TTCL

EQUITY

Thursday, February 18, 2016

Magufuli: kazi zote za wasanii zilizo feki zikamatwe, liwe ni zoezi la kuwatafuta wezi wa kazi zao

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na makundi mbalimbali yaliyoshiriki katika kampeni za uchaguzi mkuu 2015 wakiwemo wasanii.
Rais Magufuli akiambatana na makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Hassani, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi Abdalah Bulembo pamoja na mawaziri kadhaa wa serikali yake amekutana na makundi hayo ikulu jijini Dar es salaam kwa nia ya kuwashukuru na kutoa agizo la katazo la utoaji wa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi.
Aidha Dkt Magufuli ameiagiza mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kufanya operesheni maalum ya kukamata kazi zote za wasanii zisizo na alama maalum ya mamlaka ya mapato nchini kufuatia malalamiko ya wasanii kushindwa kumudu ushindani katika soko kutokana na kazi nyingi kuingizwa nchini bila ya kulipia ushuru.
Pia amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa Na Michezo Mh. Nape Nnauye kuangalia utaratibu wa chama cha haki miliki Tanzania (COSOTA) kuwa chini ya wizara yake tofauti na ilivyo sasa ambapo chama hicho kiko chini ya wizara ya viwanda na biashara.
Kwa upande wake makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu hassani amewashukuru wasanii hao kwa mchango wao uliokiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuwataka kuendelea kushirikiana na serikali katika masuala mbalimbali ya kuhamasisha maendeleo huku waziri mkuu Mh Kassim Majaliwa akiwaahidi kusimamia kwa vitendo maagizo yote yaliyotolewa na Rais.
Kwa upande wasanii hao wamemshukuru Rais kwa uamuzi wake wa kuwaita na kuzungumza nao ikiwa ni jitihada za kutambua mchango wao katika uchumi na maendeleo ya nchi na miongoni mwa makundi yaliyofanikisha chama cha mapinduzi kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2015..

No comments:

Post a Comment