Wakati Kikwete akisafiri kwenda mataifa mbalimbali tangu astaafu ikiwamo Uingereza, Magufuli hajakwea pipa hata mara moja kwenda ughaibuni tangu aapishwe.
Wakati Rais John Magufuli, akitumia siku zote 38 za kuwa kwake madarakani hadi kufikia jana kwa kusimamia kampeni yake ya kuongeza mapato ya serikali na kukomesha vitendo vya ufisadi kupitia kile anachokiita ‘kupasua majipu’, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, anaendelea kupasua anga baada ya kuzifikia nchi nne tangu kuachia madaraka.
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akizungumza na
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, walipokutana kwenye Mkutano wa Tano
wa China na Nchi za Afrika jijini Johannesburg, Afrika Kusini wiki
iliyopita.
Hata hivyo, wakati Kikwete akiendelea kusafiri kutokana na majukumu
mbalimbali yanayomkabili akiwa Rais mstaafu, Rais Magufuli ameendeleza
rekodi yake ya kutosafiri kwenda nje ya nchi tangu aingie Ikulu.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa tayari alishakwea ‘pipa’ na
kuzifikia nchi za Ethiopia, Uingereza, Visiwa vya Comoro na pia Afrika
Kusini, huku baadhi ya safari hizo zikitokana na mialiko maalum
anayopewa.
Mara baada ya kuingia madarakani Novemba 5, mwaka huu kufuatia
ushindi wake wa asilimia 58.46 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba
25, Rais Magufuli alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi yasiyo ya
lazima kwa serikali na pia kuwabana wakwepa kodi ili hatimaye kuinua
mapato na mwishowe kunufaisha Watanzania kwa kuwaondolea kero mbalimbali
zitokanazo na huduma za jamii.
Hadi sasa, tayari Rais Magufuli ameshachukua maamuzi kadhaa makubwa
yaliyookoa mabilioni ya fedha na pia kuongeza nidhamu ya kazi katika
ofisi za umma.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli ni pamoja na
tangazo lake la kudhibiti safari holela za nje ya nchi kwa viongozi wa
Serikali ambazo sasa ni lazima zipate kibali chake au cha Katibu Mkuu
Kiongozi wa Ikulu. Pia ameshafuta matumizi ya fedha za serikali kwa
ajili ya maadhimisho ya siku mbalimbali za kitaifa ikiwamo ya Ukimwi
ambazo huigharimu serikali mabilioni ya fedha. Kadhalika, mwendelezo wa
utumbuaji majipu wa serikali ya Rais Magufuli umewezesha kufichua
ukwepaji kodi kupitia uondoaji mizigo bandarini uliokuwa ukilikosesha
taifa takriban bilioni 600, zaidi ikiwa ni kutokana na kontena 2,431
yaliyopitishwa kinyemela bila kulipiwa kodi. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Kodi Tanzania (Rished Bade) amesimamishwa kazi kutokana na kashfa ya
kontena, kama ilivyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), Awadh Massawe, ambaye pia uteuzi wake umetenguliwa, kuvunjwa kwa
Bodi ya Wakurugenzi ya TPA na pia maafisa takriban 50 wa mamlaka hizo
wakifikishwa mahakamani kutokana na tuhuma zinazohusiana na ukwepaji
kodi huo.
SAFARI ZA MAGUFULI
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa tangu alipoingia Ikulu Novemba 5, Rais
Magufuli hajawahi kupanda ndege ili kwenda safari yoyote na ameonekana
akitumia muda mwingi kuandaa mazingira ya utekelezaji wa ahadi zake
mbalimbali alizozitoa kwa Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika kile kinachoonekana kuwa ni
kuonyesha njia juu ya namna ya kutekeleza dhamira yake ya kudhibiti
safari holela za nje, Rais Magufuli hajasafiri kwenda ughaibuni walau
kwa gia ya kujitambulisha kwenye jumuiya ya kimataifa kama ilivyozoeleka
kwa marais wengi mara tu waingiapo madarakani .
Magufuli alisafiri kwa gari kutokea Ikulu jijini Dar es Salaam hadi
katika Ikulu Ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Novemba 17, 2015. Alikaa
Dodoma kwa zaidi ya wiki moja na kutimiza jukumu lake la kutangaza jina
la Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), kumuapisha (Waziri Mkuu) na kisha
kuzindua Bunge.
