TTCL

EQUITY

Thursday, November 12, 2015

‘Waliopewa ubunge upinzani wakiwa CCM ni mamluki’

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema viongozi wa jumuiya zake walioteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika ubunge wa Viti Maalumu, walikuwa mamluki na maharamia kwa kukiuka kiapo cha chama.

Aidha, kimeeleza kuwa uteuzi wa kumpata mgombea ubunge wa chama hicho katika Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, utafanyika leo baada ya kumalizika kwa kura za maoni juzi.

Wabunge hao wateule wa Chadema walioteuliwa wakiwa bado wanachama wa CCM ni aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Anna Gideria na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Wilaya ya Iringa Mjini, Risala Kabongo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib alisema wanachama hao wameamua kuondoka na hawaruhusiwi kujishughulisha tena na chama hicho.

Khatib alisema wanachama na viongozi hao walikuwa mamluki na maharamia wakati wa kampeni na kukiuka kiapo cha chama walichoapa kuwa wanachama waaminifu na kulinda siri za chama. “Katika kiapo cha wanachama wa CCM walikula kiapo cha kuwa waaminifu kwa chama, lakini wamekiuka isipokuwa kama wameamua kuondoka hatuwezi kuwazuia,” alieleza Khatib.

Alisisitiza kuwa tangu mwaka 1992 nchi ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi, wamekuwa wakiondoka wanachama wake na kwenda upinzani hivyo chama hakitatereka na uharamia waliufanya.

Wabunge hao wawili waliteuliwa na Chadema kuwa wabunge wa kuteuliwa wanawake katika nafasi tano alizopewa mgombea urais wa chama hicho, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alikaririwa na gazeti moja la jana akisema katika nafasi hizo za Lowassa waliingizwa wateule wanne waliomsaidia kwenye kampeni ambao ni Dk Sware Semesi, Gideria, Kabongo na aliyepata kuwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais –Utumishi na Makamu wa Rais, Ruth Mollel.

Akizungumzia uteuzi wa Jimbo la Ludewa, Khatib alisema baada ya kumalizika kwa kura ya maoni, matokeo yatapelekwa katika Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa ajili ya uteuzi utakaofanyika leo.

No comments:

Post a Comment