KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amemjibu aliyekuwa mgombea
urais wa Chadema, Edward Lowassa, aliyedai kuwa kazi nzuri anazofanya
Rais John Magufuli, ni utekelezaji wa sera za vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za
mgombea ubunge wa Arusha, Philemon Mollel (Monaban), uliofanyika katika
kata ya Daraja Mbili jana, Kinana alisema sera ya kupambana na ufisadi
ilizungumzwa katika kampeni na Dk Magufuli peke yake na si Lowassa wala
kiongozi yeyote wa Ukawa.
Kinana alisema anamshangaa kiongozi huyo kwa kuwa mbali na kushindwa
kuzungumza wakati wa kampeni za urais, pia hakuwa na hotuba yoyote
ambayo ingeweza kukaririwa na Dk Magufuli.
Alisema Lowassa hakuweza kuzungumzia masuala yoyote ya kupambana na
ufisadi kwa kuwa yeye ni mtuhumiwa na vyama vina vyounda umoja huo ndiyo
vimekumbatia ufisadi kwa sasa.
Kwa mujibu wa Kinana, Lowassa alinadi sana mabadiliko kama angeweza
kuingia madarakani, lakini hakufafanua ni mabadiliko yapi ambayo
angeweza kuyaleta, wakati anatoka katika mfumo ule ule aliokulia kwa
zaidi ya miaka 40 akiwa ndani ya CCM na Serikali yake.
“Jamani Lowassa alisema mabadiliko lakini hao wanaotaka mabadiliko
wana umri wa ujana sawa na jua linalochomoza la saa mbili asubuhi,
wakati yeye anayedai kuleta mabadiliko ana umri wa uzee sawa na jua
linalozama la saa 12.30 jioni, si vichekesho hivyo?” Alihoji Kinana.
Alisema kutokana na ukweli huo, ndiyo maana Watanzania walipima na
kuamua kumpa ushindi wa kishindo Dk Magufuli, kutokana na uadilifu wake
pamoja na uwezo wake wa kuchapa kazi na kuamua kumnyima Lowassa na ndiyo
maana kwa sasa anajifariji kwa kusema sera zinazotekelezwa ni za Ukawa.
Akizungumzia kazi alizoanza kuzifanya Rais Magufuli, Kinana alisema
zimewakuna Watanzania wengi na kusema kuwa hiyo ndiyo kazi aliyoahidi
kwao kuifanya na kwamba anaamini ataifanya kwa dhati katika kuwapigania
wananchi wanyonge.
Mfumo CCM Akizungumzia madai kuwa hakuna kiongozi yeyote
atakayetokana na CCM anayeweza kupambana na machafu ndani ya Serikali,
kwa kuwa hilo ni suala la mfumo, Kinana alipinga na kusema si kweli.
Akifafanua alisema mfumo unaweza kubadilishwa hata na mtu mmoja kama
anavyofanya Dk Magufuli, Makamu wake, Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema moja ya mambo aliyoyaondoa Magufuli katika mfumo huo, ni
pamoja na kufuta safari za nje kwa viongozi akiwemo yeye binafsi,
kuondoa semina, warsha, makongamano, sherehe na maadhimisho mbalimbali
pamoja na posho mbalimbali na kuagiza fedha hizo kwenda katika mahitaji
mengine ikiwemo hospitalini.
Akizungumzia uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa kufanyika Desemba 13
mwaka huu, Kinana aliwataka wananchi wa Jimbo la Arusha Mjini, kuachana
na ushabiki wa vyama na badala yake wachague kiongozi kutokana na sifa
zake na kuangalia maslahi yao na siyo ya chama wala kiongozi husika.
Alisema kwa sasa wananchi wa jimbo hilo wanapaswa kuangalia maslahi
yao katika kumchagua mbunge, yakiwemo maslahi ya shule, afya,
miundombinu, amani pamoja na mambo mengine mengi, badala ya kubaki
kuimbiwa kuwa wanafundishwa kuiwajibisha Serikali huku wakibaki katika
lindi la umasikini, ukosefu wa amani na maandamano kila kukicha.
Taarifa ya NEC
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Jaji Damian Lubuva akizungumzia uchaguzi huo unaofanyika kesho,
amewasihi viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia shughuli za tume hiyo,
ili waipe nafasi ya kusimamia uchaguzi na kutangaza matokeo kwa uhuru
na haki.
Alisema Jumapili hii kutafanyika uchaguzi katika majimbo mawili
ambayo ni Handeni na Arusha Mjini, ambapo kwa Mkoa wa Arusha, idadi ya
waliojiandikisha ni 317,814 na vifaa vyote vimeshakamilika.
Jaji Lubuva alisisitiza viongozi wa vyama vya siasa na viongozi
mbalimbali kutoingilia kazi za NEC, huku akisema daftari litakalotumika
ni lile lile la Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba mwaka huu. Aliwataka
wasimamizi wa uchaguzi na mawakala, wahakikishe hakuna mtu atakayepiga
kura zaidi ya mara moja.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd ambaye ni Msimamizi wa
Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, alisema vituo vyote vya kupigia kura ni
721 na aliwaomba wapiga kura wajitokeze kupiga kura na kurudi nyumbani
kwa sababu hakuna haja ya vurugu wakati kuna maisha baada ya uchaguzi.
Alisema katika uchaguzi huo wagombea wako watano ambao ni Godbless
Lema (Chadema), Philemon Mollel (CCM), Bibi Navoi Mollel (ACT
Wazalendo), Hamisi Zuberi (CUF) na Rashidi Mkama (NRA).
No comments:
Post a Comment