Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, alipokuwa akizungumza na wananchi
walioathirika na vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, huko
Gomani, katika kisiwa cha Tumbatu, Zanzibar, mwishoni mwa wiki.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (Zec) ni chombo huru na ndicho pekee kinatakiwa
kuratibu na kusimamia uchaguzi bila ya kuingiliwa na taasisi yoyote ya
ndani wala nje ya nchi.
Alisema Zec imetangaza rasmi kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu
wa Oktoba 25, mwaka huu na tamko hilo kuchapishwa katika Gazeti la
Serikali la Novemba 6, mwaka huu kwa mujibu wa sheria.
“Tume ya Uchaguzi itaratibu na kusimamia uchaguzi wa marudio bila
ya kuingiliwa na taasisi yoyote iwe ya kitaifa au kimataifa kwa sababu
ni kinyume cha Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema.
Kheir aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu kujiandaa na
uchaguzi wa marudio ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua
Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani kwa misingi ya demokrasia.
Aliwataka wananchi kudumisha amani na umoja wa kitaifa wakati huu wa kuelekea kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani humo.
“Zanzibar haiwezi kupiga hatua kubwa ya maendeleo bila ya kuwapo
kwa mazingira ya amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake. Nawapa
pole waathirika wa vurugu za uchaguzi waliochomewa nyumba zao moto kwa
sababu za kisiasa. Haya ni mambo ya kulaaniwa na yasiyopaswa kufanywa na
waliostaarabika,” alisema
Waziri huyo aliwakabidhi waathirika hao misaada mbalimbali ikiwamo,
magodoro, vitanda, nguo, vyombo vya nyumbani, pamoja na fedha za
kusadia gharama za ujenzi wa nyumba kwa familia saba zilizobomolewa
katika vurugu zilizotokea katika mji mdogo wa Gomani, Kisiwani Tumbatu.
Aidha, alisema wananchi wanaosubiri mgombea urais wa Cuf, Maalim
Seif Sharif Hamad, aapishwe kuwa Rais wa Zanzibar kwa matokeo ya
uchaguzi uliyofutwa wanapoteza muda na kujidaganya wenyewe.
“Watu wanaofanya kisomo na kuchoma ubani wakitia nia kuomba Mungu
Maalim Seif awe Rais wa Zanzibar katika mitaa mbalimbali wanapoteza muda
wao na kujidaganya kutokana na matokeo ya uchaguzi huo kuwa si halali
na yamefutwa,” alisema.
Kheri alisema Mwenyekiti wa Zec alifuta matokeo hayo kwa kutumia
kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar pamoja na Sheria ya
Uchaguzi Zanzibar kifungu cha 3(1) na 5(a) vya Sheria namba 11 ya
Uchaguzi ya Mwaka 1984 baada ya kubaini kufanyika udaganyifu mkubwa
katika uchaguzi huo na kinachosubiriwa kwa sasa ni tume hiyo kutangaza
tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio.
No comments:
Post a Comment