Mara baada ya kulihutubia Bunge Ijumaa, Novemba 20, Rais Magufuli
alirudi Ikulu jijini Dar es Salaam Novemba 26, ambako alijichimbia na
kuendeleza kasi yake ya ‘kutumbua majipu’. Alhamisi ya wiki iliyopita,
akiwa Ikulu jijini Dar, Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri
lililojumuisha mawaziri na naibu mawaziri 30, huku nafasi za mawaziri
wanne akiziacha wazi kutokana na kile alichodai mwenyewe kuwa ni
kuendelea kutafuta watu wenye sifa ya kuziongoza. Wizara hizo ni Fedha
na Mipango; Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Maliasili na
Utalii na pia Wizara ya Elimu, Teknolojia na Ufundi
Aidha, inakumbukwa kuwa wakati akilihutubia Bunge, Magufuli alisema
safari holela za nje huligharimu taifa mabilioni ya fedha ambazo
zingeweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo. Alitoa mfano wa
safari za nje zilizogharimiwa na serikali katika mwaka wa fedha
2013/2014 na 2014/2015 ambazo ni Sh. bilioni 356, huku Sh. bilioni 104
kati ya hizo zikiteketea kwa posho za safari hizo kwa viongozi na
maafisa wengine wa juu wa serikali.
SAFARI ALIZOJINYIMA MAGUFULI
Pengine katika kutekeleza agizo alilolitoa la kudhibiti safari za
nje, Rais Magufuli hakujihusisha na safari ya kwenda kwenye mkutano wa
wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), uliofanyika visiwa vya Malta
Novemba 27, 2015.
Badala yake, Magufuli alimtuma Balozi wa Tanzania nchini Uingereza
kwenda kumuwakilisha katika mkutano huo, akiwa pamoja na maofisa wengine
watatu na hivyo jumla yao kuwa watu wanne. Inaelezwa kuwa wakati wa
utawala wa awamu ya nne, msafara kwenye mkutano kama huo uliofanyika
Malta ulikuwa ukimhusisha Rais, baadhi ya mawaziri na maafisa wengine wa
juu serikalini ambao kwa ujumla walikuwa takriban 50.
Novemba 29, Magufuli alitakiwa kuwapo jijini Paris, Ufaransa katika
mkutano wa kimataifa wa 21 kujadili mabadiliko ya tabia nchi duniani
(COP21) ambapo wakuu wa nchi takriban 150 kutoka katika nchi 195
walishiriki, wakiwamo marais Barack Obama wa Marekani na Xi Jinping wa
China. Hata hivyo, Magufuli hakukwea ndege kwenda kuhudhuria mkutano huo
na badala yake akabaki nyumbani akiendelea kushughulikia ‘upasuaji
majipu’ , hasa TPA na TRA.
Desemba 5, 2015, Rais Magufuli hakupanda ndege pia kwenda
Johannesburg, Afrika Kusini kulikokuwa na mkutano wa tano wa wakuu wa
nchi za Afika na Rais wa China, Xi Jinping, kupitia Jukwaa la Nchi za
Afrika na China (FOCAC). Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwakilishwa
na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
SAFARI ZA KIKWETE
Siku moja baada ya kushuhudia mrithi wake akiapishwa, (Novemba 6,
2015), Rais mstaafu Kikwete alisafiri kwa ‘chopa’ kutoka Dar es Salaam
kwenda kijijini kwake Msoga, jimbo la Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani
Pwani.
Siku chache baadaye, Kikwete alikuwa jijini Addis Ababa, Ethiopia
ambako aliwahi kuripotiwa Novemba 26, 2015 akiipongeza timu ya taifa ya
Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyokuwa imetinga robo fainali ya
Kombe la Chalenji.
Novemba 30, Kikwete alikwenda Moroni, Comoro baada ya kuteuliwa
kuwa mmoja wa wajumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kwenda kuhudhuria mkutano
ulioangalia namna ya kukabili dalili za mgogoro wa kisiasa visiwani humo
kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Aprili, 2016.
Baadaye Kikwete alikwenda jijini London, Uingereza ambako
alihudhuria mkutano Mkuu wa 20 wa Taasisi ya Ushirikiano wa Usimamizi wa
Sayansi na Teknolojia kwa nchi za Jumuiya ya Madola (CPTM) na
kutunukiwa tuzo maalum kwa kutambua mchango wake katika ukuaji wa
matumizi ya Sayansi na Teknolojia, ikiwamo matumzi ya simu katika utoaji
wa huduma za fedha. Alitunukiwa tuzo hiyo Desemba 1, 2015.
