TTCL

EQUITY

Thursday, February 18, 2016

SAU: Serikali ya kitaifa si ya CCM na CUF.

 Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Sauti ya Umma (SAU), Issa Mohammed Zonga.
 
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Sauti ya Umma (SAU), Issa Mohammed Zonga, amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, haijaundwa kuongozwa na CCM na CUF pekee.
Akizungumza na Nipashe mjini haopa jana, Zonga alisema hata kama  CUF haitashiriki uchaguzi wa marudio, hicho si kigezo au sababu ya kuvunjika kwa serikali hiyo. 
“Nchi hii si ya CCM wala CUF. Wananchi ndio wenye uamuzi wa kutaka kuendelea na serikali ya umoja wa kitaifa au vinginevyo,” alisema.
Alisema kila chama kilichoamua kuingia katika uchaguzi, lengo na dhamira ni kushinda na si kusindikiza CCM na CUF kama ilivyojengeka dhana kwa baadhi ya wanasiasa.
Zonga alisema vyama vyote vya siasa vimeibuka baada ya mfumo wa vyama vingi kwa kuwa  kabla ya hapo, ilikuwapo CCM tu, nayo ilisajiliwa upya baada ya kuanzishwa kwa vyama vingi. 
“Nawashangaa sana wanaodharau vyama vingine. Ukiacha CCM na CUF hapa Zanzibar kwani sisi hatuwezi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa endapo wananchi wataamua?” alihoji Zonga.
Hata hivyo, alisema chama chake kinashiriki katika uchaguzi wa marudio  unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu na kimeshaidhibitishia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) juu ya ushiriki wao.
Naye mgombea urais wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Said Soud, ameiomba ZEC  kuharakisha kuwapatia ulinzi wagombea urais wa Zanzibar wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi wa marudio.
Soud ambae pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,  alisema ni wajibu wa  ZEC kufanya hivyo ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza ikiwamo mgombea yeyote kupata madhara. 
Wagombea hao waliwashauri wananchi wote waliojandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura, kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao hiyo ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.

No comments:

Post a Comment