TTCL

EQUITY

Thursday, February 18, 2016

Malalamiko ya huduma ya utoaji haki kufanyiwa kazi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe.
 
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe (pichani), amesema serikali itayafanyia kazi malalamiko yote ya wananchi yanayojitokeza kwenye huduma ya utoaji haki, yakiwamo ya upepelezi wa kesi unaochukua muda mrefu na ucheleweshaji wa nakala za hukumu usio na tija.
Dk. Mwakyembe aliyasema hayo wakati akijibu malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza wakati wa mikutano yake ya kampeni katika ziara yake ya kutembelea wananchi kusikiliza kero zao wilayani Kyela.
Alisema mambo mengine ambayo yatafanyiwa kazi na wizara yake ni tatizo la na ubambikizwaji wa makosa kwa wananchi wasio na hatia.
Dk. Mwakyembe alisema wizara yake na ya Mambo ya Ndani ya Nchi, zimedhamiria kwa pamoja kumaliza changamoto hizo ndani ya muda mfupi ujao ili haki itendeke na wananchi kujenga imani kubwa na vyombo vinavyotoa haki.
Mapema akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mji mdogo wa Ipinda, Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kyela, Dk. Hunter Mwakifuna, aliitaka serikali ikomeshe vitendo vya rushwa, ucheleweshaji kesi na kuwabambikizia kesi watu wasio na hatia, upungufu ambao waziri alithibitisha kuwapo.
"Tumetumia muda mrefu kuisoma hali halisi kwenye vyombo vyote vya utoaji haki. Upungufu huo upo na dawa yake iko jikoni inatokota," alisema.
Alieleza changamoto nyingine kubwa katika utoaji haki nchini ni uhaba mkubwa wa mahakama za mwanzo ambao tayari Serikali inaufanyia kazi.
 "Uamuzi wa Mheshimiwa Rais hivi majuzi kuipatia Mahakama fedha zake zote za maendeleo kwa mwaka huu wa fedha, yaani Sh. bilioni 12.3, ulilenga kuiwezesha mahakama kujenga mahakama za mwanzo zaidi mwaka huu ili kupunguza adha iliyokuwapo," alisema.

No comments:

Post a Comment