” anasimulia Sibula.
Anasema ngoma hiyo ilitolewa baada ya Serikali ya Tanzania kuvunja
utawala wa machifu na kuweka mfumo mpya wa utawala. Chemchemi hiyo ina
simulizi nyingi za kale zinazoelezea utamaduni wa Kiafrika na nguvu za
miungu ya asili ambayo ilitumika kabla ya kuingia kwa dini ya Kiislamu
na Kikristo.
Kwa mujibu wa wazee wa kimila wa eneo hilo, wakati Wamisionari wa
Kanisa Katoliki walipofika eneo hilo walitaka kujenga kanisa kwa kuwa
ilikuwa rahisi kupata maji. Hata hivyo, walipoanza kuweka miundombinu ya
kutoa maji kwenye chemchemi hiyo hadi kwenye kiwanja walichokuwa
wakifyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa kanisa maajabu yaliwatokea.
Anasema masimulizi yanaonesha kwamba chemchemi hiyo maarufu kama
Nawinga kwa wakazi wa eneo hili ilihama kwa maana ya kukauka ghafla na
kubakia mchanga tu kisha ikajitokeza kwenye eneo lililojulikana kama
Korodea. “Kukauka kwa chanzo hicho cha maji kuliwalazimisha Wamisionari
hao kuamua kuondoka na kujenga kanisa lao katika kijiji cha Mamba,
umbali wa kilomita tano kutoka kijiji cha Majimoto.
Anasema, ili kulinda chanzo hicho cha maji, serikali imejenga uzio wa
maji ili wananchi waweze kuyachota bila kutumbukiza vyombo au taka
kwenye uzio huo. Pia serikali imepiga marufuku ujenzi wa miundombinu
kwenye chemichem hiyo kwa lengo la kusambaza maji kijijini kwa sababu
usambazaji wa maji kwa kutumia mabomba unaweza kusababisha chemchemi
hiyo kukauka.
Chimichem hiyo inalindwa na wakazi wa eneo hilo kwa kutumia miiko na
desturi za kale zinazokataza watu kuchafua maji hayo wala kuruhusu
wageni kufika eneo hilo bila ruhusa ya wenyeji. Baada ya kizuizi hicho
maji hayo yanaendelea kutiririka hadi eneo la makaburi yanapozikwa
watemi na wakati wote maji hayo yanatakiwa kutiririsha maji yake juu ya
makaburi hayo vinginevyo wanaamini maji yasipofurika juu ya makaburi
hayo kutasababisha ukame na njaa.
Mwandishi wa makala haya alishuhudia mti wa mbuyu ukiwa umeota juu ya
chanzo hicho cha maji ambapo simulizi zinaeleza kuwa umekuwepo hapo
karne kadhaa lakini haukui kama miti mingine ya mibuyu.
No comments:
Post a Comment