MAPAMBANO dhidi ya vita vya ubadhirifu wa fedha pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma katika Halmashauri za wilaya,Miji,Manispaa pamoja na Majiji huenda yakageuka kuwa shubiri kwa baadhi ya watendaji wake wasiokuwa waaminifu,waadilifu na wenye ulafi uliotawaliwa na ubinafsi.
Katika hali ambayo inaonekana maamuzi magumu endapo yatasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria yanawezekana,yamedhihirika katika Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara. 
Dhamira ya dhati ya maamuzi ya Halmashauri ya wilaya ya Hanang,yalilazimika kutolewa na Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kushindwa kuvumilia vitendo vya ubadhirifu wa fedha za wananchi uliokuwa ukifanywa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo,Felix Mabula. 
Kutokana na kutoridhishwa na ulafi huo wa kiongozi mkuu wa Halmashauri hiyo ndipo madiwani wa Halmashauri hiyo katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,lilipofikia hatua ya kutoa maamuzi magumu ya kuwasimamisha kazi watumishi wanne wa Halmashauri hiyo,akiwemo Mweka hazina wa Halmashauri hiyo kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara. 
Aidha katika maamuzi yake Baraza hilo pia limeazimia kwa kauli moja kwamba halina imani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Felix Mabula kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wa shilingi 82,873,000/= na hivyo kupendekeza kwenye mamlaka zinazohusika kumsimamisha kazi Mkurugenzi huyo kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazomkabili. 
Akifunga mkutano wa Baraza hilo maalumu,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,George Bajuta amewataja watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni pamoja na Mweka hazina wa Halmashauri,Mazengo Matonya,Mhasibu msaidizi,Marseli Siima,mhasibu wa matumizi,Wellu Sambalu na afisa mipango wa Halmashauri hiyo,Hamisi Khatimba. 
Aidha Bajuta anasema kwamba kwa mujibu wa kanuni,sheria na taratibu za mikutano ya Halmashauri,Mkurugenzi mtendaji ndiye katibu wa vikao hivyo na kwa kuwa pamoja na kuwa na taarifa ya mkutano huo hakuweza kuonekana katika ukumbi huo,wajumbe wa mkutano huo walilazimika kumchagua,afisa kilimo wa wilaya,Paul Lukumai kuwa katibu wao.

DSCN0013 
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara waliohudhuria mkutano maalumu wa Baraza la madiwani na kutokuwa tayari kuendelea kufanyakazi na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Felix Mabula

 “Kwa mujibu wa neno katibu kwa maana ya mikutano ya Halmashauri na kamati zake ni Mkurugenzi au afisa aliyeteuliwa kufanya shughuli za Mkurugenzi,sisi kama baraza tuna mamlaka ya kufanya hivyo na kwa sababu niliwashirikisha wajumbe na mkapendekeza watu wawili,na baadaye tumeamua kumpendekeza mmoja,kwa kanuni hii tunamtaka ndugu Lukumai aje akae kwenye kiti cha katibu”alisisitiza Bajuta huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo maalumu. 
Akitoa utetezi wake baada ya kuchaguliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya,afisa kilimo wa wilaya hiyo,Paul Lukumai ametaka kufahamu uteuzi wake ni wa maandishi au wa maneno tu,kwani anachofahamu yeye wajumbe hao wamemchagua yeye kukaimu na siyo kumteua,au kama mwanasheria ataeleza vinginevyo. 
“Siyo ubishi mwenyekiti ni hivii ni uelewa tu mwenyekiti nilikuwa naomba,ingawaje kanuni iliyosomwa na mwanasheria ni mkurugenzi au afisa aliyeteuliwa na uteuzi inaweza ikawa ya maandishi au ya namna gani kwa sababu uteuzi,labda hapa ni kumchagua mtu atakayesimamia mkutano huu,lakini kama ni uteuzi kwa maana ya maandishi,labda ifafanuliwe kidogo”alisisitiza Lukumai
 Hata hivyo mkutano huo maalumu nusura uingie dosari baada ya mkuu wa wilaya ya Hanang,Thobiasi Mwilapwa kuingia ukumbini na kutaka kumtetea Mkurugenzi mtendaji huyo, huku akiwatishia wajumbe wa mkutano huo kwamba mkutano haukuwa halali.
 “Naomba tuelewane vizuri nikiwa nimevaa ile sura ya kwanza ya kama kiongozi mwenzenu wakati nikiwa na ujumbe wa serikali nilitaka niufikishe ujumbe huo kwa njia ya diplomasia,nikatuma ujumbe kwa mwenyekiti kwamba mwenyekiti na makamu waje tuonane mahali ili tuzungumze ikiwezekana wao waje watoe ule ujumbe na mimi nikae kama mjumbe mwenzenu”alifafanua mkuu wa wilaya. 

DSCffN0020Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara,Bwana George Bajuta(wa kwanza kutoka kushoto) akiwa kweneye mkutano maalumu wa kumkataa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Bwana Felix Mabula.(Picha Na Jumbe Ismailly).

