Kodi ya magari kulipwa kwa simu
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
imesema inaanzisha mfumo wa wamiliki wa magari kulipia leseni za magari
kwa kutumia simu za mkononi, ili kuondoa foleni katika ofisi za mamlaka
hiyo.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Fedha wa TRA,
Saleh Mshoro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ulipaji kodi kwa njia ya mtandao utakaoanza
rasmi Julai mosi mwaka huu.
Mshoro alisema kumekuwa na msongamano wa walipaji
wa leseni hizo kwa sababu ni benki chache zinazotumika katika malipo ya
kodi hiyo.
“Kuanzia mwezi ujao wateja wetu watakuwa wakilipia
leseni hizo kwa kutumia simu za mkononi kwa kutuma namba ya gari lake
TRA ili aweze kuelezwa anatakiwa alipe shilingi ngapi halafu atalipa
kiasi hicho kwa njia ya simu na kisha kwenda kwenye ofisi za TRA
kuchukua leseni yake,” alisema.
Alisema benki zote zilizopo nchini zitaingizwa katika mfumo huo ili kurahisisha ulipaji na kuondoa foleni zilizopo hivi sasa.
Akizungumzia mfumo wa kulipa kodi kwa njia ya
mtandao, Mshoro alisema utatumika kwa wafanyabiashara ambao hulipa
kuanzia Sh5 milioni na kuendelea.
Alisema kwa wale wanaolipa chini ya hapo wataendelea kutumia mfumo wa sasa.
“Utaratibu huu utarahisisha ulipaji wa kodi na kupatikana kwa taarifa mbalimbali za kodi kwa haraka,” alisema Mshoro.
Mshoro alisema mlipaji kodi atalipia katika benki
yoyote na taarifa hizo zitafika TRA kwa haraka hivyo kurahisisha
ufanyaji wa biashara za wateja wao.
Alisema mfumo huo umefanyiwa majaribio kwa miezi
sita na kuonekana unafaa na wameshirikiana na Benki Kuu ya Tanzania
katika kufanikisha utaratibu huo.
Alielezea matumaini kuwa wamiliki wa magari kote nchini, watafurahia mfumo huo.
No comments:
Post a Comment