TTCL

EQUITY

Tuesday, February 7, 2017

SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA LAENDELEA KUCHUKUA SURA MPYA BUNGENI

Kufuatia Sakata la dawa za kulevya kuendelea kurindima nchini na Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiongoza katika vita hivi, jana mjini Dodoma Bungeni, wabunge wanataka orodha ya ‘wauza unga’ ambayo Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwahi kusema anayo ili ifanyiwe kazi na Rais wa sasa Dkt John Magufuli.
Halima Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema), alimtaka Rais Magufuli kuacha kuendesha nchi kwa sanaa na kutafuta habari zake zipewe uzito katika vyombo vya habari, badala ya kushughulikia tatizo.
Aliongeza kuwa mwaka 2016/2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini ambayo ndiyo yenye dhamana ya vita hiyo haikupata fedha za maendeleo. “Leo bajeti ya tume ni sifuri halafu anasimama mkuu wa nchi anasema vita ipiganwe. Tuache kutafuta vichwa vya habari kwenye vyombo habari,” alisema Mdee.
Pia aliongeza, “Vita hii inahitaji utashi wa kisiasa. Kikwete alisema anawajua wauza unga kwamba ana orodha. Alipoondoka Ikulu si aliacha mafaili? Orodha unayo hapo Ikulu tusicheze na akili za Watanzania,” alisema.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema Rais Kikwete aliwahi kuutangaza wazi wazi kuwa anayo orodha ya vigogo wa dawa za kulevya hivyo alitaka wakamatwe ili watumiaji waachiwe. “Kikwete alisema anayo orodha ya wauza dawa za kulevya. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mwigulu Nchemba) amfuate kule Msoga ili ampe hiyo orodha. Naamini watumiaji wataachiwa,” alisema. “Vita ya dawa za kulevya siyo ya Paul Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam), hii ni vita ya Serikali na naamini itamuunga mkono. Mtu akipimwa akionekana ni mtumiaji atusaidie kumpata muuzaji,” Bashe alisema.

No comments:

Post a Comment