TTCL

EQUITY

Thursday, November 12, 2015

Magufuli kuishangilia Stars mwanzo mwisho

RAIS wa Awamu ya Tano nchini, Dk John Magufuli anatarajiwa kuwa mmoja wa mashabiki watakaoipa nguvu timu ya soka ya taifa ya Tanzania `Taifa Stars’ katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia Urusi 2018 dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa keshokutwa Jumamosi.
Akizungumza jana ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alisema Dk Magufuli ataongoza watanzania kwenye mechi hiyo na taratibu zote zimekamilika. “Rais Dk Magufuli amekubali kuja kwenye mechi kuungana na watanzania wengine, labda kama atapata dharura nyingine za kiofisi, lakini tunatarajia atahudhuria,” alisema.
Aidha, Sadiki alitumia nafasi hiyo kumwalika Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuhudhuria mechi hiyo pia ili kuwapa hamasa wachezaji. Kikwete juzi alizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kusema kama Stars itahitaji ushindi dhidi ya Algeria haina budi kujituma.
Katika utawala wake, Kikwete alikuwa akihudhuria mechi za timu ya taifa mara kwa mara, huku Serikali ikibeba jukumu la kulipa mishahara ya jopo la makocha wa timu za taifa za michezo mbalimbali. Endapo Dk Magufuli atahudhuria pambano hili, itakuwa mara yake ya kwanza kujitokeza kwenye shuguli za michezo tangu alipoapishwa wiki iliyopita.
Rais huyo ni mpiga ngoma mzuri. Wakati huo huo, kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema wamejipanga kuifunga Algeria keshokutwa. Timu hiyo iliyokuwa Afrika Kusini kwa kambi ya siku 10 imerejea jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya kupanda ndege kurejea Dar es Salaam Mkwasa alisema anafahamu wanakutana na timu ngumu na bora kisoka, lakini kwenye soka lolote linaweza kutokea.
Alisema katika kambi ya Afrika Kusini amerekebisha makosa kadhaa aliyoyaona katika mechi zilizopita ikiwemo ya kirafiki dhidi ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya Afrika Kusini iliyochezwa juzi na Stars kulala kwa mabao 2-0.
“Kuna mambo mengi tumerekebisha kama umaliziaji, najua hatuwezi kumaliza mapungufu yote yaliyopo lakini kwa sehemu kubwa tumejitahidi kurekebisha,” alisema. “Si kwamba naidharau Algeria, hapana tunaiheshimu sana, lakini mpira wa siku hizi si kama wa zamani, timu zinajituma kushinda hivyo nasi tutajituma na tumeshajipanga kila mmoja anafahamu jukumu lake,” alisema.
“Tunacheza na wapinzani wetu tukijua fika kwamba mpira wa sasa hauna nyumbani wala ugenini, tumejipanga kupata matokeo mazuri tunajua matokeo mazuri ndiyo yatakuwa silaha yetu kwenye mechi ya marudiano,” alisema.
Aliwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi keshokutwa ili kuwapa nguvu wachezaji katika kusaka ushindi. “Mabadiliko kwenye timu tunayaona… ninachoomba watanzania waje kwa wingi Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi hii wachezaji wakiwaona wamejaa uwanjani wanazidi kuwapandisha morali ya ushindi,” alisema.
Algeria na Tanzania zimeachana kwa mbali kwenye viwango vya ubora vya Fifa vilivyotolewa Novemba 5 mwaka huu ambapo Algeria ni ya 26 na Tanzania ikishika nafasi ya 135 duniani.

No comments:

Post a Comment