TTCL

EQUITY

Wednesday, December 23, 2015

Hofu akaunti zao kushikiliwa, vigogo walalia noti

Dr-Philip-Mpango1 Kaimu Kamishna wa TRA, Philip Mpango.

MATUMBO joto! Kufuatia agizo la serikali kuwataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwasilisha tamko la mali wanazomiliki ili kubaini kama utajiri walionao unaendana na vipato vyao, imebainika kuwa vigogo mbalimbali wa mamlaka hiyo wanahaha kuhakikisha wanazitoa fedha zao benki na kuzihamishia majumbani kabla hazijashikiliwa na serikali, Risasi Mchanganyiko limetonywa.

Agizo hilo lilitolewa hivi karibuni na Kaimu Kamishna wa TRA, Philip Mpango kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani, Stella Cosmas ikiwa ni siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kumsimamisha kazi Kamishina Mkuu wa TRA, Rished Bade kwa tuhuma za upotevu wa makontena zaidi ya 349 kupitishwa bandarini pasipo kulipia kodi.
Stella aliwataka watumishi wote wa TRA kuwasilisha fomu za tamko la mali na madeni yao kwa mwaka 2015 kabla ya Desemba 15 ambapo vyanzo vinaelewa kuwa mara baada ya agizo hilo kutolewa, vigogo mbalimbali ambao wana ukwasi mkubwa walianza kuzitoa fedha walizokuwa wamejilimbikizia katika akaunti zao.

TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo ambacho kipo ndani ya benki moja maarufu Bongo kilieleza kuwa, vigogo hao wanafanya miamala mikubwa siku baada ya siku ili kufanikisha zoezi la kukwepa fedha zao kushikiliwa na kuhojiwa wamezipataje.
“Kuna miamala mikubwa inafanyika fastafasta kwa kushirikiana na wafanyakazi wa benki, bila shaka ni hawa vigogo wa TRA maana kasi imeongezeka zaidi mara baada ya ule waraka wa Mkurugenzi wa Mambo ya Ndani wa TRA (Stella) kuwataka watoe orodha ya mali wanazomiliki kutangazwa.

WAZIBADILI KUWA DOLA
“Hawatoi katika mfumo wa fedha za nyumbani. Wanazibadili juu kwa juu na kupewa zikiwa kama dola ili kupunguza mzigo usiwe mkubwa na waweze kuzibeba kirahisi na kutoshtukiwa na vyombo vya usalama,” kilisema chanzo hicho.

WAZICHIMBIA MAJUMBANI
Chanzo hicho makini kilizidi kudai kuwa, vigogo hao wanapozitoa fedha hizo zikiwa kama dola, wanalazimika kuzificha majumbani kwao kwa kuangalia sehemu ambayo anaamini si rahisi mtu kubaini kama anaweza kuweka fedha nyingi kiasi hicho.
“Wanaficha chini ya magodoro. Wengine nasikia wanaweka kwenye majaba yale ya kuwekea maji. Ukiingia nyumbani kwake unaweza ukafikiri amehifadhi maji kumbe yamejaa hela. Yani hata visado vile vya lita tano, wanavitumia maana hali ni mbaya.
“Magufuli amewakalia kooni hivyo hawana ujanja. Walijilimbikizia fedha nyingi katika akaunti tofauti sasa wanahaha zitakapokaguliwa hawawezi kuwa na maelezo ya kutosha, hawakuzipata kihalali,” kilisema chanzo.

WABADILISHA HATI ZA NYUMBA, VIWANJA
Kama hiyo haitoshi, imeelezwa kuwa, mbali na kutorosha fedha hizo katika akaunti zao, vigogo hao pia wanafanya michakato ya kubadilisha hati za nyumba zao kwa kuandika majina ya ndugu, jamaa na marafiki zao ili iwe vigumu kushtukiwa pindi watakapoanza kukaguliwa mali walizoorodhesha na mali halisi wanazomiliki.

INARUHUSIWA KUTOA FEDHA NYINGI KWA MKUPUO
Kwa mujibu wa taarifa za benki mbalimbali, mtu unapotaka kutoa fedha nyingi katika akaunti yako, lazima benki husika ihoji na kujiridhisha juu ya matumizi ya pesa hizo hivyo inadaiwa vigogo hao wanacheza dili na wafanyakazi wa benki ili kufanikisha matakwa ya kutorosha fedha nyingi kwa mkupuo.

POLISI WACHUNGUZA
Ili kutaka kujua kama jeshi la polisi lina taarifa juu ya vigogo hao wanaodaiwa kuficha fedha majumbani mwao, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Huwa hatupuuzi taarifa zozote tunazopata au kusikia na hii ni mojawapo ya ambazo tutazifanyia kazi haraka iwezekanavyo,” alisema na kuongeza;
“Hiyo unanipa kama tip, nitaifuatilia na polisi wakibaini watu hao, tutawakamata na nyinyi kama chombo cha tutawataarifu,” alisema Kova.

No comments:

Post a Comment