Hatima ya Mbilinyi mikononi mwa DPP
Dodoma. Hatma ya kufikishwa mahakamani kwa
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘’Sugu”( Chadema), iko mikononi
mwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime,
alisema jana kuwa jeshi lake limekamilisha upelelezi kuhusu tuhuma
zinazomuhusu Sugu na kwamba wanasubiri maelekezo ya kumfikisha
mahakamani.
Mbilinyi alikamatwa juzi mchana akiwa mjini Dodoma
anakohudhuria vikao vya bunge na habari zilisema anatuhumiwa kutoa
maneno ya kashfa na uchochezi dhidi ya Waziri, Mkuu Mizengo Pinda.
Inadaiwa kuwa mbunge huyo amefanya hivyo kupitia mtandao wa kijamii.
Kamanda huyo alisema jana Mbilinyi aliripoti
katika Kituo cha Polisi Kati kama alivyotakiwa na jeshi hilo na
kuongezewa dhamana hadi leo anapotakiwa kurudi tena kusikiliza hatma
yake.
Misime alisema “jeshi hilo liliamua kumkamata
mbunge huyo baada ya kugundulika kuandika maneno ya kumtukana Waziri
Mkuu kuhusu utendaji wake na kumdhalilisha katika siku ambayo
hakuitaja.”
Taarifa zisizo rasmi zinaonyesha kuwa, mbunge huyo
anatuhumiwa kuandika maneno hayo ya kashfa kufuatia kauli ya Pinda hivi
karibuni kuhusu kuwataka polisi kuwapiga raia wasiotii sheria. Alikuwa
akijibu swali la papo kwa papo ndani ya Bunge wiki iliyopita ambapo
alisema Serikali imechoshwa na vitendo vya watu kutotii sheria na kutoa
mfano wa matukio ya Mtwara na Arusha.
Huko Mtwara polisi walitumia nguvu zaidi
kuwadhibiti wananchi waliokuwa wakikataa gesi isisafirishwe kwa njia ya
bomba kwenda Dar es Salaam, wakati huko Arusha, walifanya hivyo katika
kuwatawanya wafuasi wa Chadema, waliokuwa wakishiriki katika tukio la
kuaga maiti.
Baadhi ya watu wakiwamo wanaharakati walisema kauli hiyo inaweza kuleta chuki kati ya polisi na wananchi.
No comments:
Post a Comment