Mh. Rais Dkt. JP. Magufuli, kushoto ni Katibu Kiongozi Ombeni Sefue, Makamu wa Rais Samiah Suluh, na Kulia ni Waziri mkuu Majaliwa Kasi. |
SHIRIKISHO la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso) wamepongeza hatua ya
Serikali ya Rais John Magufuli kuongeza idadi ya wanafunzi ambao
wamepata mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 34,128 mwaka jana hadi
kufikia wanafunzi 53,032 mwaka huu.
Tahliso kupitia kwa viongozi wake wakuu wamesema mabadiliko ya haraka
yaliyotokea katika uongozi wa Serikali ya awamu ya tano ni kuongeza
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi
ambao wanasoma vyuo vikuu kuongezeka.
Wakati akiwa kwenye kampeni zake za kusaka urais, Dk Magufuli
aliahidi kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapata mikopo yao bila
kusumbuliwa. Pia aliahidi kwamba wanafunzi wote wenye sifa ya kupatiwa
mikopo hiyo watapatiwa na ndivyo ilivyotokea mwaka huu.
“Kwa sababu hii sisi kama Tahliso tumeona tuandae mdahalo kutoa fursa
kwa Watanzania wengi kujadili utendaji wake kupitia hotuba yake wakati
anazindua Bunge la 11 mjini Dodoma,” alisema Mwenyekiti wa Tahliso,
Nzilanyingi John.
John alisema mdahalo huo utafanyika kesho Jumapili katika ukumbi wa
Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na utaongozwa na Mhadhiri
Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Ayubu Rioba.
Wazungumzaji katika mdahalo huo ni mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo
Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi na Dk John Jiung kutoka Idara ya
Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanadiplomasia wa
siku nyingi Balozi Christopher Liundi.
Akizungumzia sababu nyingine ya kuandaa mdahalo huo ni kujadili namna
Rais Magufuli alivyoanza kutekeleza majukumu yake kwa nafasi hiyo.
Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, John alisema mwaka huu kuna
ongezeko la wanafunzi 18,000 na akasema hayo ni mafanikio makubwa ambao
yalikuwepo kwenye hotuba ya Rais ya uzinduzi wa Bunge.
Alisema kwa upande wa bajeti iliyotumika mwaka huu ni Sh bilioni 473
wakati mwaka jana fedha zilizotumika zilikuwa ni Sh bilioni 341 ikiwa ni
ongezeko la Sh bilioni 132 katika bajeti ya mwaka huu.
No comments:
Post a Comment