TTCL

EQUITY

Tuesday, February 7, 2017

ZITTO KABWE, WABUNGE WA UKAWA NA WABUNGE WA CCM WAINGILIA SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA

Sakata la dawa za kulevya jana lilitikisa Bunge mjini hapa baada ya wabunge kutaka orodha ya ‘wauza unga’ ambayo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema anayo ili ifanyiwe kazi na mrithi wake, John Magufuli.
Akichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Ukimwi na ile ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema Rais Kikwete aliwahi kuutangazia umma kuwa anayo orodha ya vigogo wa dawa za kulevya hivyo alitaka wakamatwe ili watumiaji waachiwe.
“Kikwete alisema anayo orodha ya wauza dawa za kulevya. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mwigulu Nchemba) amfuate kule Msoga ili ampe hiyo orodha. Naamini watumiaji wataachiwa,” alisema.
“Vita ya dawa za kulevya siyo ya Paul Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam), hii ni vita ya Serikali na naamini itamuunga mkono. Mtu akipimwa akionekana ni mtumiaji atusaidie kumpata muuzaji,” alisema.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alimtaka Rais Magufuli kuacha kuendesha nchi kwa sanaa na kutafuta habari zake zipewe uzito katika vyombo vya habari, badala ya kushughulika na tatizo.
Mbunge huyo alisema kwa mwaka 2016/2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini ambayo ndiyo yenye dhamana ya vita hiyo haikupata fedha za maendeleo. “Leo bajeti ya tume ni sifuri halafu anasimama mkuu wa nchi anasema vita ipiganwe. Tuache kutafuta vichwa vya habari kwenye vyombo habari,” alisema Mdee.
Aliongeza, “Vita hii inahitaji utashi wa kisiasa. Kikwete alisema anawajua wauza unga kwamba ana orodha. Alipoondoka Ikulu si aliacha mafaili? Orodha unayo hapo Ikulu tusicheze na akili za Watanzania,” alisema.
 
Image may contain: 1 person
 Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) amesema Serikali imeshindwa vita dhidi ya madawa ya kulevya kwa kutokiwezesha chombo kilichoundwa na sheria ili kupambana nayo.“Kamati ya (Bunge) imelalamika kuwa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya ina bajeti finyu na hata hiyo bajeti haitolewi na hivyo kusababisha Mamlaka kukosa vitendea kazi, kushindwa kutoa elimu kwa umma, kushindwa kufanya operesheni za ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kushindwa kutoa ushauri nasaha kwa waathirika,”alisema Zitto.Zitto alikuwa akizungumzia taarifa ya Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi imebaini dosari nyingi katika sera ya dawa za kulevya ya mwaka 2004 ambayo imepitwa na wakati.Wakichangia katika taarifa ya shughuli za kamati kwa mwaka 2016/17, wabunge, akiwemo Zitto, walisema dawa za kulevya ni janga la taifa na linahitaji mikakati ya kupambana na siyo kuwaweka rumande waathirika ambao wanahitaji kupatiwa matibabu.Zitto alibainisha kuwa watuhumiwa waliokamatwa katika vita inayoendelea jijini Dar es Salaam wamelazwa ndani kwa zaidi ya siku tatu bila kufikishwa mahakamani.“Baadhi ya watuhumiwa wameelezwa kuteswa na kupigwa na polisi na kulazimishwa kutoa maelezo kwa Polisi," alisema Zitto."Umma haujaelezwa kama watu hawa wamekamatwa na madawa hayo ama wamehisiwa kuwa ni watumiaji tu.”