Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Said Meck Sadick akiongea na waandishi wa
habari hawapo pichani ofisini kwake jana alipokutana nao kuelezea
utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa DAWASCO kuhusu usambazaji wa maji
safi na salama ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Mhandisi Cyprian Luhemeja akiongea na
waandishi wa habari hawapo pichani Dar es salaam leo alipokutana nao
kuelezea utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Serikali kuhusu
usambazaji wa maji safi na salama ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa
wa kipindupindu.(Picha zote na Ally Daud-Maelezo).
Shirika
la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) limeongeza uzalishaji
na usambazaji wa Maji safi na Salama kwa wakazi wa jiji hilo hadi
kufikia mita za ujazo 280,000 kwa siku ili kubabiliana na mlipuko wa
ugonjwa wa kipindupindu uliolikumba jiji hilo hivi karibuni.
Hatua
hiyo inatokana na utekelezaji wa maagizo ya Serikali yaliyotolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Said Meck Sadiki kuitaka DAWASCO kusambaza
maji safi na salama kwa wakazi wa jiji hilo ili kupambana na Ugonjwa wa
Kipindupindu.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkuu wa mkoa huo Bw.
Sadick amesema kuwa kufuatia maagizo aliyoyatoa kwa shirika hilo ikiwemo
kusambaza maji safi na salama kwa wananchi pamoja na kutengeneza
mifereji ya kupitsha maji taka ili yasiingiliane na mikondo ya maji
safi, DAWASCO wametekeleza kwa kiasi kikubwa maagizo hayo.
“Dawasco
imehakikisha inazalisha maji safi na salama kati ya mita za ujazo
270,000 na 280,000 kila siku kwa muda wote tangu mlipuko ulipotokea na
imehakikisha inasafisha na kusambaza kwa wananchi yakiwa katika viwango
vya ubora unaokubalika kwa ajili ya matumizi kwa binadamu” amesema Bw.
Sadick.
Ameongeza
kuwa Dawasco imejenga vizimba vya maji safi na salama kwenye maeneo
mbalimbali ambayo hayajakumbwa na yaliyokumbwa na athari za mlipuko wa
ugonjwa huo kwa jumla ya vizimba 48 ambavyo maeneo ya Kinondoni vizimba
5, Magomeni vizimba 38 na Ilala vizimba 5.
Aidha,
amesema kuwa DAWASCO kwa kushirikiana na Ofisi ya Bonde Wami Ruvu
imeanza kazi ya kusajili na kuwatambua watu binafsi wenye visima virefu
vilivyopo kisheria ambao wanauza maji kwa wananchi ili kuvitambua na
kudhibiti ubora wa maji na bei yake ambapo zoezi hili litaendelea hadi
Machi 2016.
“Dawasco
imefanya jitihada za kuweka dawa ya kuua wadudu aina ya chrolination
kwenye maboza wakati wa usajili kabla ya kuruhusiwa kufanya biashara
ya kuuza maji kwa wananchi na kuongeza sehemu za kuchota maji kwa
kuwapelekea wananchi huduma hiyo wakitumia magari yenye matanki
yaliyokuwepo kutoka 12 mpaka kufika 49 kwa sasa” aliongeza Bw.Sadick.
Katika
hatua nyingine Bw. Sadick alitoa rai kwa wakazi wa jiji hilo kuendelea
na tabia ya kufanya usafi mara kwa mara ili kutokomezakabisa ugonjwa wa
kipindupindu kwani kuanzia juzi hakuna wagonjwa waliopokelewa katika
vituo vyote.
Kwa
upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Mhandisi Cyprian Luhemeja
alisema kuwa wako katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa mifereji
ya kupitisha maji machafu ili isiingiliane na maji safi kwa wiki mbili
zijazo.
“kufikia
Februari mwakani tutaweza kutoa maji safi na salama ya kutosha kwa
wananchi wote wa Dar es salaam bila ya matatizo yoyote” alisisitiza
Mhandisi Cyprian.
No comments:
Post a Comment