Rais Dk. John Magufuli.
Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi chini ya
uratibu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umemtaka Rais Dk. John
Magufuli, kuzingatia usawa katika uteuzi uliobaki ili kuleta mabadiliko
chanya katika serikali ya awamu ya tano.
Baadhi ya nafasi zilizosalia mpaka sasa ni uteuzi wa wabunge,
mabalozi, wakuu wa mikoa na wilaya, wakuu wa taasisi na mashirika ya
umma pamoja na wajumbe wa bodi.
Mkurugenzi Mtendaji TGNP, Lilian Liundi, aliyasema hayo wakati
akitoa maoni yake kuhusu uteuzi uliofanywa na Rais Magufuli kwamba
haukuzingatia usawa wa jinsia kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/20.
Liundi alisema serikali ya awamu ya tano hajaonyesha mwanzo namna
ya kutekeleza Ilani ya chama tawala kama inayoelekeza kwa kumuwezesha
mwanamke kushika nafasi sawa na mwanaume kwa maana ya asilimia 50/50
katika uongozi kwenye vyombo vya maamuzi ngazi zote.
“Tunasisitiza kuheshimiwa na kutekelezwa kwa vitendo kwa malengo
hayo ili wanawake wapate fursa sawa za kutoa maamuzi juu ya masuala
muhimu ya taifa letu, tunaitaka serikali kutekeleza ahadi zake za
kuzingatia usawa wa kijinsia kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM,”
alisema Liundi.
Aidha, alimtaka Rais Dk. Magufuli na viongozi wenzake, kusimamia
kikamilifu utekelezwaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa na Tanzania
hususan ile inayohusu usawa wa kijinsia ili kupunguza pengo lililopo.
Liundi aliitaja mikataba hiyo kuwa ni pamoja na Mpango Kazi wa
Beijing wa mwaka 1995, Mkataba wa Maputo, Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia
na Maendeleo Kusini mwa Afrika na tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za
Binadamu (1948).
No comments:
Post a Comment