Kabila la Waha limesheheni mila na deturi zinazoliwezesha kabila hilo
kuwa na sifa za kipekee ikiwa ni pamoja na utaratibu maalumu wa kulinda
afya ya mama na mtoto ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi pia
vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa kitabu cha Waha, Historia na Maendeleo kilichoandikwa
na P. Chubwa, Waha wanathamini mtoto kuanzia siku mimba inapotungwa
ambapo wazazi wa mtoto, ndugu, jamaa, ukoo na majirani na jamii nzima
hutakiwa kutoa ushirikiano katika malezi ya mimba hadi mtoto
atakapozaliwa. Chubwa anaeleza kuwa mila na desturi za Waha zilithamini
sana ustawi wa jamii, hivyo maisha ya mtoto yajadiliwa kabla na baada ya
kuzaliwa na kuendelea kutathminiwa hadi siku ya kufa kwa sababu
wanaamini kuwa kuna maisha baada ya kifo.
Mafunzo kwa wanandoa Waha wana desturi ya kutoa mafunzo maalumu kwa
vijana waliofunga ndoa ili kuwaandaa kuwa wazazi wazuri. Mafunzo hayo
hufanyika kwa nadharia na kwa vitendo ambapo vijana waliyofunga ndoa
hufundishwa miiko na mbinu za kulea mimba ili kupata watoto wenye afya
njema na kuepuka vifo vinavyotokana na uzazi.
Kwa kuwa miaka ya nyuma wasichana wengi waliolewa katika umri mdogo
wakwe zao waliwafundisha jinsi ya kutambua dalili za mimba na kuhimizwa
kuwaarifu waume zao mara baada ya kuona dalili hizo. Mume akishapata
taarifa, huchunguza mabadiliko ya mwili ya mkewe na anapothibitisha kuwa
mkewe ni mjamzito, taarifa husambazwa kwa ndugu, jamaa marafiki na
majirani ili waweze kutoa huduma kwa mama mjamzito.
Miiko wakati wa ujauzito Chubwa anasema mimba hulelewa na jamii nzima
inayomzunguka mama mjamzito ambapo hata wapita njia hukuchua tahadhari
na kufuatilia mwenendo wa mama mjamzito ili asikiuke miiko na kufanya
mambo ambayo yanaweza kumdhuru mtoto. Mama mjamzito alipangiwa mambo ya
kufanya na kutofanya katika kipindi chote cha ujauzito. Wazee
walimuagiza mjamzito kula chakula cha kutosha kila anaposikia njaa ili
aweze kuzaa mtoto mwenye afya nzuri.
Pia aliagizwa kufanya kazi kama kawaida, kupokea mabadiliko ya mwili
na kuyakubali hasa kitendo cha tumbo kuongezeka kwa haraka, mtoto
kucheza au kujigusagusa ndani ya tumbo. Mjamzito katika mila ya Kiha
anakatazwa kucheka au kudharau watu wenye ulemavu ili asije kuzaa mtoto
mwenye ulemavu na mwiko huu unaendelea hadi sasa kama njia mojawapo ya
kuhamasisha jamii kuacha kuwanyanyapaa na kuwadharau watu wenye ulemavu.
Kama ilivyo kwa makabila, Waha nao walikuwa na mila potofu kuwa
mwanamke akila mayai atazaa mtoto asiye na nywele hivyo ilikuwa mwiko
kwa wajawazito kula mayai. Hata hivyo tafiti za kitaalamu zimebainisha
kuwa mayai ni miongoni mwa vyakula vyenye virutubisho hivyo wajawazito
wanashauriwa kula mayai, mboga, matunda, maini, samaki, nyama na kunde
ili kuboresha afya ya mama na mtoto.
Utafiti wa sasa pia unaonesha kwamba wajawazito kukatazwa kula vitu
vyenye protini nyingi yakiwemo mayai lilikuwa ni suala muhimu na la
kisayansi kwa zama hizo. Hii inatokana na ukweli kwamba wakati huo
hakukuwa na hospitali za kisasa na hivyo walikuwa wanaepuka mama kuzaa
mtoto mkubwa ambaye inaweza kuwa shida kutoka. Uaminifu katika ndoa
Wanawake walipaswa kuwa na nidhamu na uaminifu wa hali ya juu katika
ndoa ili kuepuka kupata magonjwa ya zinaa ambayo huweza kusababisha
madhara kwa mtoto kabla na baada ya kuzaliwa.
Kadhalika Waha wana mafunzo maalum kwa mama mjamzito kwa ajili ya
kumuandaa kisaikolojia ili aweze kujifungua salama. Wazee wa kike
walimsimulia mjamzito juu ya uchungu anaopata mjamzito kabla ya
kujifungua. Walifundishwa kutofautisha maumivu ya kawaida na maumivu ya
uchungu na kutakiwa kujikaza pale atakapopatwa na uchungu. Mwanamke wa
Kiha alifundishwa mbinu za kuwa na ujasiri na kutoona aibu ili aweze
kujifungua kwa urahisi.
