TTCL

EQUITY

Wednesday, February 15, 2017

Mwanamke kuumwaumwa kabla ya hedhi (Premenstrual Tension)

 
KUMEKUWA na hali fulani ambayo huwapata baadhi ya wanawake hasa wa umri kati ya miaka ishirini na tano hadi arobaini, kujihisi wagonjwa siku chache kabla ya kupata damu ya hedhi. 

Hali hii huwafanya wanawake hawa wakapime presha kama imepanda au imeshuka, mara wakapime malaria, lakini mwisho wa siku vipimo vyote huonekana vipo sawa na akishapata tu damu ya hedhi kila kitu mwilini mwake kinakuwa sawa.

CHANZO CHA TATIZO
Kama tulivyoona, tatizo hili la kujihisi mgonjwa kabla ya hedhi Premenstrual Tension huwapata wanawake wenye umri wa miaka 25 hadi 40. Hadi sasa chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijajulikani ingawa kisayansi inasadikiwa huwatokea wanawake wanapokuwa na kiwango kikubwa cha homoni ya Progesterone na Estrogen kwenye miili yao hasa kipindi cha pili cha mzunguko wa hedhi, yaani baada ya upevushaji wa mayai Ovulation.
Hali hii ya kuwa na kiwango kikubwa cha homoni hizi mwilini husababisha kuongezeka kwa mgandamizo wa madini ya Sodium mwilini ambayo hufanya mkusanyiko mkubwa wa maji mwilini na kufanya mwili uwe mzito na kiwango hicho cha maji husababisha kuvimba kwa tishu za neva na hata maji hayo hujikusanya hadi kwenye ubongo na kukuletea hali iitwayo Cerebral Edema ambapo pia tishu za ubongo huvimba kipindi hicho.

JINSI MWANAMKE ANAVYOJIHISI
Baada ya hali hii kutokea, mwanamke huanza kujihisi mgonjwa na atakuambia hajui hata nini kinamuuma, kichwa huuma sana, maumivu ya mwili, mwili huchoka huhisi kichefuchefu, anakuwa mkali na hana raha, kila sehemu ya mwili inauma, akili inakuwa haipo sawa, wakati mwingine anashindwa kuendelea na kazi zake, hupatwa na msongo wa mawazo na kujikuta anaweza hata kugombana na watu wake wa karibu.
Hali hii inapoanza kutokea huwa ni taratibu na kabla ya kupata damu ya hedhi humtesa mwanamke takriban siku saba hadi kumi kabla hajaona damu ya hedhi na hupotea masaa machache baada tu ya kupata hedhi na kujikuta hajambo kabisa na kushangaa siku zote alizokuwa anaumwa.

UCHUNGUZI
Ni vigumu kugundua tatizo hili moja kwa moja kwani wengine hali hii inapotokea huambatana na dalili nyingine kama maumivu ya mwili mfano kiuno, mgongo, kichwa, miguu hata nyama za mwilini.
Pia wanawake wengine huhisi maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kufunga kupata haja kubwa, maumivu ya kifua, moyo kwenda mbio au kupatwa na ute mzito ukeni. Kwa hiyo unapoona tatizo hili linakuandama kila mwezi, basi ni vema umuone daktari wa magonjwa ya akina mama katika hospitali ya rufaa ya mkoa ili ufanyiwe uchunguzi wa kina.
Kwa kuwa ugonjwa huu unafanana sana na magonjwa mengine kufuatana na dalili zake, pia dalili zake zinachukua muda mrefu au siku saba hadi kumi, basi unaweza kujikuta mara kwa mara unatibiwa tatizo ambalo siyo, mfano unaweza kusikia mwanamke akilalamika kila mwezi anatibiwa malaria au kila mwezi anatibiwa yutiai au mwingine taifoidi, basi ilimradi kila mwezi unatibiwa ugonjwa huohuo usioisha.
Ugonjwa huu huchunguzwa kwa umakini kuzingatia historia ya tatizo na vipimo kuangalia kiwango cha vichocheo au homoni hizo mbili za Progesterone na Estrogen ambazo tumezitaja hapo awali. Pia kiwango cha madini ya Sodium kitahakikiwa kwenye damu ili kujiridhisha na tatizo. Baada ya hapo daktari atakushauri nini cha kufanya pamoja na matibabu ya ugonjwa wako.

MATIBABU NA USHAURI
Inashauriwa unapokuwa na tatizo hili hakikisha unakuwa mtulivu, jiweke kwenye hali ya usafi, hakuna ugonjwa ambao hauponi au haupati nafuu. Maana kama hauponi na imethibitishwa na madaktari, basi kuna njia ya mgonjwa kupatiwa nafuu.
Ugonjwa huu huwa unapona wenyewe pale mwanamke anapopata tu damu ya hedhi na huanza tena siku saba hadi kumi kabla ya tarehe ya kuona damu ya hedhi. Matibabu mengine yatatolewa kadiri daktari atakavyoona inafaa.