TTCL

EQUITY

Friday, June 28, 2013

‘Kuweni makini dhidi matangazo ya ajira’



 
WATANZANIA wametakiwa kujihadhari na mitandao ya kijamii inayo andaa matangazo mbalimbali yanayo husiana na mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwani matangazo hayo si ya kweli.
Mitandao hiyo inapotosha Umma ilhali wakijua wazi kuwa taarifa hizo wanazochapisha ama kuziandika katika mitandao hiyo ya kijamii siyo sahihi na hazijatolewa na Sekretarieti ya ajira .
Akizungumza na Wanahabari Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Ajira, Xavier Daudi aliitaja mitandao hiyo kuwa ni WWW.eastafricajobscareer.com ambao umetoa matangazo yanayoonesha mwisho wa kupokea maombi ni Julai 14 na Ogasti 10 mwaka huu.
Alisema wananchi wote wanatakiwa kufahamu kuwa Sekretariet hiyo ndiyo chombo pekee kilichoundwa kwa mujibu wa sheria kushughulikia mchakato wa masuala ya ajira katika utumishi wa umma.
Katibu huyo alibainisha kuwa Sekretarieti hiyo haiwajibiki wala haitawajibika kwa taarifa ama matangazo yanayohusu mchakato wa ajira katika utumishi wa umma yaliyotolewa na mitandao hiyo ya kijamii kwani matangazo ya Sekretarieti yanadumu kwa muda wa siku saba mpaka 21.
Alitoa rai kwa wadau wa Sekretarieti ya ajira wanaotafuta fursa ya ajira katika utumishi wa umma wajaribu kijiridhisha kwa kuthibitisha taarifa za nafasi za ajira wanapoona matangazo ya nafasi katika vyombo  vya habari kwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz au kupiga simu +255 687624975.
Aliwataka waliotuma maombi ya nafasi za kazi kwenye tangazo la kazi lililotolewa Machi 26 mwaka huu kwa lugha ya kiswahili kwa kada mbalimbali kutambua fursa za ajira ni za ushindani unaozingatia sifa na uwezo wa mwombaji.
Alifafanua kuwa idadi ya wahitimu ni kubwa kuliko miaka iliyopita hivyo wanahitaji watumishi wenye uwezo wa kitaaluma na kiutendaji kwa lengo la kuwahudumia watanzania kwa ufanisi  wa hali ya juu ni vema waombaji wakasoma tangazo na kulielewa ili waweze kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.
Alisema Sekretarieti hiyo inakabiliwa na changamoto ya watu kughushi vyeti vya elimu na vya kuzaliwa jambo linalosababishwa na ufaulu duni wa baadhi ya wahitimu hivyo watashirikiana na mamlaka zinazohusika kubainisha uhalali wa vyeti husika.

No comments:

Post a Comment