Aliyekuwa Mgombea Ubunge jimbo la Mbagara kwa tiketi ya CUF, Kondo Bungo |
MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Mbagala JIJINI Dar es Salaam,
kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Kondo Bungo amepanga kwenda mahakamani
kuzuia ubunge wa Issa Mangungu kutoka CCM.
Bungo amesema kuwa, msimamizi mkuu wa uchaguzi
kwenye jimbo hilo, Fortunatus Kagimbo amekwenda kinyume na taratibu za
uchaguzi katika kumtangaza mshindi.
Mgombea huyo wa CUF amemweleza mwandishi kwamba, tayari amewasiliana
na viongozi wakuu wa CUF na kwamba, wanaendelea na taratibu za kuandaa
ushahidi.
“Nimewasiliana na viongozi wangu wakuu wa CUF kuangalia nini cha
kufanya, wamesema kuwa hakuna namna yoyote isipokuwa kwenda mahakamani.
“Tunaendelea kukusanya ushahidi na kesi hii ipo wazi kabisa.
Unawezaje kubandika matokeo bila kutangaza na wahusika kuwepo?” anahoji
Bungo.
Oktoba 29, 2015 katika hali ya kushangaza Kagimbo alimtangaza
Mangungu kuwa mshindi kwa kura 87, 249 dhidi ya Bungo aliyetangazwa
kupata kura 77,043 na Soud Rajab wa ACT Wazalendo kura 4,398.
Taarifa za awali zilieleza kuwa, uchaguzi huo umefutwa kutoka na
dosari mbalimbali ikiwemo kutoonekana kwa fomu zaidi ya 84. Matokeo ya
uchaguzi kwenye Jimbo la Mbagala yalijaa mizengwe ikiwemo kutoonekana
kwa baadhi ya fomu na kuchomwa moto kwa masanduku ya kura.
Bungo amefafanua kuwa sio tu uchaguzi wa ubunge uliohujumiwa bali pia
hujuma kubwa zilifanyika katika kubadilisha matokeo ya udiwani kwenye
kata mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Manispaa ya Temeke inakuwa chini ya
Meya wa CCM.
No comments:
Post a Comment