TTCL

EQUITY

Friday, December 4, 2015

Chemchemi ya maji ya moto yenye historia ndefu Katavi

Wananchi wakiwa na madumu tayari kwa kuchota maji kutoka kwenye chemchemi ya maji ya moto. Maji hayo hutumika kwa shughuli mbalimbali.
MKOA wa Katavi ni miongoni mwa maeneo ya Tanzania yaliyojaaliwa kuwa na utajiri mwingi wa maliasili ikiwemo wanyama pori, madini ya aina mbalimbali, ardhi yenye rutuba na misitu. Lakini mkoa huu pia una kitu kingine, chemchemi ya maji moto. chemchemi hii ya maji ya moto ni miongoni mwa vivutio vya utalii wa ndani na nje kwani ni maeneo machache duniani ambayo aghalabu huwa na kitu hiki kisicho cha kawaida.


Mkoani Katavi, kijiji inapopatikana chemchemi hii kimepewa jina la Majimoto na kipo katika Tarafa ya Mpimbwe wilayani Mlele. chemchemi hiyo inayobubujisha maji wakati wote ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa kijiji hicho cha Maji Moto na vitongoji vyake. Kwa mujibu wa simulizi za wanakijiji wa eneo hilo, chemchemi hiyo ilivumbuliwa na mbwa wa wawindaji, takribani karne moja iliyopita.

Kila siku mamia ya watu wakiwemo watoto, wanawake, wanaume na vijana hufika katika chemchemi hiyo wakiwa na vyombo vya kuteka maji kwa matumizi ya nyumbani. Pia wageni wanafika mahala hapo kwa lengo la kushuhudia ukweli tu wa uwepo wa chanzo hicho cha maji. Mzee maarufu wa jadi wa eneo hilo, Gerald Changwa Sibula (63) anasimulia kwamba chanzo hicho cha maji kiligunduliwa na mbwa wa wawindaji waliotoka anayoita ‘nchi ya Ufipa ya Juu’ ambayo sasa ni mkoa wa Rukwa.

Sibula ambaye ambaye anajitabulisha kwamba ana nasaba na Chifu aliyewahi kutawala eneo hilo anasema chemchemi hiyo iligunduliwa miaka 1000 pale mbwa wa wawindaji wawili alipowaongoza hadi eneo hilo na anamtaja mmoja wa wawindaji hao kuwa ni Lukesa aliyekuwa kafuatana na nduguye.

Anasema kwa kuwa nchi ya Ufipa haikujaliwa utajiri wa wanyama pori wawindaji maarufu wa eneo hilo akiwemo Lukesa na nduguye walilazimika kusafiri mwendo mrefu wakipita katika milima, mito na mapori hadi Maji ya Moto ambako enzi hizo ilijaaliwa kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori wa kila aina. “Lukesa na nduguye kama simulizi zinavyosema walifika eneo hili ili kuwinda wanyama pori lakini walihaha kwa siku tatu wakisaka maji ya kunywa na kupikia chakula bila kufanikiwa,” anasema Sibula.

“Ukosefu wa maji uliwalazimu ndugu hao wawili kushinda na njaa na kiu kwa siku tatu. Siku ya nne mchana wakiwa wamekata tamaa, ghafla wakawaona mbwa wao waliokuwa nao kwenye uwindaji wakirejea wakiwa wametapakaa matope mwili mzima huku wakipiga piga mikia yao kwa furaha. “Ndipo wawindaji hao wawili walipobaini kuwa mbwa wao wamegundua kilipo chanzo cha maji na ndipo wawindaji hao wakaanza kuwafatilia kwa karibu hadi mbwa hao wakawafikisha kwenye chanzo hicho cha maji ambapo walioga, wakanywa maji hayo na kuchota mengine kwa ajili ya kupikia chakula kambini kwao,” anasema.

Sibula anazidi kusimulia kwamba wawindaji hao wakiongozana na mbwa wao walirejea kambini wakiwa na maji ya kupikia chakula na kunywa na kwamba baada ya kusonga ugali kabla hawajaanza kula walijiuliza wawatuze zawadi gani mbwa wao. Inaelezwa kuwa kuanzia siku hiyo wawindaji hao waliwathamini mbwa wao kwa namna ya kipekee wakiwaona kuwa ni wakombozi wao wakati wa shida ambapo bila wao bila shaka wangekufa kwa kiu.

Anasema kila walipokuwa wakiandaa chakula, kwa kuthamini mchango wa mbwa wao walianza kuwapa wao chakula kwa kusema “Kwanza Ipimbwe Iliyee” yaani kwanza ale mbwa. Anasema msemo huo uliendelea kutumika na kurithiwa na kizazi kimoja hadi kingine na kusambaa sehemu mbalimbali hatimaye watu wa eneo hilo wakajulikana kama Wapimbe. Watu hao walijijengea utamaduni wa kumuenzi mbwa na kusababishwa eneo hilo kujulikana kama Mpimbwe hadi leo.

Kwa sasa kijiji hicho cha Majimoto ni miongoni mwa vijiji vilivyopo katika kata ya Mpimbwe. Maajabu mengine ya chemchemi hiyo ni kwamba kina chake cha maji hakiongezeki wala kupungua na pia joto la maji hayo halipungui wala kuongezeka. Ingawa kwa kawaida sehemu nyingine maji hupungua wakati wa kiangazi na kuongezeka wakati wa masika, katika chemichem hiyo hali ni tofauti.

Kina cha maji hakiongezeki wala kupungua hata kama watu watachota maji kwa wingi kiasi gani huku joto nalo likiwa haliathiriki kwa lolote. Wakazi wa kijiji cha Majimoto wanaeleza kuwa maji kutoka katika chemchemi hiyo ni ya moto na huchukua saa sita kupoa jambo linalosababisha wageni kupata shida wakati wa kuyanywa sababu ni ya moto na yana ladha ya chumvi.

