Mgombea wa Urais Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad |
MGOMBEA wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad amesema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imepanga
kughushi malalamiko ili kujipa uhalali wa kufuta matokeo ya uchaguzi
mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa, mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maofisa wa ZEC wamekutana katika Kiwanda cha Makonyo, Wilaya ya Chake Chake kwa ajili ya kujazishwa fomu za malalamiko ili ziweze kutumika kudai kuwa yalikuwepo malalamiko katika zoezi hilo.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa, mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maofisa wa ZEC wamekutana katika Kiwanda cha Makonyo, Wilaya ya Chake Chake kwa ajili ya kujazishwa fomu za malalamiko ili ziweze kutumika kudai kuwa yalikuwepo malalamiko katika zoezi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za chama hicho
zilizoko Mtendeni Mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema njama hizo za CCM
wameshazigundua na hawatozikubali.
Amesema, njia pekee ya kuondoa utatanishi wa uchaguzi huo ni
kukamilisha uhakiki wa majumuisho na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.
Amesema kwa upande wake pamoja na chama chake, wataendeleza jitihada
za kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na Jumuiya ya
Kimataifa, ili kukamilisha uhakiki wa majumuisho ya kura kwa majimbo 14
yaliyobaki na hatimaye kutangazwa mshindi wa urais hadi ifikapo tarehe
02 Novemba mwaka huu.
Hata hivyo amesema iwapo hakutokuwa na hatua zozote zilizochukuliwa
kukamilisha uchaguzi huo na kuheshimu maamuzi ya wananchi walio wengi
hadi ifikapo siku hiyo, viongozi wa CUF wataondoa mkono wao na kuwaachia
wananchi waweze kutafuta haki yao kwa njia za amani.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa na vitendo
vinavyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuwatesa na kuwapiga
raia wasiokuwa na hatia katika makaazi yao.
Amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa zaidi katika Wilaya za
Magharibi “A na B”, na katika tukio la hivi karibuni amesema nyumba za
raia wasiokuwa na hatia zimechomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu na
kuwafanya wananchi kuanza kupoteza uvumilivu.
Wakati huo huo Sarafina Lidwino anaripoti kuwa, CUF jijini Dar es
Salaam imeeleza wasiwasi wake wa kutokea machafuko iwapo ZEC itaendelea
‘kubana’ matokeo.
Chama hicho kimeeleza kugomea uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha
Salim Jecha wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo uliofanyika
25 Oktoba mwaka huu.
Uchaguzi huo umekuwa na upinzani mkubwa kati ya Chama cha Wananchi
(CUF) kilichomsimamisha Maalim Seif Shariff Hamad na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kilichomsimamia Dk. Ali Mohamed Shein.
Siku moja baada ya upigaji kura, Maalim Seif aliitisha mkutano na
waandishi wa habari na kueleza kwamba, amepata kura nyingi kwenye
uchaguzi huo ambapo takwimbu hizo aliziweka hadharani.
CUF imeeleza kuwa kitendo cha kutotangaza matokeo ni uvunjifu wa
Katiba na Sheria za Zanzibar ambapo wamemtaka Jecha kubatilisha uamuzi
wake hivyo kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam katika
ofisi za chama hicho, Mwenyekiti Kamati ya Uongozi, Twaha Taslima
amesema chama chao kimepitia katiba za uchaguzi zote ya Tanzania Bara na
Zanzibar na kujiridhisha kuwa, Jecha amevunja katiba.
“Tumepitia Katiba ya Tanzania ya 1977, Katiba ya Zanzibar 1984,
sheria ya Uchaguzi sura 343 ya mwaka 2010, sheria ya Zanzibar Na. 11 ya
1984 na kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za 2015 na kujiridhisha
kuwa, hakuna kifungu chochote kinachozipa mamlaka NEC na ZEC kufuta
uchaguzi uliofanyika.
“Kinachosikitisha zaidi Jecha alichukua uamuzi binafsi bila
kuwashirikisha watendaji wenzake kutoka Zanzibar na hata NEC pia
hakuishirikisha, hiyo ina maana kwamba alifanya maamuzi kwa shinikizo la
Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuona kimeshindwa kuchaguliwa na
wananchi,” amesema Taslima.
Aidha, katika taarifa ya Jacha iliyotolewa juzi ilieleza kuwa katika
uchaguzi wa mwaka huu ulikabiliwa na vikwazo vingi ambavyo alidai ndivyo
vilivyomchochea kufuta uchaguzi huo na kudai kutokana na mamlaka
aliyonayo, anauwezo wa kufuta.
Taslima amesema, tangazo hilo lilizua sintofahamu hasa pale ambapo
ilibainika kuwa, hata Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kusema
hatambui uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar.
“CUF kimesikitishwa na kinalaani hatua hiyo iliyofanywa na Jecha
kwani inaweza kuanzisha mtafaruku mkubwa na kusababisha uvunjifu wa
amani nchini. Tunawataka wasimamizi wa nje kulisimamia jambo hilo na
kuhakikisha wananchi wanapata haki yao,” amesema.
Kuhusu matokeo ya urais yaliyotangazwa jana na Jaji Lubuva kwamba
mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ameshinda urais amesema, CUF
wanaungana na msimamo uliotolewa jana na mgombea urais anayewakilisha
UKAWA, Edward Lowassa wa kutotambua matokeo hayo.
Taslima amesema ikumbukwe kuwa, CUF pia ni miongoni mwa Ukawa na kwa
msingi huo, “basi tunaungana na uamuzi wa mgombea wetu Edward Lowassa wa
kutokubaliana na matokeo yaliyotangazwa na NEC kuwa ni batili.”
No comments:
Post a Comment