TTCL

EQUITY

Friday, January 1, 2016

Rais Dkt. Shein atoa salam za Mwaka Mpya

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa risala ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 kwa wananchi na kueleza kuwa takwimu za mwanzo wa mwaka 2015, uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika.
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
 
Katika risala yake hiyo kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa huduma za jamii zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za afya pamoja na elimu nazo zimeimarika ikiwa ni pamoja na kupiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu.
Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa barabara muhimu umemalizika na kuzinduliwa Unguja na Pemba pamoja na kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, pamoja na Kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho tayari kimeshatiwa taa za kurukia ndege.
Alisema kuwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa viwanja hivyo tayari imepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya ndege za Kimataifa zinazokuja Zanzibar, jambo ambalo limepelekea kuimariska kwa sekta ya Utalii na shughuli za biashara.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefanikiwa kutengenezesha meli mpya yenye mitambo ya kisasa katika Kampuni ya ‘Daewoo International’ ya Jamhuri ya Korea, ambayo ina utaalamu na uzoefu mkubwa wa kutengeneza meli.
“Nasaha zangu kwenu nyote wananchi ni kuwa tuithamini na kuienzi meli yetu hiyo... tukumbuke msemo wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kuwa ‘kithamini chako mpaka usahau cha mwenzako”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein katika risala hiyo alieleza kuwa katika mwaka 2015 Serikali imefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha dhamira ya kujenga bandari ya Mpiga Duri inaanza kutekelezwa, ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka 2016.
Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kusambaza umeme vijijini Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kuufikisha umeme huko Kisiwa Panza na Kisiwa cha Makoongwe kwa upande wa Pemba, kwa kuwatumia wataalamu wazalendo.
Kwa upande wa huduma za afya Dk. Shein alisema kuwa katika mwka 2015 huduma hizo zimeimarishwa kwa kuongeza kasi ya kusomesha wataalamu, upatikanaji dawa na huduma mbali mbali pamoja na kuziimarisha hospitali kwa kutekeleza miradi ya ujenzi.
Akieleza kuhusu kuimariaka kwa sekta ya elimu mnamo mwaka 2015, Dk. Shein alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuanza na kumalizika kwa miradi ya ujenzi wa skuli, kuongeza fani za mafunzo katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu sambamba na kutekeleza lengo la kuondoa gharama za kuchangia elimu mashuleni.
“Lengo letu ni kuifanya elimu ya msingi kuwa bure huku tukiandaa utaratibu ili elimu ya sekondari nayo iwe bure kama ilivyodhamiriwa na Muasisi wa Mapinduzi yetu ya mwaka 1964”,alisema Dk. Shein.
Alieleza kuimarika kwa miradi ya ujenzi wa miji na majengo ya kisasa katika sehemu mbali mbali ili kuweza kuijenga taswira mpya ya Zanzibar katika kipindi kifupi kijacho. Aidha, alieleza kukamilika kwa viwanja vya kufurahishia watoto hapa nchini.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kuwa walinzi wa miundombinu iliyopo na wasichelee kuwafichua wale wote wanayoiharibu na kueleza kusikitishwa kwake katika mwaka uliomalizika baadhi ya watu waliiharibu miundombinu hiyo kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na kusahau maslahi ya wote.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa huduma za matrekta na pembejeo za kilimo kwa wakulima ambao kwa msimu wa mwaka 2015/2016 tani 750 za mbolea na lita 15,000 za dawa ya kuulia magugu zimekwishanunuliwa.
Kwa upande wa zao la Karafuu Dk. Shein alisema kuwa wakulima wameitikia vyema wito wa Serikali wa kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC, ambapo katika msimu wa ununuzi wa karafuu wa mwaka 2015/2016, hadi kufikia mwezi Novemba, 2015 jumla ya tani 962.7 za karafuu zenye thamani ya Tshs. Bilioni 13.471 zimenunuliwa katika vituo vya ununuzi wa karafuu vya SSTC Unguja na Pemba.
Akieleza kuhusu uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25, Oktoba mwaka 2015 ambapo wananchi wa Zanzibar walishiriki katika kuwachagua viongozi wao, ambapo kwa upande wa uchaguzi wa viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliosimamiwa na Tume ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umemaliza na CCM kupata ushindi, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Tume ya uchaguzi uliufuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba, 2015 baada ya kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa kama zilizvyoelezwa na Tume hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa katika suala zima la hali ya kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu, viongozi walishauriana kukutana ili kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia ya amani, ili nchi iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano na hatimae wakakubaliana kuanza mazunguzmo hayo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Shein katika risala hiyo, mazungumzo hayo yanayowahusisha viongozi sita yamefikia hatua kubwa na bado yanaendelea na kueleza kuwa taarifa kamili ya mazungumzo hayo itatolewa mara yatakapokamilika.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa tarehe 12 Jamuari 2016 Zanzibar itaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ambapo kama kawaida, sherehe hizo zitatanguliwa na matukio mbali mbali ya shughuli za uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika matukio mbali mbali yaliopangwa katika maadhimisho hayo ambapo pia, kushiriki kwao kwenye sherehe ya maadhimisho hayo ni hatua ya kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi kwa shabaha ile ile waliokuwa nayo waasisi wa Zanzibar.
Dk. Shein pia, alitoa wito kwa wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa kuimarisha usafi na kuzitaka Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji kwa Pemba na Halmashauri zote za Wilaya kuchukua hatua za uzoaji wa taka, na kuwataka wananchi wote kushiriki katika kuisafisha miji na maeneo wanayoishi hapo siku ya Januari 3 mwaka 2016.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi kuwa tarehe 1 Januari ni siku ya kujitokeza kufanya mazoezi hivyo wajitokeze kwa wingi kufanya mazoezi.

No comments:

Post a Comment