TTCL

EQUITY

Friday, May 27, 2016

Serikali yaandaa mpango kabambe wa mipango miji (Master plans)




Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaandaa Mpango Kabambe wa Mipango Miji (Master Plan) utakaoainisha matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro ya ardhi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa  Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mhe. Angelina Mabula  wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mpango wa Serikali kumaliza migogoro ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Mabula alieleza kuwa Wizara yake inashirikiana na  Halmashauri za Wilaya na Miji 18 kwenye program ya Urban Local Government Supporting Programme (ULGSP) katika kuandaa Mipango Miji hiyo.
Pia Mhe. Mabula alibainisha kuwa Wizara inaandaa na kukamilisha programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi Tanzania itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia 2015 hadi 2025.
“Serikali imekuwa ikiziagiza Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji kwa kuwa inatambua umuhimu wa kupima viwanja na mashamba ili kuwa na matumizi bora ya ardhi yetu” alisema Mabula.
 
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Mhe. Angelina Mabula

Aidha, Mabula aliongeza kuwa Serikali kupitia Mradi wa Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kununua vifaa vya upimaji ambavyo vitasambazwa katika kanda 8 za Wizara ya Ardhi ili Halmashauri zote zilizopo ndani ya kanda hizo ziweze kunufaika.
Alieleza kuwa makadirio ya awali ya gharama za mradi huo ni Dola za Kimarekani Milioni 4 ambapo Dola Milioni 2 zitatumika kwenye upimaji na Dola Milioni 2 zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa.
Katika kupunguza na kutatua migogoro ya ardhi iliyopo sasa, Mabula alisema kuwa Wizara ya Ardhi imeandaa kitabu cha orodha ya migogoro nchi nzima kinachoainisha vyanzo vya migogoro hiyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Hali kadhalika, Mabula alisema kuwa Wizara imesambaza Sera na Sheria za Ardhi hasa kwenye maeneo yenye migogoro, wameimairisha mfumo wa kielektroniki  katika kutunza kumbukumbu, na kuboresha ofisi za Kanda ili kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.

No comments:

Post a Comment