Anasema kwamba kutokana na sababu au mazingira yalivyo au nafasi ilivyo haikuwezekana kukutana na viongozi hao na ndipo alipofikia uamuzi wa kwenda kusimama mwenyewe kutoa ujumbe wa serikali akiwa mkuu wa wilaya kwamba mkutano huo siya halali. 
Kikao hicho kilichotakiwa kuanza majira ya saa nne asubuhi kililazimika kuanza majira ya saa sita mchana kutoka na wajumbe wa mkutano huo kumsubiri katibu wa kisheria wa mkutano huo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji kwa saa mbili bila mafanikio,zaidi ya kumtumia Mkuu wa wilaya,Thobiasi Mwilapwa ambaye hata hivyo alijikuta akitolewa nje ya ukumbi huo. 
Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Jaccob Mugeta anasema Halmashauri hiyo imetumia jumla ya shilingi 82,873,000/=kugharamia huduma mbalimbali zinazodhaniwa kutotolewa kabisa katika Halmashauri hiyo wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015. 

DSCN0003 
Jengo la ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara

Akisoma taarifa ya ukaguzi wa ndani kwa robo ya pili kwa mwaka 2015/2016,kwenye mkutano maalumu wa Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Hanang,Mugeta anafafanua kuwa baada ya kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika katika matumizi ya fedha za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wameweza kubaini kuwa Halmashauri hiyo haikupatiwa huduma walizodai kuhudumiwa na watoa huduma mbalimbali waliopo katika mji wa Hanang na nje ya wilaya hiyo.
 “Kwa kutumia fomu maalumu zilizoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi nchini(PPRA) tulibaini manunuzi yenye thamani ya shilingi 82,873,000/= kuwa yalilipwa kwa huduma ambazo hazikupokelewa na Halmashauri”alifafanua Mkaguzi huyo wa ndani. 
Mkaguzi huyo wa ndani anasema kwamba manunuzi hayo yalichukuliwa kama malipo ambayo hayakuwa na tija kwa Halmashauri kwa kuwa yalikosa ushahidi juu ya kufanyika kwake na hivyo hapakuwepo na thamani ya fedha iliyopatikana kwa upande wa Halmashauri. 
Anasema Mugeta kwamba kati ya kiasi hicho cha shilingi 82,873,000/=kilichodaiwa kutumika kwa matumizi mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu,Halmashauri ilikodisha ukumbi wa mikutano wa SUMMIT HOTEL na kutakiwa kulipa 12,600,000/= kwa muda wa siku tatu. 
Matumizi mengine yaliyolipwa kwa mmiliki wa SUMMIT HOTEL kwa mujibu wa mkaguzi huyo ni chakula na viburudisho 9,780,000/=,huduma za kudurufu nyaraka 2,970,000/= pamoja na ukodishwaji magari kutoka Dar-es-Salaam kwa ajili ya matangazo muhimu ya uchaguzi mkuu 7,920,000/=. 
Anaweka wazi Mugeta taarifa hiyo kwamba ukodishaji wa magari kwa ajili ya ubebaji wa vifaa wakati wa uchaguzi mkuu kutoka Dar-es-Salaam 26,400,000/=,ulipaji wa madeni, waendeshaji wa mitambo (BVR Operators) na wasaidizi wa vituo 14,105,000/= 
“Malipo kwa wasimamizi wasaidizi 66 ngazi ya kata kwa ajili ya ujumlishaji wa kura kwa muda wa siku kumi kwa shilingi 16,500,000/=shughuli mbali mbali za uchaguzi ambazo hazina maelezo zilitumia 1,742,000/=,uendeshaji wa ofisi ya Afisa uchaguzi na ulinzi kwa siku 14 zilitumika 2,800,000/= na shilingi 300,000/= ni malipo ya posho kwa waapishwaji, msimamizi wa uchaguzi,Afisa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo”alisisitiza Mkaguzi huyo wa ndani. 
Mkaguzi huyo hata hivyo hakusita kuweka bayana kuwa hundi ya malipo ya shilingi 113,302,000/= iliandikwa na kulipwa kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo na kwamba shilingi 82,,873,000/= ndizo ambazo zinahojiwa matumizi yake.
Mugeta hata hivyo hakusita kuyataja mapungufu mengine
waliyobaini wakati wa ukaguzi huo kuwa ni kuwepo matumizi ya 223,342,000/= yaliyotumika bila kupitishwa na Afisa uchaguzi,malipo ambayo hayakufanyiwa ukaguzi wa awali 83,512,000/=,ziada ya vituo vya kupigia kura 7,210,000/= na malipo yenye nyaraka pungufu 6,192,000/=. 
Kwa upande wao baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo wakizungumzia sakata hilo la ubadhirifu wa fedha uliofanywa na Mkurugenzi mtendaji huyo,wanasema kuwa mkaguzi wa ndani ndilo jicho la Halmashauri hiyo na kwa maana hiyo kama shilingi milioni 223 hazina idhini ya mkuu wa idara,tayari hiyo ni mashaka. 
Naye diwani wa kata ya Gendabi,Stephen Sulle pamoja na kuishukuru kamati ya fedha,lakini anasema msururu wa upotevu wa fedha hizo za Halmashauri ya Hanang unatajataja baadhi ya wataalamu ukimtoa Mkurugenzi,kipengere hicho siyo kizuri na kisiachwe hivi hivi. 
“Kuna watu wanaguswaguswa na taarifa ya Mkaguzi wa ndani naomba na hao tuwaweke mahali,lakini mkuu wa wilaya anajua wazi tumeshaibiwa fedha lakini yeye bado anaonekana kuwabebabeba watumishi hao huku akionyesha kutokitambua kikao chetu cha leo,je huyo ni dc kweli?alihoji huku akishangiliwa na wajumbe.