“Kwa sisi wenyeji tunayatumia maji haya kwa matumizi mbalimbali yakiwemo kupikia, kunywa, kuoga na kufulia,” anasema Kiomboi Rasta, mkazi wa kijiji cha Majimoto. Anasema wakazi wa eneo hilo wamekunywa maji hayo tangu walipokuwa watoto lakini hadi sasa hawajasikia mtu yeyote kadhurika kutokana na kutumia maji hayo. Mariam Klaudio anasema yeye na familia yake wanaamini maji hayo kuwa na salama hivyo huyanywa bila kuchemsha.

“Ni maji meupe… Hayana kiluwiluwi cha mdudu yeyote yule na hivyo hatuna sababu ya kuyachemsha kwa sababu yameshachemshwa tayari na Mwenyezi Mungu… Sisi tumebahatika kupata maji ambayo tumechemshiwa tayari,” anasema Klaudio. Robert Salum Mashishanga ambaye ni mwanzilishi wa kijiji hicho anasema alifika eneo hilo mwaka 1991 likiwa pori tu alikitokea mkoa wa Shinyanga. Mwaka 1994 aliweka mashine ya kusaga ambayo ilikuwa ikitumia maji kutoka chanzo hicho cha maji.

Anasema chemchemi hiyo pia imekuwa chanzo cha kutunza utamaduni na mila za wakazi wa eneo hilo kwa kuwa hadi sasa wanazingatia miiko iliyowekwa na mababu zao. Sibula anaeleza kuwa miiko iliyokuwepo wakati huo ni kwamba hadi sasa mgeni akifika kijijini hapo kwa mara ya kwanza anakaribishwa kwa kugusisha kichwa chake juu ya jiwe lililopo karibu na chanzo hicho cha maji ndipo ataruhusiwa kunywa au kunawa maji hayo.

“Hata wewe mwandishi ni lazima ugonge kichwa chako kwenye jiwe hili ili upate kibali cha kuyatumia maji hayo na kupata maelezo ya kina kuhusu chemchemi hii… Huu ni utaratibu wa kawaida ili kudumisha mila na desturi za kuilinda chemichem hii,” anasema Sibula. Sibula anasema kuwa miaka ya nyuma eneo la chemchemi hiyo lilitumika kama kitovu cha mawasiliano. Anafafanua kwamba karibu na chemchemi hiyo kulikuwa na ngoma iliyokuwa na uwezo wa kujipiga yenyewe na kutoa mlio ulioashiria jambo fulani.

“Haijulikani ni nani aliyeiweka ngoma hiyo ila ilipojipiga watu wote walilazimika kuacha shughuli zao na kutimua mbio hadi kwenye makazi ya chifu ili kusikiliza taarifa mpya kutoka kwa chifu,” anasimulia Sibula. Anasema ngoma hiyo ilitolewa baada ya Serikali ya Tanzania kuvunja utawala wa machifu na kuweka mfumo mpya wa utawala. Chemchemi hiyo ina simulizi nyingi za kale zinazoelezea utamaduni wa Kiafrika na nguvu za miungu ya asili ambayo ilitumika kabla ya kuingia kwa dini ya Kiislamu na Kikristo.

Kwa mujibu wa wazee wa kimila wa eneo hilo, wakati Wamisionari wa Kanisa Katoliki walipofika eneo hilo walitaka kujenga kanisa kwa kuwa ilikuwa rahisi kupata maji. Hata hivyo, walipoanza kuweka miundombinu ya kutoa maji kwenye chemchemi hiyo hadi kwenye kiwanja walichokuwa wakifyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa kanisa maajabu yaliwatokea.

Anasema masimulizi yanaonesha kwamba chemchemi hiyo maarufu kama Nawinga kwa wakazi wa eneo hili ilihama kwa maana ya kukauka ghafla na kubakia mchanga tu kisha ikajitokeza kwenye eneo lililojulikana kama Korodea. “Kukauka kwa chanzo hicho cha maji kuliwalazimisha Wamisionari hao kuamua kuondoka na kujenga kanisa lao katika kijiji cha Mamba, umbali wa kilomita tano kutoka kijiji cha Majimoto.

Anasema, ili kulinda chanzo hicho cha maji, serikali imejenga uzio wa maji ili wananchi waweze kuyachota bila kutumbukiza vyombo au taka kwenye uzio huo. Pia serikali imepiga marufuku ujenzi wa miundombinu kwenye chemichem hiyo kwa lengo la kusambaza maji kijijini kwa sababu usambazaji wa maji kwa kutumia mabomba unaweza kusababisha chemchemi hiyo kukauka.

Chimichem hiyo inalindwa na wakazi wa eneo hilo kwa kutumia miiko na desturi za kale zinazokataza watu kuchafua maji hayo wala kuruhusu wageni kufika eneo hilo bila ruhusa ya wenyeji. Baada ya kizuizi hicho maji hayo yanaendelea kutiririka hadi eneo la makaburi yanapozikwa watemi na wakati wote maji hayo yanatakiwa kutiririsha maji yake juu ya makaburi hayo vinginevyo wanaamini maji yasipofurika juu ya makaburi hayo kutasababisha ukame na njaa.

Mwandishi wa makala haya alishuhudia mti wa mbuyu ukiwa umeota juu ya chanzo hicho cha maji ambapo simulizi zinaeleza kuwa umekuwepo hapo karne kadhaa lakini haukui kama miti mingine ya mibuyu.

No comments:

Post a Comment