Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Umeshawahi kujiuliza unaweza kuufanyia nini
mshahara wa shilingi elfu 60 kwa mwezi? Basi usishangae pale
unapozidishiwa bili, unapoombwa ofa au kutegwa kwa namna yoyote ili utoe
fedha zaidi, hii yote huja ili kuongezea kipato.
Piga hesabu hizi, kodi ya chumba shilingi 15,000,
nauli ya daladala kwa siku tufanye shilingi 800 kwa siku (inaweza kuwa
zaidi kwa wanaopanda mabasi manne kwa siku) , kilo moja ya unga 900,
sukari shilingi 2,000 ukipiga na mahitaji mengine muhimu unaweza kuona
hii shilingi elfu 60 inaisha ndani ya siku mbili tu.
Sasa je wanamudu vipi gharama za maisha ambazo
zinapanda kila kukicha? Salma Chitenga (Sio jina lake halisi) anasema
kila kazi ina mbinu zake; kwani kila mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake.
Anasema yeye na wenzake sita wanaishi katika
chumba walichopewa na mmiliki wa baa anayoifanyia kazi iliyopo maeneo ya
External jijini Dar es Salaam.
“Ninaishi katika chumba tulichopewa na mmiliki wa
baa ninayoifanyia kazi ( mwenyewe analiita ‘ghetto’) akisema kuwa fedha
anazolipwa zinamsaidia kujikimu na kusaidia ndugu zake waliopo
kijijini.
“Ninalipwa shilingi 60,000 kwa mwezi, lakini kila
siku ninapewa shilingi 1,500 kwa ajili ya chakula, pia tajiri ametupa
chumba tunaishi hapa, fedha ninayopata ninanunua nguo na pia kiasi
kidogo huwa ninamtumia mama yangu kijijini,” anasema Salma.
Aisha Suleiman ni mfanyakazi wa baa na ni mama wa
mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Yeye anasema
changamoto yake kubwa iliyo mbele yake ni jinsi ya kuibana fedha ndogo
anayoipata.
“Nina mtoto mdogo ambaye anahitaji matunzo na
mshahara wenyewe ni duni, inabidi nitumie mbinu mbalimbali kujiongezea
kipato,” anasema Aisha.
Aisha anasema zipo njia nyingi za kujiongezea
kipato ambazo wafanyakazi wa baa huzitumia huku akisisitiza kuwa zipo
mbaya na nzuri.
Anakiri kuwa mshahara wa shilingi 60,000 ni mdogo
hasa kwa mtu mwenye familia kama yeye kwani lazima apange chumba na
aache hela ya chakula kila siku.
“Kwa kuwa kazi zangu ninafanya usiku, inabidi
katika hiyo fedha ninunue na maziwa ya mtoto pia nimuachie fedha kidogo
mtu anayenitunzia mtoto wangu wakati sipo, nimeshindwa kuajiri
mfanyakazi wa ndani kwa kuwa kipato changu ni kidogo,” anasema Aisha.
Waswahili wanasema njaa huleta akili na hivi
ndivyo anavyosimulia Aisha akisema kuwa msukumo wa kutafuta fedha zaidi
umetokana na majukumu aliyonayo kwa familia yake.
“Kuna njia nyingi za kujiongezea kipato, mfano ukipata wateja na
kuwapa huduma nzuri hawawezi kuondoka bila kukupa chochote au hata ofa
ya kinywaji,” anasema na kuongeza.
“Ukiwa mkarimu kwa mteja, hasa wanaume, anaweza
kukupa ofa ya bia, hapo ni ujanja wako sasa ‘kucheza’ ili ile ofa
usiinywe na badala yake uchukue fedha kwasababu wateja wengine akikupa
bia anakulazimisha uinywe,” anasema Aisha.
Aidha anasema hategemei ofa za bia peke yake,
anapohudumia wateja vizuri pia humpa kitu kidogo maarufu kwa jina la
‘tip’ akisema hizo pekee kwa siku kama mambo yakienda vizuri anaweza
kupata hata Sh 5,000.
Hii ni sehemu tu ya maisha ya wafanyakazi wa baa,
wapo ambao hulipwa kutokana na huduma waliyotoa kwa siku, wapo ambao
hulipwa kwa kuongeza bei ya kawaida ya vinywaji ya baa husika, lakini
wapo ambao hujilipa wanavyojua wenyewe.
Usikose kusoma shuhuda za wafanyakazi wa baa jumatatu.
No comments:
Post a Comment