TTCL

EQUITY

Monday, May 2, 2016

UKAWA waingiza kanuni zao bungeni

Na Bakari Kimwanga, Dodoma
KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mara ya kwanza wametoa kanuni zao ambazo zitatumika kama mwongozo kwa wabunge wanaotokana na vyama hivyo.
Kanuni hizo ambazo zimeridhiwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kwa wapinzani kuwa na kanuni zao.
Akizungumza na mwandishi wetu Aprili 30 Jumamosi Mkurugenzi wa Bunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema, alisema mchakato wa kupata kanuni hizo ulipitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha wabunge wa kambi ya upinzani ambao walizisoma na kusaini.
Kitabu cha Kanuni hizo chenye kurasa 24, kilitolewa jana na kusainiwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kugawiwa kwa kila mbunge wa upinzani hasa wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Tumeamua kuwa na kanuni za kuelimisha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na awali tulifanya utafiti kwa nchi zote za Afrika hakuna kambi ya upinzani yenye kanuni ila kwa Tanzania ni ya kwanza.
“Ni matumaini yetu nchi hizo zitakuja Tanzania kujifunza namna tulivyotunga kanuni hizi, ambapo zimepitia hatua mbalimbali ikiwemo kushirikisha vyama husika na unajua Kambi inaundwa na wabunge wa vyama vinavyounda Ukawa.
“Imesomwa na kila mbunge na wote wameridhia na kuisaini kila mmoja na baadae Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliridhia kuanza matumizi yake, ninawapongeza wabunge wote wa upinzani kwa kuzikubali kanuni hizi ambazo ndizo zitakuwa mwongozo wao,” alisema Mrema
Mkurugenzi huyo wa Masuala ya Bunge wa Chadema, alisema anaamini wabunge wote wa upinzani watazifuata kanuni hizo na kuwaongoza katika majukumu yao ya kazi za kibunge.