Na Florence Majani,Mwananchi
Ni saa 9.00 alfajiri katika Kijiji cha Sintale,
wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa. Maumivu ya uchungu wa kujifungua
yamemuanza binti aitwaye Naomi John.
Amewahishwa katika zahanati ya kijiji ambayo hata hivyo haina dawa wala vifaa zaidi ya mkunga wa zamu wa siku hiyo.
Kwa kuwa hakuna usafiri wa ku mwahisha Naomi
katika hospitali ya wilaya, mkunga anajaribu kumsaidia katika
kujifungua, lakini baada tu ya kujifungua, dada huyu anatokwa na damu
kwa wingi, lakini pia, kichanga kilichozaliwa kinashindwa kupumua na kwa
bahati mbaya wote… wanapoteza maisha.
Roho za kinamama na watoto wengi zinapotea kila
kukicha kutokana na ukosefu wa huduma za afya, jambo ambalo
limesababisha idadi ya vifo vya makundi haya kuwa milioni 6.9 kwa
mwaka.
Vifo vya mama na mtoto vinaepukika na katika
kupunguza vifo hivyo wataalamu wa afya wamebuni teknolojia nyepesi na
nafuu itakayowezesha wataalamu wa afya katika eneo lolote Kusini mwa
Jangwa la Sahara kuokoa maisha ya viumbe hawa muhimu duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa,
uvumbuzi wa teknolojia rahisi utaweza kuokoa maisha ya wanawake na
watoto zaidi ya milioni 7.5 kwa mwaka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki- Moon
amesema, uvumbuzi huo ni sehemu muhimu kwa kila mwanamke na kila mtoto
duniani kwani ni miongoni mwa harakati za kuokoa maisha ya wanawake na
watoto milioni 16 ifikapo mwaka 2015.
Kupunguza vifo vya wanawake na watoto ni miongoni
mwa malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Ripoti za Umoja wa Mataifa
zinaeleza kuwa, kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa nchini kila siku, 26
hufariki kwa sababu zinazoweza kuzuilika. Wasaidie watoto kupumua
(Helping Baby Breath) ni teknolojia inayotumiwa na wataalamu wa afya
sehemu yeyote ile kuwasaidia watoto wanaozaliwa na kushindwa
kupumua.(birth asphyxia) Teknolojia hii imesaidia kupunguza asilimia 47
ya vifo vya watoto wanaozaliwa na tatizo la kupumua nchini.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake, Profesa
Cyriel Massawe anasema, iwapo teknolojia zaidi zingevumbuliwa, basi vifo
vya wanawake na watoto vingekwisha kabisa.
“Tatizo kubwa ni kuwawezesha wataalamu wa afya.
Hata kama teknolojia hizi zitavumbuliwa bado wataalamu wanahitaji
usafiri ili kuzifikisha vijijini ambako kuna vifo zaidi, ” anasema
Profesa Massawe.
Profesa Massawe anasema ni teknolojia rahisi
kutumika kwani inafundisha mbinu za kumkausha mtoto pindi anapozaliwa na
kumvalisha kifaa maalumu kinachomsaidia kupumua.
Wakunga nchini walipewa mafunzo hayo na jinsi ya
kutumia kifaa aina ya ‘Neonatalie’ ambacho ni kifaa rahisi kutumiwa na
mtaalamu yeyote hata mkunga wa jadi ili kumsaidia mtoto mwenye matatizo
ya kupumua pindi tu anapozaliwa. Teknolojia nyingine inayofanana na HBB
ni ‘Bubble CPAP,’ kifaa cha njia ya upumuaji ambacho huwasaidia watoto
waliopata matatizo ya mfumo wa upumuaji ikiwemo nimonia.
Kifaa hiki huingiza hewa safi katika mapafu ya mtoto. Kwa
gharama ya Sh640,000 kifaa hiki kinachotumia pampu na chupa ya maji
kinaweza kuokoa maisha. Simu za Oximeter ni simu za gharama nafuu
zenye kifaa kinachosimamiwa kinachopima kiwango cha oksijeni katika
damu na kuwapa taarifa watendaji wengine wa afya kupima nimonia.
Teknolojia ya simu kupima saratani ya shingo ya
kizazi nayo imo kwenye orodha hii. Wataalamu wa afya wa Tanzania na
Canada wameshirikiana katika kupunguza vifo vya wanawake wenye saratani
ya shingo ya kizazi kwa kutumia simu za mkononi katika maeneo ya
vijijini.
Timu ya wataalamu wa afya itakwenda katika maeneo
ya pembezoni nchini ili kuwapima wanawake wanaoishi mbali na huduma za
afya. Wauguzi ambao watapewa vifaa vya kupimia saratani hiyo pamoja na
simu zenye teknolojia.
Watatakiwa kutumia simu kuchukua picha za kizazi
cha mama na kuzituma kwa njia ya ujumbe kwa wataalamu wa afya. Wataalamu
walio katika hospitali zenye vifaa wataichunguza picha ya kizazi.
Watarudisha majibu kwa waugu na kuanzishiwa tiba.
Ipo pia teknolojia ya Kit Yamoyo. Hiki ni
kisanduku kilicho na dawa za kuzuia kuhara, pamoja na sabuni. Teknolojia
hiyo ambayo kwa jina jingine inaitwa Cola Life inasambazwa katika
masanduku ya vinywaji vya Coca Cola ili kuwafikia watu wengi zaidi hata
walio mbali vijijini. Magonjwa ya kuhara kwa watoto yanasababisha vifo
zaidi ya 600,000 kila mwaka.
Anti–shock garment. Hiki ni kifaa kinachofungwa
katika sehemu ya chini ya mwili wa mama ili kuzuia damu kutoka kwa wingi
baada ya kujifungua na vilevile kifaa hiki husaidia kuhifadhi damu
katika ogani ya moyo, mapafu na ubongo hadi mama atakapopewa huduma
zaidi.
Mhadhiri wa Ukunga katika Chuo cha Ukunga
Muhimbili, Dk Selbada Leshabari anasema mama anapotoka damu kwa wingi
ogani ya moyo, mapafu na ubongo hupata mshtuko kwa sababu damu
hujikusanya sehemu za chini na miguuni.
Majaribio ya uvumbuzi huu yalifanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu na katika kambi mbili za wakimbizi.
Kifaa hiki huifanya damu itembee katika sehemu nyingine za mwili na hivyo kuzuia kifo.
Kutoka damu kwa wingi ni sababu kuu ya vifo vya kinamama na huua wanawake zaidi ya 72,000 kila mwaka.
Chlorhexidine. Hizi ni dawa zinazotolewa kwa
gharama nafuu ili kuzuia maambukizi katika kitovu cha mtoto mchanga.
Maambukizi katika kitovu husababisha vifo kwa watoto kwa asilimia 12
kila mwaka.
Rotovac, ni chanjo kwa ajili ya kuzuia virusi
vinavyosababisha ugonjwa wa kuhara ambao ni maarufu katika nchi
zinazoendelea. Chanjo hii inayotolewa pamoja na madini ya zinc na ORS
ina uwezo wa kuondoa ugonjwa wa kuhara.
No comments:
Post a Comment