TTCL

EQUITY

Thursday, November 12, 2015

Rais Magufuli asikika, MRI Muhimbili yatengamaa

MASHINE ya MRI iliyokuwa imeharibika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), sasa imeanza kufanya kazi baada ya kukamilika kwa matengenezo yake.

Utengenezaji wa mashine hiyo ni utekelezaji wa amri ya Rais John Magufuli aliyoitoa kwa uongozi mpya wa MNH aliouteua, baada ya kutembelea hospitali hiyo hivi karibuni.

Novemba 9, mwaka huu, Dk Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza ya kutembelea hospitali hiyo majira ya mchana na kusikitishwa na taarifa ya kutofanya kazi kwa mashine za CT- Scan na MRI kwa takribani miezi miwili, huku mashine kama hizo zikifanya kazi katika hospitali za watu binafsi.

Rais Magufuli mbali na kuamuru matengenezo ya mashine hizo, lakini pia alivunja Bodi ya Wakurugenzi pamoja na kumuondoa aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, Dk Hussein Kidanto na kumrudisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.

Alimteua Profesa Lawrence Mseru aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), kukaimu nafasi hiyo. Tayari ameripoti kazini juzi. Aidha, Wizara ya Fedha ilitoa kiasi cha Sh bilioni tatu kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo ya haraka mashine hizo na nyinginezo katika hospitali mbalimbali za serikali nchini.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa Hospitali Taifa Muhimbili jana na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha, iliuarifu umma kuwa mashine hiyo ya MRI imeanza kazi.

“Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili inapenda kuutangazia umma kwamba mashine aina Magnetic Reasonance Imaging (MRI) imeanza kufanya kazi majira ya saa tisa alasiri leo (jana),” ilisema taarifa ya Aligaesha.

Mashine hiyo imefanyiwa matengenezo na mafundi wa Philips na hutumia sumaku kupiga picha badala ya mionzi na picha zake zina ubora zaidi ya picha zilizopigwa kwa kutumia mashine ya CT-Scan.

“Tunapenda kuutangazia umma kuwa jitihada zinaendelea kuhakikisha mashine ya CT-Scan inatengenezwa. Taarifa zaidi kuhusu matengenezo ya CT-Scan tutawapatia kesho (leo) Alhamisi Novemba 12, 2015 majira ya saa nane mchana,” alieleza msemaji huyo wa Muhimbili.

Katika taarifa yake ya kuvunja Bodi na kumteua Profesa Mseru iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Magufuli aliuagiza uongozi wa Muhimbili ndani ya wiki moja mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ziwe zinafanya kazi na ziwe zinahudumia wananchi inavyopaswa.

No comments:

Post a Comment