Makontena Bandarini. |
MAKONTENA yaliyotolewa bila kulipa ushuru katika bandari ya Dar es
Salaam yamezidi kuongezeka tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipobaini
kutoroshwa kwa makontena 2,431 katika bandari hiyo bila kulipa ushuru.
Jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova, alipozungumza na
waandishi wa habari, alitaja idadi mpya ya makontena hayo iliyobainika
katika uchunguzi unaoendelea, yamefikia 2,489, sawa na ongezeko la
makontena mapya 58.
Idadi hiyo ya makontena yaliyotolewa katika bandari hiyo bila
kulipiwa kodi, ni tofauti na makontena mengine 329, ambayo yalikuwa ya
kwanza kubainika kutolewa bila kulipa kodi, lakini safari hii yakiwa
kupitia Bandari Kavu (ICD) ya Azam.
Mbali na kuongezeka kwa makontena yaliyobainika kupitishwa bila
kulipa kodi, Kova alisema pia sasa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, inawashikilia watu 40 kwa tuhuma za kula njama na kuikosesha
Serikali mapato kwa kushiriki katika ukwepaji wa kodi wa makontena zaidi
ya 2,500.
Watuhumiwa hao ambao 26 ni wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na watatu wa Bandari Kavu (ICD) ya Azam wanaohusika na upotevu wa
makontena 329 yaliyotolewa katika bandari hiyo kinyume cha taratibu.
Aidha, wengine ni watumishi 11 wakiwemo wanne waliokamatwa hivi
karibuni wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambao wanahusika na
upotevu wa makontena hayo 2,489.
Kova alisema kwa sasa watu hao wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano
wakati uchunguzi unaendelea ili kubaini waliohusika na kukosesha
Serikali mapato hayo. Alisema uchunguzi unaoendelea pia unahusisha
kupitia kumbukumbu mbalimbali na kadhia za forodha, ili kubaini mtindo
uliotumika na kuwabaini wote waliohusika katika mpango huo.
“Makontena 329 yaligundulika kukosekana katika bandari ya ICD ya Azam
kuanzia Julai hadi Novemba, mwaka huu, wakati makontena 2,489
yaligundulika kutolewa bandarini kuanzia Machi hadi Septemba, mwaka jana
kinyume cha taratibu kwa lengo la kukwepa kodi na ushuru,” alisema
Kova.
Alisema baada ya uchunguzi kukamilika majalada ya kesi yatapelekwa
kwa Mwanasheria wa Serikali ili watuhumiwa watakaobainika kuhusika
wafikishwe mahakamani.
Kigogo mmoja Aidha, Kova alisema pia wanamtafuta Wakala wa Forodha,
Abdulkadir Kassim Abdi (38), mkazi wa Temeke Mikoroshini ambaye
anahusika kutoa makontena yote 329 katika Bandari Kavu ya Azam bila
kulipa kodi.
Abdi ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Regional Cargo Services Ltd
na pia ni mkurugenzi katika kampuni nyingine za Jas Express Freight Ltd
na XL Clearing and Forwarding Co, ambazo zote kwa pamoja ndizo
zinazodaiwa kuhusika kutoa makontena hayo 329.
Kova alisema wakati wakimtafuta Abdi, wanawashikilia watu wawili
ambao ni Safari Kasera (39) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jas
Express Ltd pamoja na Godfrey Masilamba (37), ambaye ni ofisa forodha wa
kampuni hiyo.
“Mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu mtuhumiwa huyu atoe taarifa kwa
Kanda Maalumu au kwa ofisa mwingine wa Polisi aliye karibu naye au kituo
chochote cha Polisi,” alisema.
Kova aliongeza kuwa watuhumiwa hao wawili wanaendelea kuhojiwa kwa
tuhuma za kuwezesha ukwepaji wa kodi ulioisababishia Serikali hasara na
uchunguzi utakapokamilika, jalada la kesi hiyo litapelekwa kwa
Mwanasheria wa Serikali kwa hatua za kisheria.
Alisema zawadi ya Sh milioni 20 itatolewa kwa yeyote atakayetoa
taarifa za kukamatwa kwa mtu huyo, ili sheria ichukue mkondo wake, huku
akimtaka mtu huyo ajisalimishe kwa hiari yake kuliko kusubiri kukamatwa.
Katika hatua nyingine, Kova alitoa onyo kwa matapeli ambao
wamejitokeza hivi karibuni na kujifanya ni maofisa wa Serikali na hivyo
kugeuka kuwa kero kwa wafanyabiashara.