Kadhalika, Kikwete alikwenda jijini Johannesburg, Afrika Kusini,
kama mualikwa, kuhudhuria Mkutano wa Tano FOCAC uliofanyika Desemba 4,
2015. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kudumisha maendeleo ya pamoja kati
ya nchi za Afrika na China, kuibua maeneo ya maendeleo yakiwamo ya
miundombinu na kuimarisha fursa za kibiashara.
Siku ya Uhuru, (Desemba 9, 2015), Kikwete alionekana akiwa na
wananchi wenzake wa Chalinze, wakishiriki kufanya usafi ili kuunga mkono
maelekezo ya Rais Magufuli ambaye aliwataka Watanzania kusherehekea
siku hiyo kwa kufanya usafi kwenye maeneo yao ili kukabiliana na
magonjwa kama kipindupindu.
WASOMI WANENA
Akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kutowahi kwenda nje ya nchi
hadi sasa, Profesa Chriss Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
alisema Rais (Magufuli) anatatua kero alizizoziona kwa wananchi wakati
akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu na hivyo, anaamini hiyo ndiyo
sababu ya kutumia muda wake wote hadi sasa akiwa nchini na kwamba, hilo
ni jambo jema.
Alisema kadri aonavyo, Rais Magufuli amejipanga vizuri katika
kutatua mambo ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa wananchi likiwamo suala
la ufisadi katika mashirika ya umma.
Aliongeza kuwa anachokifanya sasa Rais Magufuli ni sawa na mtu
aliyehamia nyumba yake mpya, hivyo hawezi kuanza kusafiri pasipo
kusafisha nyumba hiyo na kujiridhisha kuwa iko katika hali nzuri.
Mkuregenzi Mtendaji wa Asasi ya Concern For Development Initiatives
in Afrika ( forDIA), Bubelwa Kaiza, alisema Rais Magufuli amechaguliwa
na wananchi na hivyo anataka kuwatumikia na siyo kusafiri kila uchao.
Alisema kadri aonavyo, Rais Magufuli ameamua kutosafiri kwa sababu
anaamini bado wananchi wake wana matatizo mengi na hivyo anahitaji
kuyatatua kwanza ndipo aangalie uwezekano wa kusafiri ili kushughulikia
masuala ya kimataifa.
Alisema nchi kwa sasa ina matatizo mengi, ikiwamo matumizi makubwa
ya fedha katika wizara, ufisadi bandarini na Mamlaka ya Kodi (TRA)
pamoja na baadhi ya viongozi kutokwenda sambamba na mfumo anaouhitaji
yeye.
“Rais Magufuli ameangalia hapa nchini na kuona kuna matatizo mengi
… hivyo akaamua asisafiri hadi pale angalau atakapoyapunguza matatizo
hayo. Hili ni jambo zuri na anastahili pongezi,” alisema Kaiza.
Aliongeza kuwa Rais mstaafu Kikwete ni mtu ambaye anasafiri sana
kutokana na ukweli kuwa alitokea katika nafasi ya kuwa Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo ilimlazimu kusafiri mara kwa
mara.
Aliyekuwa Katibu Mtendaji Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki,
Profesa Mayunga Nkunya, alisema mambo anayoyafanya Rais Magufuli kwa
sasa ni mfano wa kuigwa kwa kiongozi yoyote.
Alisema kwa mtazamo wake, anaamini Rais Magufuli anatakiwa
kuhakikisha kuwa mabadiliko ameshayafanya ndani ya nchi kwa namna
inayotakiwa na ndipo aanze kusafiri kwenda nje ya nchi.
Kuhusu safari za Rais mstaafu Kikwete, alisema ni vyema Watanzania
wakasahau yaliyopita na kuangalia yajayo kwa manufaa ya taifa.
Septemba 15, 2015, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye
pia ni Mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama
cha Wananchi (CUF) na NLD, alimlalamikia Rais Kikwete kwa kutumia muda
mwingi wa kuwa madarakani akiwa safarini, huku akidai kuwa ametumia
takriban Sh. trilioni 4.5 kugharimia safari katika miaka yake 10 ya kuwa
madarakani.
MBATIA, MEMBE
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ilimjibu Mbatia kwa kueleza kwa kifupi kuwa safari hizo za Kikwete
(wakati huo akiwa Rais) zilikuwa na manufaa makubwa kwa taifa.
Kadhalika, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, aliwahi kukaririwa akimpongeza Rais Magufuli
kwa kuamua kudhibiti safari holela za nje ya nchi kwa kukiri kuwa wakati
wao walikuwa wakipishana na ndege hewani utafikiri Tanzania ilikuwa
ikiwaka moto.
No comments:
Post a Comment