Mawakala wa kuuza wasichana mbaroni
Sakata
la biashara ya binadamu ambalo limeibuka kwa kasi nchini limeanza
kufanyiwa kazi na serikali baada ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Maji
kuwatia mbaroni mawakala watano ambao ni wanawake wakituhumiwa
kujihusisha na biashara hiyo.
Kamanda
wa Polisi wa Kikosi cha Maji, Mboje Kanga, akizungumza na NIPASHE jana
kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na jeshi hilo kukabiliana na tatizo
hilo, alisema mawakala waliokamatwa ni wakazi wa Zanzibar na kwamba
hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi yao.
Kamanda
Kanga ambaye hata hivyo, hakutaja majina ya mawakala hao, alisema
walikamatwa kati ya Januari 23 na 24, mwaka huu wakiwa na watoto watano
ambao waliwanunua kutoka mikoani.
Alisema
watoto ambao ni wanafunzi wa shule za msingi walikamatwa wakitaka
kusafirishwa na mawakala hao kwenda Zanzibar, umri wao ni kati ya miaka
14 na 15 na walitoka katika wilaya za mikoa ya Ruvuma, Tabora na Mtwara.
Aliongeza
kuwa katika mahojiano na watoto hao walisema walipata ridhaa ya
kuchukuliwa na mawakala hao ambao haijafahamika baada ya kusafirishwa
kwenda Zanzibar wangepelekwa katika nchi gani.
“Biashara
ya binadamu imeshamiri sana nchini, lakini tumejipanga kukabiliana
nayo, tutaendelea kuwasaka mawakala wengine zaidi wanaojihusisha na
biashara hiyo,” alisema Kamanda Kanga.
Uchunguzi
uliofanywa na NIPASHE, umebaini kuwa biashara hiyo iliibuka kuanzia
Desemba mwaka jana na kushika kasi Januari mwaka huu na wanaosafirishwa
wengi ni watoto wa kike kutoka mikoa mbalimbali nchini. Wapo wachache wa
kiume pia.
Uchunguzi
huo ulibaini kuwa mikoa ambayo watoto hao wananunuliwa na mawakala
kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchi za Uarabuni kufanya kazi mbalimbali
zikiwamo za ndani ni Mtwara, Lindi, Manyara, Pwani, Tabora, Ruvuma,
Tanga na Shinyanga.
Jana gazeti hili liliandika habari kubwa ikielezea jinsi watoto hao wanavyosafirishwa kwenda kutumikishwa na maeneo wanayotoka.
Watoto
hao ambao NIPASHE iliwagundua, kuwaona na kuzungumza na baadhi yao
lakini majina yao tuliyasitiri kwa sababu za kimaadili wana umri wa
miaka 14 na 15 wote kutoka kijiji cha Nakapanya wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma; mmoja mwenye umri wa miaka minane anatoka mkoa wa Tabora;
wakati mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 15 anatoka kijiji cha
Mkangula mkoa wa Mtwara, ilhali mwenzake kutoka kijiji cha Mbembaleo
mkoani Mtwara ana umri wa miaka 14.
Pia
NIPASHE iliripoti kuwa Januari 25, mwaka huu watoto waliokamatwa
bandarini wakitaka kusafiri kwenda Zanzibar ni binti mwenye umri wa
miaka 13 kutoka kijiji cha Manoro wilaya ya Lushoto mkoa wa Tanga;
mvulana mwenye umri wa miaka 13 kutoka wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma
na binti mwenye umri wa miaka 12 kutoka Tunduru Mjini.
Wengine
ni binti mwenye umri wa miaka 14 kutoka kijiji cha Namalumbusi wilaya
ya Masasi mkoa wa Mtwara, mvulana mwenye umri wa miaka 12 kutoka mkoa wa
Manyara na mvulana mwingine mwenye umri wa miaka 10 kutoka wilaya ya
Nachingwea mkoa wa Lindi.
Watoto
waliokamatwa Januari 26, mwaka huu ni binti mwenye umri wa miaka 12
kutoka kijiji cha Ndanda mkoa wa Mtwara; binti mwenye umri wa miaka 13
kutoka kijiji cha Mteruka wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi na mwingine
mwenye umri wa miaka 13 kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja mkoa wa Mtwara.
Wengine
ni binti (13) kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Mtwara, binti (14)
kutoka mkoa wa Manyara na binti (17) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha
tatu kutoka kijiji cha Kokoro wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga.
Januari 27, mwaka huu alikamatwa binti (14) mkazi wa Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.
Taarifa
kutoka ndani ya Kituo cha Kikosi cha Polisi Maji, zinaeleza kuwa watoto
hao wakishakamatwa na kuzuiwa kusafiri, wamekuwa wakichukuliwa maelezo
na baadaye kuachiwa warejee walikotoka, lakini wengine hushindwa kurejea
kutokana na kukosa nauli hivyo mawakala kupanga njama za kuwasafirisha
kinyemela.
Taarifa
zinaonyesha kuwa mawakala hao wakishafanikiwa kuwapata watoto hao
kutoka katika mikoa hiyo huwapeleka jijini Dar es Salaam na baadaye
kusafirishwa kwa usafiri wa majini kutoka Bandari ya Dar es Salaam
kwenda Zanzibar.
Imebainika
kuwa watoto hao wakifikishwa Zanzibar hukutana na watu maalum ambao
huwapokea na kufawanyia mipango ya kuwasafirisha kwa usafiri wa ndege au
wa majini kwenda Uarabuni ambako hutumikishwa kazi mbalimbali.
Mawakala
hao wakishafanikiwa kuwasafirisha kutoka Bandari ya Dar es Salaam
hulipwa wastani wa Dola za Marekani 5,000 (Sh. milioni 8) kwa kila mtoto
wanayefanikisha kumvusha kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.
Kwa
mujibu wa uchunguzi huo, ili kuhalalisha safari za kuwasafirisha watoto
hao, mawakala hula njama na baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa
kwa kuandika barua zinazoelezea sababu za watoto hao kwenda Zanzibar.
Wastani wa watoto kati ya watano hadi 10 hufika katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafiri kwenda Zanzibar kila siku.
Uchunguzi
huru wa NIPASHE umebaini kuwa Januari 23, mwaka huu waliwatilia shaka
na polisi na kuzuiwa kusafiri ni watoto wanne ambao walifunguliwa jalada
la upelelezi kituo cha Polisi Maji ambazo ni MUD/RB/40/2013 na
MUD/RB/36/2013.
No comments:
Post a Comment