Pia alifundishwa kusukuma mtoto kwa kuzingatia maagizo ya mkunga wa
jadi. Baadhi ya mambo yamebadilika na hivi sasa wanawake wanashauriwa
kufika vituo vya afya na kuzingatia ushauri wa daktari na maagizo ya
mkunga wa kituo cha afya ili waweze kujifungua salama. Mafunzo kwa
wanaume Pia Waha wanatoa mafunzo kwa wanaume wanaotarajia kupata mtoto.
Mwanaume alifundishwa jinsi ya kutoa matunzo ya kipekee kwa mke wake
katika kipindi chote cha ujauzito.
Alifundishwa mbinu mbalimbali za kupokea na kukubali mabadiliko ya
mwili wa mkewe na kuendelea kumpenda kwa dhati. Pia walifundishwa jinsi
ya kushinda vishawishi na tamaa za mwili wakati mke akiwa mjamzito. Pia
waliaswa kutokutoka nje ya ndoa kwa kuwa kitendo hicho kinaweza
kusababisha maradhi hasa magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kumuathiri
mama na mtoto anayetarajia kuzaliwa.
Wanandoa wanaotarajia kupata mtoto walifundishwa jinsi ya kujithamini
na kujiweka tayari kupokea kiumbe kipya kinachohitaji upendo wa wazazi
wote wawili, malezi bora, usalama, chakula, mavazi na malazi. Wanandoa
walifundishwa na kuhimizwa kuzungumzia habari za mimba kwa wanaukoo wa
mwanaume kwa kuwa mtoto hurithi kwa baba yake. Mume na mke walifundishwa
kutenda kwa imani kwamba ni la tunda, baraka na kiini cha ndoa,
familia, ukoo na jamii yote katika eneo la Buha.
Imani ya uwepo wa Mungu Waha wanaamini kuwa Muumba wa Mbingu na dunia
hupita katika nyumba za watu usiku na kukamilisha kazi ya uumbaji kwa
kutumia maji. Kutokana na imani hiyo wazee waliwahimiza wanandoa
kuhakikisha wanaweka maji ndani ya nyumba hasa usiku kama ishara ya
kusaidiana na Muumba katika uumbaji wake. Wanandoa hao walihimizwa
kukubaliana na matokeo ya muumbaji na kupokea kwa upendo mtoto yeyote
atakayezaliwa ili kuepuka vitendo ya ubaguzi wa kijinsia.
Hata hivyo, wanawake wa Kiha hupendelea mtoto wa kwanza awe msichana
ili aweze kumtumia kama msaidizi wake wa kazi za nyumbani. Mtoto wa kike
au wa kiume? Wanawake wanaamini kuwa mtoto wa kwanza akiwa wa kike
nyumba inachangamka na kuwa na baraka zaidi kwa kuwa msichana huyo
atasaidia kazi za kupika, kuteka maji, kutafuta kuni na kubeba wadogo
zake.
Wanaume nao hupenda mtoto wa kwanza awe mvulana kwa kuwa uzao wa
kwanza ukiwa wa mtoto wa kiume huwa na uhakika wa kupata mrithi wa
kuendelea na kudumisha ukoo wa baba yake. Ingawa kila mwanandoa alivutia
kwake, Waha wanaona umuhimu kupata watoto wa kike na wa kiume kwa
kuchanganya. Familia yenye watoto wa kike na wa kiuume huwa na furaha
zaidi kwa kuwa watoto wa kike walitumika kuboresha maisha ya mtoto wa
kiume ambaye alionekana kuwa na thamani kubwa zaidi.
Hivyo watoto wa kike katika familia walitumika kufanyakazi na wakati
mwingine walilazimishwa kuolewa mapema ili mahari yao itumike kwenda
kuposa mke wa mtoto wa kiume. Mtoto kukaribishwa duniani Mtoto
anapozaliwa alifanyiwa mila na ibada ya kumkaribisha duniani ili aweze
kuishi kwa amani na usalama. Jamii iliendelea kuendelea kumtembelea mama
aliyejifungua kwa lengo la kumpa hongera na kuangalia afya na maendeleo
ya mtoto.
Baada ya siku 40 mtoto alifanyiwa sherehe maarufu kwa jina la Idenga
ambayo ni mahususi kwa ajili ya kumtoa mtoto nje aweze kuonekana
hadharani. Sherehe hiyo inahudhuriwa na wanawake ambao hukusanyika kisha
kuimba na kucheza huku wakipongeza mama mzazi. Pia sherehe hiyo
hutumika kama semina isiyo rasmi ambapo wanawake huhimizana na
kuhamasishana kuboresha afya ya uzazi salama.
No comments:
Post a Comment