Dawa za binadamu za Sh 2 bilioni zateketea
Na Bakari Kiango, Mwananchi
(email the author)
“Moto huu umeteketeza kila kitu kilichomo humu ndani na kuna dawa zingine zimekuja jana tu hapa,”
Dar es Salaam. Vifaa tiba na dawa za binadamu
zenye thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni vimeteketea kwa moto katika
bohari ya Pyramid Pharma ambayo inahifadhi dawa hizo na kuzisambaza
iliyopo eneo la Mwenge jijini.
Moto huo ambao chanzo chake bado hakijajulikana ulianza kuteketeza vifaa hivyo jana saa 3 asubuhi katika bohari hiyo.
Meneja Operesheni wa Bohari hiyo, Naftal Philip
aliwaambia waandishi wa habari kwamba vifaa na dawa vyote vilivyokuwa
kwenye ghala vimeteketea na hakuna kilichobaki.
Alisema baada ya kutokea kwa moto walifanya
jitihada za kutafuta vikosi vya uokoaji, lakini kikosi cha zimamoto cha
jiji kiliwahi katika tukio dakika 20 baada ya kupewa taarifa.
“Moto huu umeteketeza kila kitu kilichomo humu ndani na kuna dawa zingine zimekuja jana tu hapa,” alisema Philip.
Alibainisha kuwa katika tukio hilo hakuna madhara
yoyote kwa binadamu na kwamba bado wanaendelea kufanya tathmini ili
kubaini chanzo cha moto huo ambao umesababisha hasara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni,
Charles Kenyela alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema bado taarifa hizo
hazijafika ofisini kwake na kwamba apigiwe baada ya nusu saa.
“Bado sijapata taarifa hizo, naomba unipigie baada ya nusu saa nadhani nitakuwa nimepata taarifa,” alisema Kamanda Kenyela.
Ofisa wa Kikosi cha Uokoaji cha jiji, Sanjeti Meja
Kulwa Nzelekela aliwaambia waandishi wa habari kwamba chanzo cha moto
huo inasemekana ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika ghala hilo.
“Tulifika eneo la tukio dakika 20 baada ya
kupigiwa simu na tulienda pale na magari manne, na kampuni hiyo (Pyramid
Pharm) waliamua kutuongezea nguvu kwa kuwa na magari binafsi ya
kusambaza maji ili kutujazia maji kupunguza usumbufu wa kwenda na kurudi
kufuata maji,” alisema Meja Nzelekela.
No comments:
Post a Comment