MAMLAKA ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imeweka mfumo wa
kompyuta ambao unatumika kutambua wateja wake wote wanaomiliki viwanja.
Mfumo huo ambao unafahamika kwa jina la Land Management System ambao mpaka sasa umeingiza kumbukumbu za viwanja 40000.
Akizungumzia mfumo huo, Ofisa Habari wa CDA, Angella Msimbila amesema
mfumo huo unasaidia kutunza kumbukumbu za viwanja na kurahisisha mteja
kuhudumiwa haraka tofauti na awali.
“Tulikuwa tukitumia muda mrefu kutafuta mafaili na tulikuwa
tunakumbana na malalamiko mengi lakini baada ya mfumo huo kwa sasa
huduma inaenda kasi tofauti na hapo awali,” amesema msimbila.
Ametaja mfumo mwingine kuwa ni ule wa kufunga na kufungua milango kwa kutumia kadi maalum.
Amesema mfumo huo umesaidia kupambana na madalali ambao walikuwa
wakiingia ofisini hapo kiholela na kushirikiana na baadhi ya watumishi
wasio waaminifu kuuza viwanja.
Angella amesema mbali na kuwepo kwa kadi maalumu za kufungua milango
pia jengo zima la CDA limefungwa kamera kwa ajili ya kuwabaini wale wote
ambao si waaminifu.
“Kutokana na kamera hizo unaweza kugundua mtumishi katoka ndani ya
jengo na kuingia mara ngapi kwa siku na alikuwa akizungumza na nani na
kwa nia ipi,” amesema Msimbila.
Wakati huohuo, CDA imetangaza mikakati rasmi ya kuufanya mji wa
Dodoma kuwa kati ya mikoa bora na safi nchini tofauti na ilivyo sasa.
Mbali na kuufanya mji wa Dodoma kuwa bora CDA ilianza kutekeleza
kaulimbiu ya kutunza mazingira tangu Agosti mwaka huu kwa lengo la
kuufanya mji kuwa safi na wenye kuvutia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu mkurugenzi wa CDA, Paskasi
Mulagili amesema zoezi la usafi katika mkoa wa Dodoma ni endelevu na
kila mtumishi ni lazima ashiriki siku huyo ya Jumamosi.
Mkuu huyo amesema mji wa Dodoma ni kati ya miji ambayo inakusudiwa
kuwa jiji na ni mji ambao unapokea wageni wengi hivyo unatakiwa katika
kiwango cha juu cha usafi.
No comments:
Post a Comment