Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. John Kijazi ameutaka uongozi wa hospitali ya Mwananyamala kuhakikisha kuwa dawati la malalamiko kwa wagonjwa linafanya kazi masaa 24 ili  kuboresha huduma katika hospitali hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kupokea msaada wa magodoro Dkt. Kijazi amesema kuwa wagonjwa wanatakiwa kuhudumiwa kwa wakati na kusikilizwa malalamiko yao muda wote wanapopatwa na changamoto hospitalini hapo ili kuweza kuboresha huduma kwa watanzania.
“Nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walipata matatizo usiku wa kuamkia leo na hakukuwa na mtu wa kuwasikiliza kwa  wakati na kushindwa kupata huduma bora walipokuwa na shida hivyo naagiza uongozi kuhakikisha dawati la malalamiko kufanya kazi masaa 24 ili kuondoa kero za Wagonjwa wote”.alisema Dkt Kijazi.
Aidha Dkt. Kijazi ameushukuru uongozi wa Umoja wa Makanisa ya Pentekoste kwa kutoa msaada wa magodoro 50 yenye thamani ya shilingi milioni 1.631 ili kuendeleza huduma bora kwa wagonjwa wa Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es salaam.

Ally Hapi
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Ally Hapi wa kwanza kushoto akimsikiliza mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali ya Mwananyamala  akitoa kero zake kuhusu hospitali hiyo wakati wa hafla fupi ya kupokea msaada wa magodoro 50 kutoka kwa Umoja wa Makanisa ya pentekoste  iliyofanyika katika hospitalini hapo.
Akipokea msaada huo Dkt. Kijazi  alisema kuwa anawaomba viongozi wa Umoja huo na taasisi zingineziendelee na moyo wa  kuchangia kwenye shughuli za kijamii kadriwanavyoweza ili kuifikisha Tanzania salama katika kilele cha mafanikio.
“Nawaomba Umoja wenu, taasisi na wadhamini mbalimbali kuweza kusaidia kuinua na kukuza huduma bora za kijamii ikiwemo mahospitalini ili kusaidia serikali kupiga hatua katika kupambana na changamoto ya vifaa zinazoikabili hospitali ya Mwananyamala” aliongeza Dkt. Kijazi.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bw. Ally Hapi amesema kuwa ana Imani na Serikali ya awamu ya tano katika kutatua kero za wananchi hususani katika Wilaya yake kwani ameshaona mfano wa kupokea msaada huo na kuungwa mkono na Katibu Mkuu Dkt. John Kijazi kwa kushirikiana vizuri kwenye shughuli hiyo.
“Nafurahi kukutana na kushirikiana  kwa pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi katika shughuli za kijamii hususani katika hili la kuendeleza huduma bora zitolewazo na hospitali ya Mwananyamala ili kuifikisha mbali Tanzania mpya” alisema Bw. Hapi.