“Tumepokea malalamiko kwamba watu hao wanawapigia simu
wafanyabiashara na kuwaita au kutaka kukutana nao katika sehemu
mbalimbali za jiji kwa madai ya ufuatiliji wa makosa yanayohusu ukwepaji
kodi,” alisema Kova.
Alisema watu hao wanajifanya ni maofisa wa Usalama wa Taifa, TRA,
Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi nyingine kwa lengo la kujipatia
fedha ambapo alisema siku zao zinahesabika. Aliwataka wafanyabiashara
wanapokumbana na hali hiyo na kuwa na wasiwasi kuhusu watu wa aina hiyo,
watafute uthibitisho kutoka kwa uongozi wa juu wa TRA au Polisi.
Mabilioni Katika hatua nyingine, wakati jana ilikuwa siku ya mwisho
kwa wafanyabiashara waliohusika kukwepa kodi kutakiwa kulipa kodi hiyo
kwa hiari, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 10
kutoka kwa wafanyabiashara hao mpaka juzi.
Akizungumzia kuhusu kiasi cha fedha ambacho kimeshalipwa na
wafanyabiashara hao katika mkutano huo, Meneja wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi, Diana Masalla alisema hadi kufikia juzi katika muda wa saa
za kazi kiasi kilichokusanywa kilikuwa Sh bilioni 10. 07.
Alisema kiasi hicho kimekusanywa kutoka kwa makampuni 22 ambayo
yalihusika na uondoshwaji wa makontena 329 katika Bandari Kavu ya Azam
kinyume cha sheria na taratibu za forodha.
“Mpaka kufikia jana (juzi) katika saa za kazi tulikuwa tumekusanya Sh
bilioni 10 ambazo zimelipwa kutoka kwa makampuni 22 yaliyohusika na
uondoshwaji wa makontena bandarini kinyume cha sheria, sasa sijajua
mpaka muda huu tuko hapa kama zimekusanywa nyingine,” alisema Masalla.
Alisema kati ya kampuni hizo, kampuni sita zimelipa kodi zote
walizokadiriwa pamoja na adhabu, ambapo kampuni 16 zimelipa sehemu ya
kodi iliyokadiriwa pamoja na adhabu. Alisema thamani ya mzigo uliokuwa
katika makontena hayo ni zaidi ya Sh bilioni 28 ambazo ushuru wake
ulikadiriwa kuwa Sh bilioni 12 ambayo ndiyo kodi iliyotakiwa kulipiwa
makontena hayo.
“Aidha makampuni 26 hayajalipa kodi kiasi cha Sh 4,789,924,609.69
pamoja na kwamba zoezi la ukadiriaji limeshafanyika,” alisema. Aidha
alisema ICD ya Azam imelipa Sh bilioni nne kama dhamana na iwapo
wafanyabiashara hao watalipa kodi zote kiasi hicho kitarudishwa kwa
Bandari hiyo.
Hata hivyo, Masalla alisisitiza kuwa mizigo hiyo iliyokuwa katika
Bandari hiyo si ya Azam bali ni ya wafanyabiashara mbalimbali waliotumia
kupitishia mizigo yao katika bandari hiyo.
Aidha, alisema kuanzia leo kwa wafanyabiashara ambao hawakujitokeza
kwa hiari kulipa kodi walizokwepa mamlaka hiyo itachukua hatua za
kisheria katika kukusanya kodi. Masalla alitaka wananchi kufichua watu
wanaokwepa kodi kwa kuwa wakifanya hivyo watapata asilimia tatu ya kodi
itakayokombolewa lakini asilimia hiyo haitazidi Sh milioni 20.
Naye Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman
Kova alisema, watashirikiana na mamlaka hiyo kuhakikisha kodi yote
inalipwa na waliohusika kuikosesha mapato Serikali wanachukuliwa hatua.
Rais Magufuli alitangaza kiama kwa wafanyabiashara wote wenye tabia ya
kukwepa kulipa kodi ambapo alisisitiza kuwa kamwe Serikali ya Awamu ya
Tano haitavumilia kitendo hicho. Alisisitiza kuwa endapo mfanyabiashara
yeyote aliyekwepa kodi akakiuka kujitokeza katika siku saba alizotoa
ambazo zimeisha jana, baada ya hapo Serikali haitakuwa na huruma na mtu
yeyote na sheria itafuata mkondo wake.
No comments:
Post a Comment