TTCL

EQUITY

Wednesday, March 4, 2015

Tanzania kukumbwa na ukame

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk.Agnes Kijazi (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za masika katika kipindi cha Machi mpaka Mei na kusema kuwa hali ya mvua haitarajiwi kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.
TMA imesema kuwa kutokana na kuwapo kwa kiwango hicho cha mvua, maeneo mengi yatakumbwa na ukame.
Hayo yalisemwa jana na mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alipokuwa akitoa mwelekeo wa hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi ambayo hayajapata mvua za masika za kutosha.
Aliitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua za wastani mpaka chini ya wastani kuwa ni Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Unguja na Pemba, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Simiyu.
Mikoa mingine ni Singida, Dodoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Shinyanga na Manyara ambayo pia inatarajiwa kupata kiasi kidogo cha mvua.
Dk Kijazi alisema Kanda ya Ziwa inayohusisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Kagera inatarajiwa kupata mvua za wastani mpaka juu ya wastani.
Akizungumzia utabiri huo katika sekta ya kilimo, Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karim Mtambo aliwataka wakulima wanaoishi katika maeneo yatakayopata mvua chini ya wastani kulima mazao yanayokomaa haraka na kustahamili ukame.
“Mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria inaweza kupata mvua za wastani mpaka juu ya wastani, hivyo mamlaka husika zinapaswa kujiandaa kwa hali yoyote inayoweza kujitokeza,” alisema Dk Kijazi.
“Wasimamizi wa maeneo ya utalii wachukue hatua ya kuzuia uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja katika mbuga zilizo karibu na maeneo ya Ziwa Victoria.”
Mtaalam wa Afya ya Jamii kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jubilate Benard alisema kuna hatari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kwenye maeneo yatakayopata mvua nyingi.

No comments:

Post a Comment